Pages

Tuesday, May 3, 2022

Nauli mabasi ya mikoani zapaishwa kabla ya muda

nauli pic

By Emmanuel Msabaha
By Juma Issihaka

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza mabadiliko ya nauli kwa mabasi ya mikoani na mijini ambayo utekelezaji wake

unatakiwa uanze baada ya siku 14 kuanzia juzi, mawakala wa baadhi ya mabasi hayo wamesema wameshaanza kutumia viwango hivyo wiki mbili zilizopita kabla ya tamko la kupandisha.

Latra juzi ilitangaza ongezeko la nauli hizo baada ya maombi ya muda mrefu la wadau wa usafirishaji wakitaka ziendane na ongezeko la bei ya mafuta na gharama nyingine za uendeshaji.

SOMA: Latra yatangaza nauli mpya za mabasi, daladala

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema katika mabasi ya mikoani daraja la kawaida abiria atatozwa Sh41.29 kutoka 39.89 kwa umbali wa kilomita moja, sawa na ongezeko la Sh4.4 au asilimia 11.92.

Kwa daraja la kati, alisema abiria atatozwa Sh56.88 kwa kilomita moja badala ya Sh53.22. Kiwango kilichoongezeka ni Sh3.66 sawa na asilimia 6.88, huku katika barabara za vumbi zikitajwa Sh51.61 kwa kilomita moja.

Kwa mujibu wa mawakala wa baadhi ya mabasi waliozungumza na Mwananchi katika Stendi ya Magufuli jana, viwango hivyo vilivyotangazwa na Latra walishaanza kuvitumia kabla ya tamko la mamlaka hiyo.

Tito Juma, wakala wa basi moja linalofanya safari za Dar es Salaam kwenda Dodoma, alisema ni wiki ya pili sasa wanatoza Sh26,000 kwa safari hiyo badala ya Sh24,000.

“Siku mafuta yalipopanda na sisi tulipandisha bei siku ileile, tuliwasilisha maombi kwa Latra, jana (juzi) ndiyo wamejibu na kutoa taarifa hiyo, kwa maana tungewasubiri tungeendelea kuumia. Tumejiongeza,” alisema.

Alisema hawakuwa na chaguo zaidi ya kuongeza nauli na ni vigumu kusubiri siku 14, kwa kuwa katika biashara ya usafiri muda huo ni hasara kubwa.

“Utasubiri siku 14 wakati huo unamwambia nini mmiliki, yeye anataka faida, wewe wakala fanya utakavyoona sahihi umpelekee fedha,” alisema.

Augostino Manga, wakala wa basi jingine linalofanya safari za Dar es Salaam kwenda Dodoma, alisema si rahisi wasafirishaji wote wanaofanya safari zinazofanana wapandishe nauli, kampuni yake isifanye hivyo.

“Wenzio wote wameongeza baada ya mafuta kupanda wewe utaendelea kutoza nauli ya zamani watakufikiriaje, unafanya kuendana na wenzako wanavyokwenda, hata hivyo ndiyo bei inayotupa faida,” alisema.

Hata hivyo, alisema idadi ya abiria kwa sasa ni kubwa hasa kuelekeza sikukuu ya Eid el Fitr

Abiria wa Dar es Salaam kwenda Kilosa mkoani Morogoro, alisema ametozwa Sh16,000 badala ya Sh13,000 alizokuwa anatozwa awali.

“Hawakubembelezi kama hutaki wanakwambia tafuta gari lingine, kwa ufupi hiyo ndiyo nauli tunayolipa haijaanza leo (jana) na kwenye tiketi wanaandika kabisa,” alisema.

Atieno Emmanuel, msafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, alisema nauli aliyotozwa ni Sh10,000 badala ya Sh9,000.

“Nimempa Sh9,000 ameniambia nikatafute gari la nauli hiyo nikipata niende nalo na tangu saa 12 asubuhi hadi sasa (saa 6 mchana) sikupata gari,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema wanaotumia nauli zilizotangazwa na Latra kwa sasa ni kinyume na sheria.

Alieleza kuwa mamlaka ilishatoa kauli inayofafanua lini viwango vipya vya nauli vinapaswa kutumika, wanaovitumia sasa wanapaswa kuchukuliwa hatua.

Akizungumzia hilo, Ngewe alisema suala la watoa huduma kupewa siku 14 ndiyo waanze kutoza nauli mpya ni la kisheria.

“Sheria inawataka kabla ya kutoza nauli mpya wampe taarifa abiria ndani ya siku 14 na katika kipindi hicho nasi tutachapisha katika gazeti la Serikali,” alisema.Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa tayari imetumwa timu ya watumishi wa Latra katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa ajili ya kutoa elimu na kudhibiti utozaji wa kiwango hicho cha nauli mpya.

“Tayari jioni hii (saa tisa alasiri) kuna watu wamekwenda Magufuli Stendi kutoa elimu kwanza kuhusu viwango vipya vya nauli, pia kuonya yeyote atakayepandisha nauli sasa kabla ya muda uliopangwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Chama cha ACT Wazalendo, kimetoa taarifa ya kusikitishwa na uamuzi wa Latra kupandisha nauli, kikisema uamuzi huo haujazingatia mzigo mkubwa wanaobebeshwa wananchi.

“Ni dhahiri kuwa ongezeko la nauli za usafiri wa mabasi na daladala zinaenda kuongeza athari kwa wananchi kwa kwenda kupandisha gharama za maisha maradufu na kuongeza kasi ya mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu nchini,” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment