Pages

Tuesday, March 1, 2022

SADC YAZINDUA KITUO CHA UGAIDI DAR ES SALAAM

 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akihutubia wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kupambana na ugaidi cha SADC jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Kazi, Ajira, Tija, na Ukuzaji wa Ujuzi wa Botswana, Mhe. Machana Ronald Shamukuni, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe. Maledi Pandor wakizindua rasmi kituo cha Kupambana na ugaidi cha SADC


Waziri wa Kazi, Ajira, Tija, na Ukuzaji wa Ujuzi wa Botswana, Mhe. Machana Ronald Shamukuni, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe. Maledi Pandor akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha SADC jijini Dar Es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi wakiweka saini Makataba wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha SADC


Baadhi ya Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha SADC

Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeishukuru Tanzania kwa kujitolea kuwa Mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na

Ugaidi ambacho kimezinduliwa rasmi tarehe 28 Februari 2022 jijini Dar Es Salaam.


Kituo hicho kimefunguliwa na Waziri wa Kazi, Ajira, Tija, na Ukuzaji wa Ujuzi wa Botswana, Mhe. Machana Ronald Shamukuni, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe. Maledi Pandor.

Katika hotuba yake, Mhe. Shamukuni alisema kuwa kujitolea kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kituo hicho ni kudhihirisha namna nchi hiyo wakati wote, tokea enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere imekuwa na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa suala la usalama katika kanda linapewa kipaumbele.

Alibainisha kuwa kituo hicho ni cha kwanza na cha aina yake katika Jumuiya za Kikanda barani Afrika. Hivyo, kitakuwa muhimu katika kuratibu masuala ya upatikanaji wa habari za kitelejensia, kubadilishana uzoefu na kutoa ushauri wa namna ya kuandaa Sera na programu za kukabiliana na kuzuia ugaidi baina ya nchi wanachama wa SADC.

Mhe. Shamukuni alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa wakati ufunguzi wa kituo hicho unafanyika, nchi za SADC zimeshatuma tayari kikosi cha kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyotokea katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji. Amekitaja kitendo cha kutuma kikosi hicho ni ishara ya dhati ya nchi wanachama ya kuhakikisha kuwa zinakabiliana na vitendo vya ugaidi na kuvikomesha kabisa katika kanda ya SADC.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Stergomena Tax (Mb) alieleza kuwa matishio ya kigaidi ni suala linalohitaji kushughulikiwa kwa nguvu zote, na kwa ushirikiano bila ya kupepesa macho, na kuwasihi wanachama wa SADC kuikabili changamoto ya ugaidi kikamilifu.

Alieleza kuwa ugaidi si vita ya kawaida, ambapo adui anaonekana kwa uwazi kwa sababu baadhi ya wafuasi wa vikundi vya ugaidi ni sehemu ya tunaoishi nao na vitendo vyao vimesababisha madhara ya kiuchumu, kijamii na kiusalama kwa raia wasio na hatia.

Alimalizia kwa kuainisha kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuanzia mwaka 2007 hadi 2016, Bara la Afrika limepoteza Dola za Marekani bilioni 119 kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ugaidi, hivyo, nchi za Afrika endapo zitashirikiana ipasavyo kukomesha vitendo hivyo, fedha nyingi zitaokolewa na kutumika kwa ajili ya mipango ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Hafla ya ufunguzi wa kituo hicho ilihitimishwa kwa uwekaji saini wa Mkataba wa Uenyeji ambao kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula na kwa upande wa SADC ulisainiwa na Katibu Mtendaji, Mhe. Elias Magosi. 

No comments:

Post a Comment