Arusha. Rais Samia Suluhu ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika safari yake
nchini Marekani, ikiwepo kusaini mikataba na wawekezaji yenye thamani ya Sh11.7 trilioni.Akizungumza leo Alhamisi April 28, 2022 baada ya kuwasili nchini na ndege ya Qatar airways katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Samia amewataka Watanzania kujiandaa kuwapokea wawekezaji hao wakija nchini.
Rais Samia ambaye leo anazindua filamu ya Royal Tour jijini Arusha, amesema wawekezaji hao kama wakija nchini, wanatarajiwa kutoa ajira kwa watu 301,000.
"Naomba wakija tusiwasumbuwe, tumefanikiwa kiasi na wakija tutoe ushirikiano," amesema.
Amesema wakiwa nchini Marekani walionana na Meya wa mji wa Dallas aliyeahidi kuanzisha urafiki na majiji ya Dar es salaam, Mwanza na Arusha, akisema pia katika urafiki huo watatazama uwezekano wa kuwa na usafiri wa ndege moja katika nchi hizo mbili.
Katika ziara hiyo Rais Samia pia amesema walifanikiwa kukutana na watendaji wa taasisi ya SC Johnson Institute ambaye imekuwa ikisaidia taasisi ya utafiti wa wagonjwa ya binaadamu(NIMR) taasisi ya kupambana na Malaria ya Ifakara na Kituo Cha utafiti wa wadudu Tanga na imeahidi kuendelea kusaidia taasisi hizo vifaa na ukarabati.
Amesema pia itasaidia kupambana na Malaria katika mikoa mitano nchini ambayo ni Ruvuma, Katavi, Geita, Kagera na Kigoma ambapo watasaidia ujenzi vituo vya afya 200.
Kuhusu sekta ya utalii amesema baada ya kuathirika na Uviko-19 sasa watalii wameanza kuongezeka sambamba na mapato.
Amesema watalii wameongezeka kutoka 620,866 mwaka 2020 hadi 922,692 mwaka 2021 na mapato kutoka dola 714 milioni hadi dola 1,254 milioni mwaka 2021.
No comments:
Post a Comment