Na Mwandishi Wetu, Lushoto
WAFANYABIASHARA 6 waliokua wakiwahi gulio wilayani Handeni, wamefariki dunia papo hapo na wengine 7 kujeruhiwa vibaya baada ya gari aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria kuacha njia alfajiri ya jana na kupinduka katika korongo katika barabara ya Soni-Mombo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Ajali hiyo ilihusisha Fuso hiyo yenye namba za usajili T 239 AFD lililokuwa limebeba watu pamoja na bidhaa zao kama nyanya, vitunguu, makabichi, Matunda aina ya Peasi na nyombo vya nyumbani, kupinduka baada ya kufeli breki.
Mashuhuda wa ajali hiyo iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, ACP Safia Jongo wanasema Fuso lilishindwa kupunguza mwendo kwenye mteremko mkali wa eneo la Kijiji Cha Nyasa baada ya breki zake kufeli na hivyo kutumbukia kwenye korongo lenye mteremko mkali kwa chini kiasi cha mita 150 za mraba.
Akizungumza kwa simu kutokea kwenye eneo la ajali Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga Safia Jongo alisema taarifa za awali ziliomesha watu 4 ndio waliopoteza maisha papo hapo kwenye ajali na baadaye watu wengine wawili walifariki wakikimbizwa kituo Cha Afya kilichopo Mombo wilayani Korogwe.
"Waliotutoka mwanzoni tukipata taarifa, walikuwa wanne, wakaongezeka majeruhi wawili na jumla kufikia 6 ambapo kati yao waliofariki wanaume ni 4 na wanawake ni wawili, "alisema Kamanda Jongo.
Kamanda aliwataja watu waliofariki, kuwa Juma Mustafa Mohamed mkazi wa Handeni, Mwajuma Hatibu mkazi wa Handeni, Jumanne Adam mkazi wa Soni, Mohamed Said Makakala mkazi wa Handeni mjini, Zaina Ramadhani mkazi wa Handeni Kwa mkono, huku mtu wa 6 akiwa bado hajajulikana jina lake.
Aliwataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Rumisha Zuberi Msagati mkazi wa Bumbuli wena, Rasuli Said Makalala mkazi wa Handeni Komwale, Mussa Enock Kajia mkazi wa Lukozi mjini, Amina Zuberi Mhina mkazi wa Handeni, Mwajabu Mrisho Mpulizi mkazi wa Handeni Chogo na Mama Latifa mkazi wa Handeni.


No comments:
Post a Comment