Meneja Usimamizi wa Mafao wa NSSF, James Oigo, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu zoezi la uhakiki wa wastaafu na wategemezi. Kulia ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele na Kushoto ni Meneja Malipo ya Pensheni wa NSSF, Nancy Mwangamila.
Na Mwandishi Wetu,
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanza rasmi zoezi la uhakiki wa wastaafu na wategemezi wanaolipwa pensheni ya kila mwezi, huku ukiwataka walengwa kufika na nyaraka nne muhimu ili kufanikisha zoezi hilo.
Akizungumzia utaratibu wa zoezi hilo la uhakiki ulioanza leo ( Februari 1, 2022) hadi Aprili 29, 2022, Meneja Pensheni wa NSSF, Nancy Mwangamila amesema mstaafu anatakiwa kufika na nyaraka muhimu ambazo ni kitambulisho cha NSSF au kuponi, kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, picha moja ndogo ya sasa ya rangi na kwa wategemezi (watoto) wafike na cheti za kuzaliwa na kitambulisho cha shule.
Nancy amesema Mfuko umeweka utaratibu mzuri kwa wastaafu wagonjwa au wazee wasiojiweza kwamba taarifa zao zitolewe kupitia barua pepe customercare@nssf.or.tz au wapige simu ya bure 0800116773 ili waweze kuhudumiwa.
Amesema wastaafu wanaohudumiwa na Mfuko hadi kufikia Desemba 31, 2021 wameongezeka na kufikia 24,894 kutoka wastaafu 23,164 waliokuwepo mwezi Juni, 2021 sawa na asilimia 7.47.
Amesema idadi ya wastaafu waliopo katika daftari la pensheni ya kila mwezi wanalipwa wastani wa Shilingi bilioni 8.4 kwa mwezi.
Nancy amesema lengo la uhakiki huo ni kwa ajili ya kuhuisha taarifa za wastaafu ili kupata taarifa sahihi kama sehemu wanazoishi, namba za simu na namba za kitambulisho cha Taifa.
Amesema kwa wastaafu waliopo Zanzibar watahakikiwa katika ofisi zote za ZSSF zilizopo Unguja na Pemba huku wastaafu waliopo Dar es Salaam uhakiki wao utafanyika katika ofisi za mkoa ambazo ni Ilala, Kinondoni na Temeke pia katika ofisi za Wilaya zilizopo Daraja la Mwalimu Nyerere na Mbezi Beach.
Kwa upande wake, James Oigo ambaye ni Meneja Usimamizi wa Mafao wa NSSF, Meneja Usimamizi wa Mafao wa NSSF, James Oigo, amesema zoezi la uhakiki wa wastaafu na wategemezi wanaolipwa pensheni ya kila mwezi limeanza rasmi tarehe 1 Februari, 2022 hadi Aprili 29, 2022.
Oigo amesema zoezi hilo la uhakiki ni muhimu kwa sababu Mfuko unapata taarifa sahihi za wastaafu na wategemezi wake na kuuwezesha kuendelea kulipa mafao kwa wahusika kila mwezi bila ya usumbufu wowote pamoja na kuhuisha kanzi data zake.
Amesema zoezi hilo litafanyika kila siku Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 10:30 jioni kwenye ofisi zote za NSSF za mikoa na kwamba moja kati ya malengo makuu ya Mfuko ni kutoa mafao ya muda mrefu ambayo ni ya pensheni na mafao ya muda mfupi.
Oigo amefafanua kuwa mafao ya pensheni yanatolewa kwa wanachama waliofikia umri wa kustaafu ambao ni miaka 55 mpaka 59 kustaafu kwa hiari na miaka 60 kustaafu kwa mujibu wa sheria na awe amechangia katika Mfuko michango isiyopungua ya miezi 180 sawa na miaka 15.
Amesema NSSF pia inatoa pensheni ya ulemavu ambayo hulipwa kwa mwanachama aliyepoteza angalau theluthi mbili (2/3) ya uwezo wa kufanyakazi na awe amepata ulemavu wa kimwili au kiakili kama ilivyothibitishwa na taarifa ya daktari na kwamba pensheni nyingine ni ya urithi ambayo hulipwa kwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki ambao ni mke/mume na watoto walio na umri usiozidi miaka 18 au 21 ikiwa wapo masomoni.
Oigo amesema katika kuwaondoshea usumbufu wastaafu Mfuko umeunda group la ujumbe mfupi wa maneno (SMS) ambazo zimeshaanza kutumwa kwa wastaafu zikiwataka waende kuhakikiwa kwa vipindi tofauti tofauti kwa mfano baadhi ya wastaafu wataanza kuhakikiwa mwezi huu wa Februari, mwezi Machi na kundi la mwisho mwezi Aprili. Hiyo itaondosha msongamano na kuzingatia tahadhari za ugonjwa wa UKIVO 19.
Aidha, Mfuko katika kuendelea kutoa huduma zake kidigitali umekuwa ukitumia mfumo wa kuchukua alama za kidole gumba (Biomentic/ Fingerprint) utaratibu ambao unarahisisha zoezi la uhakiki na kuwa la muda mfupi kwa kuwa mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mfumo wa NIDA ambao una taarifa za wanachama na kufanya zoezi la uhakiki kuwa la muda mfupi endapo mstaafu atakuwa na namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA).
No comments:
Post a Comment