Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Aymen Benabderrahmane mara baada ya kukabidhi ujumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali ya Algeria.
*Asisitiza juu ya ushirikiano katika sekta ya nishati
NA MWANDISHI MAALUM
Ziara ya Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba nchini Algeria imefungua kurasa zilizokuwa zimefungwa kwa muda mrefu za ushirikiano baina ya Tanzania na Algeria ikiwa ni nchi marafiki tangu enzi za ukombozi wa Afrika.
Waziri Makamba ametembelea Algeria kwa lengo la kukuza uhusiano wa kisekta na pia kuwasilisha ujumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Aymen Benabderrahmane mara baada ya kukabidhi ujumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali ya Algeria. Katika kikao hicho Waziri makamba aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Balozi Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu, Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Ndg. Michael Mjinja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio.
Ujumbe huo maalumu kutoka Serikali ya Tanzania kwa Serikali ya Algeria ulipokelewa na Waziri Mkuu wa Algeria, Mhe. Aymen Benabderrahmane kwa niaba ya Rais wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune.
Akiongea baada ya kupokea ujumbe huo, Mhe. Benabderrahmane alisema Tanzania na Algeria ni marafiki wa kihistoria na ni wakati muafaka kwa nchi hizi mbili kuboresha zaidi mahusiano na namna moja wapo wa kufanya hivyo ni kushirikiana kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili”.
Aidha Waziri Mkuu huyo alieleza kuwa kuna maeneo mengi ya kiuchumi ambayo Tanzania na Algeria wanaweza kushirikiana na eneo mojawapo ni sekta ya nishati ambayo Algeria ina uzoefu wa zaidi ya miaka 50 huku ikiwa na ugunduzi mkubwa wa mafuta na gesi asilia.
Aidha Waziri Makamba alieleza nia ya Serikai ya Tanzania kuanzisha uhusiano na Algeria katika eneo la nishati ambapo tayari nchi hizi mbili zilishaanzisha majadiliano na hata kuandaa rasimu ya hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding-MoU) katika maeneo ya gesi asilia na umeme.
Tayari kuna kazi kubwa ilikwishafanyika huko nyuma na ziara hii imelenga kuhakikisha kazi hiyo kubwa inakamilika ili kuona urafiki wetu unaimarika zaidi kwa kushirikiana katika kukuza uchumi alisema Waziri Makamba.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Aymen Benabderrahmane mara baada ya kukabidhi ujumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Serikali ya Algeria.
Mara baada ya kuwasilisha ujumbe huo, Waziri Makamba alipata nafasi ya kutembelea kampuni za Sonelgaz na Sonatrach ambazo ni kampuni za Serikali zinazojihusisha na mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya nishati (mafuta, gesi na umeme).
Kwa upande wa Sonelgaz, Waziri Makamba alitembelea kituo cha kuzalisha umeme ambapo aliweza kujionea matumizi makubwa ya teknolojia katika kuendesha na kusimamia gridi ya taifa ya umeme.
“Nimeweza kuona namna wenzetu wanatumia teknolojia katika kusimamia gridi na hii ni moja ya eneo ambalo tunaweza kushirikiana kwa kubadilishana ujuzi na uzoefu," alisema Waziri Makamba.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgaz, Ndg. Chahar Boulakhras wakati alipofanya ziara ya kutembelea kituo cha kuzalisha umeme Jijini Algiers kinachoedeshwa na Sonelgaz. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mwambata wa Jeshi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria, Brigedia Jenerali Adolf Peter Mutta, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio na Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Ndg. Michael Mjinja.
Pamoja na kuwa Algeria ni nchi kubwa kuliko zote Afrika kwa eneo lakini wameweza kusambaza umeme kwa zaidi ya asilimia 90 ya watu wake na pia kujenga mtandao wa kusambaza gesi asilia wa kilometa 22,000.
Akitoa maelezo wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgaz, Ndg. Chahar Boulakhras alimueleza Waziri Makamba kuwa Sonelgaz iko tayari kuwekeza Tanzania na itasubiri mualiko rasmi ili kutuma timu ya wataalam kuendeleza mazungumzo ambayo yalikwishaanza hapo awali.
Kwa upande wa Sonatrach, Waziri Makamba alitembelea moja ya kiwanda cha kusafisha mafuta kilichopo Algiers ambapo alijionea namna shughuli za usafishaji mafuta ghafi zinavyofanyika na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kiwandani hapo ikiwemo dizeli, petroli, JET A1 na gesi ya mitungi (LPG).
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Waziri Makamba alisema Tumejionea namna hawa wenzetu walivyopiga hatua katika eneo hili na ninaamini Tanzania tunaweza kujifunza na kujenga mahusiano zaidi ya kibiashara na Algeria kwa maslahi mapana ya nchi zetu.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Sonelgaz, Ndg. Chahar Boulakhras (wa nne kutoka kulia) pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu (wa tatu kutoka kulia), Kamishna wa Petroli na Gesi, Ndg. Michael Mjinja (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio ( wa pili kushoto). Wengine pichani ni maafisa waandamizi kutoka Sonelgaz.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara yake nchini Algeria, Waziri Makamba alisema Tunatarajia kuwaalika wataalamu kutoka Algeria kuja nchini Tanzania kwa lengo la kukamilisha rasimu za hati ya makubaliano ambazo zilishafanyiwa kazi huko nyuma ili kuweza kuanza ushirikiano wetu mara moja bila kuchelewa.
Katika ziara hiyo, Waziri Makamba aliambatana na Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Ndg. Michael Mjinja na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio wakisindikizwa na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu, Mwambata wa Jeshi, Brigedia Jenerali Adolf Peter Mutta, Mwambata wa Siasa na Utamaduni Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria, Ndg. Suleiman Rashid na maafisa wengine kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria.
No comments:
Post a Comment