Pages

Friday, April 1, 2022

WATAALAM WA MAJENGO NA MAJENZI WAASWA KUHUSU UMUHIMU WA KULIPA KODI

 
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ((Sekta ya Ujenzi), Richard Mkumbo akifungua mafunzo endelevu kwa Wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi (AQRB), (hawapo pichani) Jijini Dodoma.



Msajili wa Wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi (AQRB), Arch:Edwin Nnunduma, akizungumza na baadhi ya wakandarasi wakati wa ufunguzi wa mafunzo endelevu kwa wabunifu wa majengo na wakadiliaji majenzi yaliyofanyika jijini Dodoma.

  

Baadhi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kutoka mikoa mbalimbali wakimsikiliza mgeni rasmi Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Richard Mkumbo, (Hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wataalam hao, yaliyofanyika katika ukumbi wa St Gaspar, Jijini Dodoma.

………………………………………..

Imeelezwa kuwa ulipaji kodi kwa kuzingatia miongozo iliyopo kutoka kwa mwa wadau na wataalam wa sekta ya ujenzi ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa uchumi wa nchi hali itakayopunguza utegemezi kutoka nje ya nchi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu Bw. Richard Mkumbo wakati akifungua mafunzo endelevu ya Wataalam wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa niaba ya katibu Mkuu wa sekta hiyo jana Jijini Dodoma na kusisitiza pamoja na kodi hizo Serikali inawekeza nguvu katika kushirikishwaji wa sekta binafsi ili kukuza sekta hiyo.

Mkumbo amesema kuwa pamoja na mambo mengine Kikao hicho kitajikita katika masuala yanayojitokeza kwenye Sheria ya Kodi hususani katika Sekta ya Ujenzi, malipo ya kodi kwa njia ya kielektroniki na kujaza fomu za ushuru zitakazowasilishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Kwa siku mbili hizi kupitia mafunzo haya, nina Imani tutatoka hapa na michango itakayosogeza sekta ya ujenzi mbele na lengo ni kuhakikisha kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi unabadilika kwa kasi kubwa’amesema Katibu Mkuu Mkumbo.

Mkumbo ameongeza kuwa katika suala la kuvutia uwekezaji na kudhibiti kodi za serikali katika sekta ya ujenzi Serikali inaendelea kuhakikishakuwa inafanya maboresho hususani kwenye eneo la misamaha ya Kodi la Ongezeko la Thamani (VAT)

Aidha, Mkumbo amewasihi wataalam wote kuzingatia na kutoa kipaumbele kwa Sheria na Kanuni za Kodi wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwani shughuli za ujenzi zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Ukuuaji wa 2020, shughuli za ujenzi zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwa asilimia 27.5, zikifuatiwa na kilimo kwa asilimia 25.8, usafiri na uhifadhi asilimia 13.6 na shughuli za uzalishaji viwandani asilimia 7.8.



Awali akiwasilisha taarifa ya bodi Mbunifu Majengo Edwin Nnunduma, amesema kuwa toka mwaka 2003 Bodi imejipangia ratiba za kuendesha Semina za Mafunzo Endelevu (Continuing Professional Development – (CPD)) kwa lengo la kuwanoa Wataalam waliosajiliwa na Bodi ili kuwawezesha kuendana na maendeleo au mabadiliko ya Sheria, Kanuni, Sayansi na Teknolojia yanayotokea Ulimwenguni.

Aidha, aliongeza kuwa mada zitakazowasilishwa zina lengo la kuwakumbusha Wataalam hao umuhimu wa kufuata na kuzingatia Maadili na Utawala Bora katika ulipaji wa Kodi za Serikali.

Mbali na hayo Mbunifu Majengo Edwin Nnunduma, amesema kuwa Bodi imefanikiwa kuboresha utaratibu wa kusajili Wataalam na Miradi kwa kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Bodi ujulikanao ‘Online Registration System (ORS) ambao utasaidia wataalam wanaotaka kujisajili au kusajili miradi wanawasilisha nyaraka zao kwa njia ya Mifumo ya Mitandao bila kufika kwenye ofisi za Bodi.

“Maboresho yaliyofanyika katika mfumo huu ni rahisi na wa Kisasa, kwani humuwezesha Mtaalam kuwasilisha nyaraka akiwa mahala popote ambapo anaweza kupata huduma za mtandao” amesema Nnunduma.

Aidha, amesema kuwa hadi kufikia Februari, 2022 Bodi imesajili jumla ya Wataalam 1,377 na kusajili Kampuni za Kitaalam 486. Aidha jumla ya wataalamu 132 na kampuni 72 wamefutiwa usajili kutokana na makosa mbalimbali ya kitaalamu.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika jijini Dodoma kwa kuwakutanisha wataalam zaidi ya 300 kupata uzoefu, kujadili na kutafuta suluhu za changamoto mbalimbali zinazowakuta.

No comments:

Post a Comment