Pages

Wednesday, April 27, 2022

NIC Kutoa Gawio Kwa Serikali

Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la  Taifa la Bima (NIC) Dk.Elirehema Doriye akizungumza  na  waandishi wa habari kuhusiana mafanikio ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam,Kushoto ni Msajili wa Hazina Mgonya Benedicto.
Msajili wa Hazina Mgonya Benedicto (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika Shirika la Taifa la Bima (NIC) kuhusiana na maendeleo ya Shirika hilo pamoja na kutoa gawio kwa Serikali jijini Dar es Salaam kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi wa NIC Laston Msongole watatu kutoka kushoto ni Mkurugezi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Bima (NIC) Dk.Elirehema Doriye.
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Taifa la Bima (NIC) Laston Msongole akizungumza kuhusiana na mafanikio ya Shirika hilo kwa miaka minne mfululizo jijini Dar es Salaam.

*Msajili wa Hazina aipongeza NIC kwa kupunguza matumizi yasio ya Ulazima

*Dk.Doriye aahidi kwenda kwa kasi zaidi kwa kuboresha mifumo mbalimbali ya kuzaa tija

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) ni miongoni mwa mashirika ya umma linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa lengo la kutoa huduma za bima nchini.

NIC ni shirika kongwe ambalo limepitia changamoto kadhaa ikiwemo ile ya kuwekwa katika orodha ya mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa kotokana na kushindwa kujiendesha kwa faida.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita NIC imeonesha uwezo wa kujiendesha kwa faida kutokana na usimamizi bora wa utendaji pamoja na kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia ya habari na mawasiliano hali iliyochangia kukua kwa shirika hili na hata kuzalisha faida ambayo sasa inakwenda kutoa gawio Shilingi bilioni 1.5 kwa serikali.

Katika kutoa gawio hilo, faida nyingine ya shilingi Bilioni 12.05 inakwenda kuongeza nguvu kwenye mtaji wa shirika. Kuongezeka kwa mtaji huo kunaifanya NIC kuwa shirika lenye mtaji mkubwa kuliko kampuni nyingine za bima nchini.

Katika mazungumzo ya Msajili wa Hazina, Wafanyakazi wa NIC pamoja na Mwenyekiti wa Bodi Laston Msongole, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Dk.Elirehema Doriye amesema kuwa shirika hilo kwasasa liko katika ushindani wa soko tofauti na hapo nyuma lilipoanzishwa kutokana na kutoa huduma bora za Bima.

Amesema Shirika kwa mtaji wa nyongeza wa Sh.bilioni 12.05 wanakwenda kuongeza uwezo wa shirika na kuimarisha mifumo mbalimbali ya kurahisisha kutoa huduma katika viwango bora.

Dk. Elirehema Doriye amesema licha ya mafanikio hayo ya miaka minne bado hajaridhika kwani anaamini shirika lina kila sababu ya kuwa na mafanikio zaidi ya hayo kama litaendelea kuweka mikakati madhubuti pamoja na kujipanga vizuri kama timu ya mpira ili kufika sehemu ambayo kila mtu atazungumzia huduma za Bima za NIC.

"Nia yetu kama wafanyakazi ni kuona adhima ya serikali ya kuanzisha shirika inatimia tena kwa kuleta faida ya kuhudumia wananchi pamoja na kuisaidia serikali katika utekelezaji wa miradi na huduma mbalimbali za maendeleo"amesema Dk. Elirehema

Aidha, Dkt Doriye, amesema ndoto yake ni kuiona NIC inakuwa Shirika bora kutokana na ubunifu wa wafanyakazi katika utoaji huduma mbalimbali pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

Dk. Doriye ameenda mbali zaidi kwa kulitaka shirika kuongoza Taasisi zote katika kutoa gawio kubwa kwa serikali kwasababu jamii ndiyo mnufaika.

Shirika la Bima la Taifa (NIC) limetoa gawio la Sh.Bilioni 1.5 kwa Serikali baada ya kuendelea kufanya vyema kwa miaka minne mfululizo na kuweza kupata faida ambayo itasaidia kusukuma miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile maji, barabara, afya, nishati na hata reli ya kisasa.

Mkurugenzi Mtendaji huyo Dk. Elirehema Doriye amesema moja kati ya mambo ambayo wamepiga hatua kubwa ni kuwahudumia wateja wa bima kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. Kwa mfano, kwa sasa NIC wanalipa madai ya mteja aliyekamilisha nyaraka zote stahiki ndani ya siku 7. Hakuna kampuni yoyote ya Bima nchini inayolipa madai kwa uharaka huu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NIC, Laston Msongole amesema kwa kipindi cha miaka minne mfululizo iliyopita na kwa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali (CAG), NIC inayonesha kufanya vizuri na kutengeneza faida kubwa.

“Kwa miaka minne mfululizo inayoishia Juni, 2021, Shirika limekuwa na maendeleo ya kuvutia kwa kutengeneza faida inayokua kila mwaka na hilo linathibitishwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG)”. Amesema

Mwenyekiti wa Bodi wa NIC Bwana Msongole ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2018, Shirika lilipata faida ya bilioni 3.63, mwaka uliofuatia ambao ni 2019 likapata bilioni 7.79, wakati mwaka 2020 likapata bilioni 33.65 na mwaka unaoishia Juni,2021 wamepata bilioni 73.1 hivyo Shirika limeendelea kuongeza faida kila kukic.

Aidha Msongole amesema kuwa matarajio yao kufikia Juni 2022 kwa maana ya hesabu zilizokaguliwa NIC itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya hii ya sasa.

Pamoja na hayo amesema kwa mafanikio hayo waliyoyapata wanatarajia kutoa gawio kwa Serikali ili kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea nchini.

Katika hatua nyingine Msajili wa Hazina Mgonya Benedicto amesema Shirika hilo limejiweka vizuri katika kudhibiti matumizi yasiyo na tija na wakati huohuo limeendelea kujenga imani kwa watanzania ambao hivi sasa wanaokata bima kwenye shirika hilo.

Ameeleza kuwa katika majadiliano yao kupitia mahesabu ya shirika, ile faida ambayo imepatikana sehemu wameamua kuimarisha mtaji wa Shirika ambapo sasa utaiwezesha kufanya biashara kwa ufanisi na katika mazingira mazuri kiushindani ukilinganisha na hapo awali. Vilevile wamekubaliana sehemu nyingine ipelekwe kwenye mfuko wa serikali kama gawio kwa serikali ambaye ndiye mmiriki kwa asilimia 100.

No comments:

Post a Comment