Pages

Thursday, March 31, 2022

Tanzania Kuanza Majaribio Ya Chanjo Yake Ya Corona



 Na Amiri Kilagalila,Njombe


Misanga Marko mtafiti na daktari mwandamizi kutoka NIMR Mbeya,amesema nchi ya Tanzania imetengeneza chanjo ya Corona inayotarajiwa

kuingizwa kwenye majaribio huku akibainisha kuwa chanjo hiyo kutolewa kwa njia ya matone ya puani,

Amebainisha hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya ufunguzi wa mdahalo wa afya kuhusu ustahimilivu wa mfumo wa afya wakati wa magonjwa ya mlipuko uliofanyika katika ukumbi wa Johnson Hall mjini Njombe

“Tanzania tumetengeneza chanjo yetu wenyewe (ya Corona) na siku si nyingi tunaingiza kwenye majaribio,kituo cha NIMR Muhimbili na Mbeya ndio kitahusika moja kwa moja na tunatarajia mwezi wa nne tukafungua hatua za mwanzo”alisema Dkt.Misanga Marko

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Waziri Kindamba wakati akifungua mdahalo huo amesema mkoa wa Njombe bado uko chini kitakwimu katika zoezi la kupokea chanjo kwa wananchi.

“Katika mkoa wetu wa Njombe mpaka sasa wananchi 35,294 sawa na 10% tayari wamekwishapata chanjo ya Corona ingawa lengo letu ni kufikia 70% ya wananchi wenye umri wa miaka 18 ili waweze kupata chanjo hiyo” alisema Waziri Kindamba RC wa Njombe

Aidha amesema wakati akiapishwa hivi karibuni kuwa mkuu wa mkoa huo alipewa maelekezo na Rais juu ya hamasa ndogo kwa wananchi katika zoezi hilo na hivyo yuko tayari kuendeleza hamasa kwa wananchi mkoani Njombe ili kuitikia zoezi hilo.

“Mh.Rais alinielekeza kuja kusimamia swala la chanjo katika mkoa wa Njombe kwasababu namba bado ziko chini.Kwa hiyo nichukue fursa hii ya kuhamasisha kupata Chanjo wakati tunakwenda kusheherekea uzinduzi wa mbio za Mwenge kitaifa” alisema Waziri Kindamba RC wa Njombe

Naye mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza na kupokea chanjo katika maeneo yao kwa kuwa chanjo ya Corona ni salama tofauti na baadhi ya watu wanavyopotosha.

“Watu wasipochanja (Chanjo ya Corona) tutapoteza nguvu kazi kwenye nchi yetu kwasababu Corona inaua,tunawashukuru wadau wetu kwa kutuunga mkono katika kuhamasisha Chanjo kwa kuwa bado tupo chini kwenye takwimu” Kissa Kasongwa DC wa Njombe.


No comments:

Post a Comment