Mkuu wa Mauzo wa Airtel Tanzania kwa Mkoa wa Katavi Bartholomew Masatu (kushoto) akimkabidhi Mama Mkuu wa Kituo cha Mtakatifu Yohane Paul cha mkoani Katavi Rose Sungura (katikati) baadhi ya msaada uliotolewa na kampuni ya Airtel Tanzania ikiwa ni ishara ya kuonesha upendo kwa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu. Kulia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Katavi Anna Shumbi.
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kupitia kampeini maalum ya kusaidia jamii kwa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ambayo inalenga kuwanufaisha watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, leo imetoa msaada wa vyakula kwa kituo cha watoto yatima cha Mtakatifu Yohana Paul cha mkoani Katavi. Kampeini hiyo ya wafanye watabasamu, ilizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na inalenga kunufaisha vituo 12 vya watoto yatima hapa nchini.
Akiongea mara baada ya kutoa msaada huo kwa kituo hicho cha Mtakatifu Yohana Paul, Mkuu wa Mauzo Airtel Mkoa wa Katavi Bartholomew Masatu alisema muda mrefu imekuwa na utamanduni wa kusaidia jamii na kwa kipindi cha msimu wa sikukuu, kampuni iliona ni vyema ikatumia kwa kusherehekea na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Leo ni siku yenye furaha sana kwetu zote kwani mayatima ni sehemu ya Jamii yetu na ni muhimu kuwapa upendo pamoja na kuwafariji. Hiki ambacho tumekuja kutoa leo hapa ni kidogo lakini nina uhakika kitagusa mioyo yenu lakini zaidi ni kujua tuko pamoja nanyi na tunawajali sana, alisema Masatu.
Tunayo furaha kuweza kuwafikia watoto hawa ambao wako kwenye kituo hiki na dhamira yetu ni kuendelea kugusa maisha ya watoto wanaoishi kwenye mazingira mangumu na kuwafanya wajisikia kuwa sehemu ya familia ya Airtel, aliongeza Masatu.
Kwa upande wake, Mama Mkuu wa kituo cha Mtakatifu Yohana Paul Sista Rose Sungura alisema ni furaha kwa kampuni kubwa ya Airtel kuguzwa na maisha ya watoto wanaoishi kwenye kituo hiki na hatimaye kuja kutoa msaada na kutuunga mkono.
Najua kuna vituo vingi vya mayatima hapa nchini kama sisi hapa. Kuamua kuja kuwa na sisi ni Baraka kubwa kwetu. Nachukua fursa hii kuwapongeza wote kwa kile mlichotoa ambacho mnaweza kudhani ni kidogo lakini kinaleta matumaini makubwa kwetu na hasa kwa hawa watoto. Naomba kuwakaribisha tena hapa na sio lazima kuja kutoa msaada, lakini mnapokuja kujumuika na hawa watoto wanapata faraja kubwa na kujisikia kama sehemu ya Jamii kwani wengi wao hapa hawajawahi kuona Wazazi wao, alisema Sungura.
No comments:
Post a Comment