Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
CITI BANK imeahidi kuisaidia Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka katika Benki hiyo pamoja na washirika wake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kuahidi kuwa balozi wa kutafuta wawekezaji wataowekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa wa Benki hiyo anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
“Nafahamu Serikali inauhitaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ukiwemo mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuelekea nchi za Rwanda, Burundi na DRC- Congo, nasi tumeleta andiko letu serikalini, tunataka kusaidia kupatikana kwa fedha kutoka katika taasisi za fedha za kikanda na kimataifa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo uuzwaji wa hatifungani” alisema Bw. Dawodu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo hapa nchini, Bw. Geofrey Mchangila, alisema kuwa Citi Bank imekuwa ikifanya shughuli zake za kibenki hapa nchini kwa zaidi ya miaka 27 na kwamba malengo ya kutaka kufanyakazi na Serikali katika kutafuta rasilimali fedha na kwamba watahakikisha wanatafuta na kutoa mikopo yenye riba nafuu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki hiyo kwa kuwasilisha mapendekezo yake serikalini kuhusu namna ya kufanikisha ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kisasa ambao utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi si tu kwa Tanzania, bali nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ambazo hazipakani na Bahari.
Alieleza kuwa Mkandarasi atakayejenga kipande cha Reli ya Kisasa kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi mkoani Tabora amepatikana na mkandarasi atayejenga reli hiyo kutoka Isaka hadi Mwanza yuko katika eneo la mradi na Mkandarasi atakayejenga reli kuanzia Isaka hadi Tabora atapatikana muda si mrefu kuanzaia sasa.
“Dira ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona kuwa Reli ya Kisasa ya kuanzia Makutopora (Singida) hadi Mpaka Mwanza na kuanzia Tabora hadi Kigoma, ijengwe sambamba na kwa kasi, wakati huohuo Reli ya Kusini mwa Tanzania kutoka Bandari ya Mtwara hadi Mbamba bay kuelekea nchi za SADC zilizoko ukanda huo ziweze kufikiwa na reli hiyo” alieleza Dkt. Nchemba
Aidha, Dkt. Nchemba aliushukuru uongozi wa Benki hiyo kwa kuamua kuwa balozi wa Tanzania katika kutafuta wawekezaji wataowekeza mitaji na teknolojia na kwamba Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza kutokana mambo kadhaa ikiwemo uwepo wa amani na utulivu, uwepo wa soko la uhakika la kikanda pamoja na soko la ndani linalokua kwa kasi.
“Tanzania ina faida kuliko nchi nyingi za Afrika ambapo kijiografia ni lango la zaidi ya nchi 7 ambazo hazina lango la Bahari na uwepo wa amani isiyolinganishwa na nchini nyingi za Afrika ni kivutio cha mwekezaji yeyote na wanaweza kulifikia robo au robo tatu ya soko la Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara” alieleza Dk. Nchemba.
Alibainisha kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya watu hivyo kuwa na soko la uhakika la ndani linalokua kwa kasi na uchumi wake hauyumbi akitolea mfano wakati wa Janga la Uviko-19 ambapo nchi nyingi ziliyumba kiuchumi lakini Tanzania uchumi wake uliendelea kukua kwa kiwango chanya.
Mkutano huo wa Ujumbe wa Citi Bank na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Hassan Chande, Naibu Katibu Mkuu Bw. Lawrence Mafuru, Kamishna wa Idara ya Madeni Justine Japhet, Kaimu Kamishna wa Sera Bw. Wiiliam Mhoja na Maafisa Wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akieleza kuhusu fursa za Uwekezaji nchini kutokana na Tanzania kuwa lango la Bahari kwa nchi nyingi, wakati alipokutana na kufaya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu, uliofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb)
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao ulioangazia ushirikiano katika upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili miradi mikubwa ya Maendeleo nchini, uliofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu, akieleza nia ya Benki yake ya kusaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo wa Reli ya Kisasa (SGR) wakati wa mkutano wake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), hayupo pichani, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akiwa katika Mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu, katika mkutano kati yao ulioangazia upatokanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya Maendeleo nchini, uliofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Bw. Lawrence Mafuru, akifafanua jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu (hawapo pichani), jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine (katikati), akifafanua jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu (hawapo pichani), jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Lawrence Mafuru na kulia ni Mwanasheria kutoka Idara ya Sheria-Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Pauline Fungameza
Naibu Katibu Mkuu (Sera) wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CITI anayesimamia nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu (katikati) na Afisa Mtendaji Mkuu wa CITI Bank Tanzania, Bw. Geofrey Mchangila, wakifurahia jambo baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Mkurugenzi Mtendaji huyo wa CITI Bank (Afrika) na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani).
No comments:
Post a Comment