Mkurugenzi Idara ya Tiba Dkt.Omary Ubuguyu akifanya mahojiano na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya Bi.Catherine Sungura kuhusiana na afya ya akili
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya afya akili Mirembe Dkt.Innocent Mwombeki akielezea daliliza ugonjwa wa afya ya akili
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya afya akili Mirembe Dkt.Innocent Mwombeki akielezea daliliza ugonjwa wa afya ya akili
Na. WAMJW - DODOMA
Ongezeko la watu wenye matatizo ya Afya ya akili husababisha matukio ya kikatili kuongezeka ikiwemo watu kutaka kujiua.
Haya yamebainishwa leo na Mkurugenzi Idara ya Tiba Dkt. Omary Ubuguyu alipofanya mahojiano maalum na kaimu Mkuu kitengo cha Mawasiliano Serikalini Catherine Sungura,Wizara ya Afya jijini Dodoma.
Dkt. Ubuguyu amesema kuna baadhi ya magonjwa ya akili yanaweza yakaambatana na tabia ya ukali na kuwa na hisia mbaya kwa mwenza wako kuona anakusaliti hivyo familia zinatakiwa kuwa na mawasiliano mazuri ya ndani na nje ili kuwepo ubora ndani ya ndoa.
Dkt.Ubuguyu amesema kuwa familia ni taasisi hivyo uimara unajengwa kwa ushirikiana kati ya wenza na familia ya nje hivyo ubora wa familia unajengwa kwa mawasiliano ya dhati ya ndani na nje na matatizo ya wenza ni lazima yajadiliwe ili kuepusha afya ya akili kwa familia na kudhibiti matatizo ya aina hiyo.
“Mtu asiyekua na afya njema ya akili anaweza akawa mgonjwa wa akili au anaweza kushindwa tu kudhibiti hisia zake na hawezi kupima fikra zake kwa kujua jambo linaweza kuwa na madhara kiasi gani.” amesema Dkt Ubuguyu
Hata hivyo Dkt.Ubuguyu amewataka wazazi na walezi kuacha kukasikirika/kuchukia mara kwa mara mbele ya watoto kwani sehemu ya malezi hupelekea kuumiza hisia za watoto na hivyo husababisha watoto kujifunza tabia hizo kwa kuona ndio njia za kukabiliana au kawaida.
"Jamii bado inashindwa kuripoti watu wenye matatizo kwa kuhofu au kumuogopa mtu mwenye dalili ili kudhibiti watu wenye matatizo afya ya akili kwenye jamii lakini atakapofanya tukio la kikatili basi jamii inayomzunguka itasema walihisi na kuona dalili"Aliongeza.
Aidha, Dkt Ubuguyu amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa kipaumbele kwa kuweka waratibu wa Kitaifa na kwa kila Mkoa / Halmashauri na maeneo yote ya kutolea huduma za Afya kuanzia hospitali ya Taifa huduma za afya ya akili zinatolewa hivyo wananchi wasisite kufika kwenye vituo vya afya kupatiwa huduma hiyo ili kuepuka matukio ya kikatili kwenye jamii.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya akili Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Innocent Mwombeki amebainisha dalili za ugonjwa wa afya ya akili ni pamoja na Kubadilika kwa tabia, kupatwa na hasira za karibu Sana na kusikia sauti za watu kukuongelesha bila kuwaona.
“Dalili zote hizi hupelekea mtu kupatwa na ugonjwa wa afya ya akili lakini pia ugonjwa huo unatibika kwa kupata Dawa pamoja na kusikiliza wataalamu wa saikolojia.” amesema Dkt Mwombeki
Hata hivyo Dkr Mwombeki akiendelea kufafanua juu ya matibabu ya Dawa amesema Ukitumia Dawa unaweza kupona ndani ya muda mfupi na kurudi katika hali ya kawaida japo wengine huchukua muda kutokana na aina ya ugonjwa.
“Tumeanzisha kitengo kipya cha utafiti na mafunzo kwenda kwa jamii na tayari tafiti zilishafanyika kwa watu zaidi ya watu 180 kwenye Mikoa tafauti na 32% tuliwakuta na dalili za magonjwa ya akili na 10% walikua na matumizi mabaya ya pombe na 19% walishawahi kupata wazo la kutaka kujiua.” amesema Dkt Mwombeki
Hata hivyo amesema wagonjwa wote wanatakiwa kutibiwa ndani ya maeneo yao kama ni Mkoani, wilayani na mgonjwa akilazimika kutoka ndani ya Mkoa husika basi anatakiwa kuwa na mtu wa karibu kwaajili ya uangalizi.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa katika kila sekunde arobaini mtu mmoja anafanya tukio la kukatisha uhai wake na inspelekea watu laki nane duniani kujiua kila mwaka.
No comments:
Post a Comment