NA KHALFAN SAID, SABASABA
Meja Jenerali (mstaafu) wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Farah Abdi Mohammed, amesifu ubora wa bidhaa zinazozalishwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) wakati alipotembelea
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere, maarufu Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam Juni 29, 2022.Meja Jenerali (mstaafu) Farah, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo linaloendelea kukua kwa kasi, aliyasema hayo wakati alipotembeela banda la Suma JKT ili kujionea jinsi watendaji wa taasisi hiyo wanavyowahudumia wananchi wanaofika kwenye banda hilo.
Baadhi ya shughuli zinazotekelezwa na SUMA JKT ni pamoja na Viwanda, Biashara, Ujenzi na Uhandisi, Kilimo na Ufugaji.
Baadhi ya bidhaa zilizowekwa katika maonesho hayo ni pamoja na zitokanazo na mazao ya misitu kama vile samani za ofisini, shule na nyumbani, asali, vifaa vya kilimo, bidhaa za ngozi kama vile viatu, mazao ya mifugo kama vile kuku na mayai na ufugaji wa samaki.
Akiwa katika banda hilo, Meja Jenerali (mstaafu) Farah, alipokelewa na Mkurugenzi Msaidizi wa SUMA JKT, anayeshughulikia Operesheni na Utawala, Kanali Shija Lupi ambaye alimpitisha kwenye maeneo mbalimbali ya shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa SUMA JKT, anayeshughulikia Operesheni na Utawala, Kanali Shija Lupi, alisema Shirika la SUMA JKT litaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha sekta ya kilimo inazidi kukua ili nchi izidi kupata mapato yatokanayo na shughuli za uzalishaji zitokanazo na kilimo.
Alisema SUMAJKTinashiriki katika maonyesho hayo ili kuwapa fursa wananchi na washiriki wengine kwa ujumla wao kuona bidhaa mbalimbali katika sekta za kilimo, ufugaji, viwanda, biashara na huduma.
No comments:
Post a Comment