RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, miongoni mwa matukio yaliyoacha alama katika historia ya nchi yetu katika mwaka 2021ni misiba ya viongozi wetu wakuu wawili, ambao ni Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefariki dunia Machi 17, 2021 na Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliyefariki dunia Februari 17, 2021.
"Watanzania tulipata huzuni kubwa kwa kuondokewa na viongozi wetu hawa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu, awalaze mahali pema viongozi wetu hao na wananchi wengine waliotangulia mbele ya haki;
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 31, 2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati akitoa salamu za kuukaribisha mwaka mpya wa 2022 kwa wananchi.
"Tukio jingine la kihistoria lililotokea nchini katika mwaka 2021 ni kuanza kwa uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita, ikiongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa ni Rais mpya wa nchi yetu.
"Kwa mara ya kwanza, nchi yetu inapata fursa ya kuongozwa na Rais mwanamke. Hili ni tukio la historia siyo tu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali kwa Bara zima la Afrika, tukizingatia kwamba, hadi sasa ni nchi chache tu Barani Afrika ambazo zimewahi kuongozwa na Rais mwanamke. Tuendelee kumpa ushirikiano anaouhitaji Rais wetu Mpendwa na tunamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie hekima, busara na upendo ili aweze kuyatekeleza majukumu yake vyema,"amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi amemshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuturuzuku neema ya uhai na kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo ya tarehe 31 Disemba, 2021 ambapo tunauhitimisha mwaka wa 2021 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2022.
"Hakika hii ni neema kubwa kwetu na tunapaswa tushukuru tukijuwa kwamba, katika kipindi kama hiki cha kuukaribisha mwaka unaomalizika, tulikuwa na wenzetu, ambao leo hii hatunao tena wameshatangulia mbele ya haki.
"Ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanaadamu katika kipindi cha mwaka mmoja kukabiliana na matukio mengi ya furaha, misiba na mengine ya kawaida katika maisha ya kila siku. Na vile vile, ndani ya kipindi hicho Serikali hupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na kuongeza kasi ya maendeleo.
Kwa hivyo, ni vyema kila mwisho wa mwaka tukaendeleza utamaduni wa kutathmini mafanikio na changamoto kwa yale mambo tuliyojipangia kuyafanya,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Pia Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi amesema moja kati ya mambo makubwa ya kumshukuru Mola wetu ni kutubariki katika mwaka 2021 tunaoumaliza kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu pamoja na umoja na mshikamano wa wananchi.
Amesema, katika kipindi chote cha mwaka tunaoumaliza, hali ya amani imeweza kudumu nchini na kuiwezesha Serikali kutekeleza vyema majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kukuza uchumi, kuimarisha miundombinu mbali mbali na kuendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
"Mafaniko mengi tuliyoyapata katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii niliyaeleza katika hotuba yangu niliyoitoa Novemba 6, 2021 katika hafla ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani. Kadhalika, nitayaelezea mafanikio mengine tuliyoyapata na changamto zilizojitokeza kwa mwaka 2021 tunaoumaliza katika hotuba nitakayoitoa katika Sherehe za Mapinduzi siku ikifika, Inshaallah.
"Ndugu wananchi,moja ya changamoto tulioendelea kukabiliana nayo katika mwaka 2021 hapa Zanzibar, Tanzania na duniani kote kwa jumla ni janga la maradhi ya UVIKO 19 ambalo limechangia sana kuzorotesha uchumi wetu kama ilivyo katika mataifa mbali mbali duniani.
"Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO- 19 kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa, nchi marafiki, sekta binafsi na Watumishi wa sekta ya afya.
"Serikali tayari imeshaanzisha vituo 41 vyenye kutoa huduma za chanjo ya UVIKO 19, kati ya hivyo 29 viko Unguja na 12 viko Pemba. Tuendelee kufanya kazi kwa bidii katika mwaka 2022 huku tukichukua tahadhari ya maradhi ya UVIKO - 19 hasa kwa kujikinga na aina mpya ya virusi vinavyojulikana kwa jina la Omicron ambavyo viliripotiwa kuwepo nchini Afrika ya Kusini tangu tarehe 24 Novemba 2021, na hivi sasa vimeenea katika nchi mbalimbali,"amebainisha Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Pia amesema, katika juhudi za kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO 19, Serikali imepata mkopo wa dola za Kimarekani milioni 100 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 230 ambazo zitatumika katika ujenzi wa miundo mbinu ya Afya, Elimu, Maji na Nishati ya Umeme.
Aidha, amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 81 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali wadogo wadogo na wakati.
"Nawasihi wananchi wote tushirikiane katika kutekeleza miradi tuliyoipitisha na mikopo itakayotolewa kwa wajasiriamali,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi.
Amesisitiza kuwa, wakati tunajitayarisha na mwaka mpya, "nachukua fursa hii kuwahimiza wananchi kwamba, tuendelee kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, vitendo vya udhalilishaji pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.
"Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo bila ya muhali au kumuonea mtu yoyote. Nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya haki na utawala bora. Kwa hivyo lazima sheria iwe inachukua mkondo wake na kuhakikisha tunalinda haki za kila raia kwa mujibu wa Katiba.
"Kwa mara nyingine, napenda niwashukuruni kwa kudumisha amani na utulivu na niwaombeni muendelee kuzidumisha tunu hizo katika mwaka tunaouanza, kwani ni msingi muhimu wa juhudi zetu za kuleta maendeleo na kuwavutia wawekezaji.
"Katika, mwaka unaomalizika, viongozi, wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Kimataifa pamoja na mabalozi na watu mashuhuri walitutembelea na kuonesha kuridhishwa kwao na hali ya amani, mapenzi, ukarimu, pamoja na mshikamano tulio nao. Ni vyema tuazimie kuendeleza utamaduni huu kwa faida ya nchi yetu na watu wake,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa wasaidizi wake wakuu akiwemo Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais, waheshimiwa mawaziri wote, makatibu wakuu na wakurugenzi, maofisa wadhamini na watendaji wote wa Serikali kwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
"Kadhalika, nawashukuru Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa madhehebu ya Dini na Taasisi za kiraia za ndani na nje ya nchi pamoja na washirika wetu wote wa maendeleo kwa ushirikiano waliotupa kwa mwaka unaomalizika.
"Namalizia kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa, mwaka ujao ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makaazi. Sensa hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Serikali katika kupanga na kutekeleza kwa ufanisi mipango yetu ya maendeleo. Wito wangu ni kuwa, wakati ukifika sote tushiriki. Tutoe ushirikiano kwa maofisa wahusika ili zoezi hilo muhimu lifanyike kwa mafanikio.
"Kadhalika, nawakumbusha kuwa kuanzia tarehe 1 Januari hadi tarehe 12 Januari 2022 tutakuwa na shamra shamra za maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Nawahimizeni wananchi wenzangu kujitokeza kwa wingi katika matukio mbalimbali yaliyopangwa kwa ajili ya sherehe hizo. Huo ni wajibu wetu wa kuonesha uzalendo wetu kwa kubainisha kuwa tunayathamini Mapinduzi ya mwaka 1964 kuwa ndiyo yaliyoleta ukombozi na mwanzo wa maendeleo ya nchi yetu.
"Nawatakia wananchi wote ushiriki mwema na nawaomba wananchi wote tusherehekee mwaka mpya kwa amani kwa kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama.
"Natoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar, Tanzania kwa jumla, viongozi wa nchi rafiki, taasisi na washiriki wetu wa maendeleo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aujaalie mwaka mpya wa 2022 uwe wa mafanikio zaidi katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo na kudumisha amani na ustawi wa nchi yetu,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
No comments:
Post a Comment