Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akisalimiana na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Mikopo kwenye Sekta Binafsi, Kanda ya Afrika (International Finance Corporation-IFC), Bw. Sergio Pimenta, baada ya mazungumzo yaliyolenga kuisaidia sekta binafsi nchini Tanzania, mazungumzo hayo yalifanyika Washington DC, Marekani, wakati wa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.
Katibu Mkuu Wizara ya Fefdha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akiwa katika mkutano na uongozi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji mikopo kwenye Sekta Binafsi (IFC), Jijini Washington DC, Marekani. Kushoto ni Kamishna wa Idara ya Fedha na Mipango, Bi Sauda Msemo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC)
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
TANZANIA inatarajia kupata dola za Marekani milioni 200 sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 460 kutoka Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake inayoshughulika na utoaji wa mikopo na misaada kwenye Sekta Binafsi – International Finance Corporation (IFC), kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia sekta binafsi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa Taasisi inayoshughulika na utoaji mikopo na misaada kwenye Sekta Binafsi (International Finance Corporation-IFC), Kanda ya Afrika, Bw. Sergio Pimenta, Jijini Washington DC, Marekani.
Bw. Tutuba alisema kuwa fedha hizo zittumika kuendeleza shughuli za uzalishaji kwenye viwanda, maendeleo ya tehama na kusaidia miradi ya wanawake, wenye ulemavu na vijana kupitia taasisi mbalimbali za fedha.
Alisema kuwa uwekezaji wa Benki ya Dunia kwenye Sekta binafsi kupitia IFC umefikia dola milioni 282 kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji na kwamba kiasi hicho cha nuongeza kitasaidia kuimarisha sekta binafsi na kuimarisha shughuli za uzalishaji na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini Tanzania.
“Serikali imewasilisha miradi mbalimbali kwenye Taasisi hii ya Benki ya Dunia inayosaidia Sekta Binafsi ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia nne ya kuanzia Dar Es Salaam-Chalinze hadi Dodoma, ujenzi wa hoteli na maduka ya kisasa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere-Dar es Salaam, pamoja na miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo tunataka itekelezwe kwa njia ya ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma” alisema Bw. Tutuba.
Aidha, Bw. Tutuba alisema kuwa Taasisi hiyo ya Benki ya Dunia imesema iko tayari kuhamasisha wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia kwenda kuwekeza nchini Tanzania kupitia sekta za nishati ya umeme jua, upepo na joto ardhi Pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa Somanga Fungu unaotarajiwa kuzalisha megawati 320 za nishati ya umeme kupitia ubia katia ya Sekta binafsi na Umma.
“Mafanikio haya ni matokeo ya mkutano kati ya Me. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa IFC, Bw. Makhtar Diop, wakati wa ziara yake aliyoifanya nchini Tanzania mwezi Februari 2022, ambapo alimwomba Kiongozi huyo kuisadia sekta binafsi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa: alisema Bw. Tutuba.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utasaidia kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye thamani za shilingi trilion 114.8 ambao umeainisha kuwa asilimia 40 ya utekelezaji wa mpango huo sawa na shilingi trilioni 40.6 zinatakiwa kutoka katika sekta binafsi huku asilimia 60 ya gharama za mpango huo sawa na shilingi trilioni 74.2 zinatakiwa kutoka Serikalini
Katika hatua nyingine, kwa mara ya kwanza, Tanzania inatarajia kuwa nchi ya kwanza kunufaika na hati fungani mpya ya usawa wa kijinsia (Gender Bond) itakayozinduliwa na Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake inayoshughulika na utoaji wa mikopo na misaada kwenye sekta binafsi, ambapo kiasi cha dola za Marekani milioni 10 sawa na shilingi bilioni 24 kinatarajiwa kukusanywa na zitakazotumika kuwakopesha wajasiliamali kupitia Benki ya NMB.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia wa Taasisi inayoshughulika na utoaji mikopo na misaada kwenye Sekta Binafsi (International Finance Corporation-IFC), Bw. Sergio Pimenta, alisema kuwa Hati Fungani hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza na Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kunufaika nazo katika Bara la Afrika.
Aidha, Bw. Pimenta aliipongeza Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha sekta binafsi na kuahidi kuwa Taasisi yake imekusudia kuongeza fedha zaidi ili kusaidia mipango ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya wananchi wake kupitia uwekezaji kwenye sekta za kilimo biashara, nishati, ujenzi wa miundombinu na kuwasaidia wajasiriamali kufanya biashara.
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mkurugenzi anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki wa Taasisi hiyo ya IFC, Bi. Jumoke Jagun-Dokunmu.
No comments:
Post a Comment