Pages

Wednesday, September 29, 2021

MBEYA KUTENGA BAJETI YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi cheti mmiliki wa vituo vya “Dkt. Tulia Day Care” Wiseman Luvanda ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa shule hiyo kwenye utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya leo (29.09.2021).

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi cheti mwakilishi wa kampuni ya ASAS mkoani humo Ahmed Kasu ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa kampuni hiyo kwenye utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya leo (29.09.2021).

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi zawadi ya begi mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mashindano ya kutunga jumbe nzuri zinazohusu unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya leo (29.09.2021).

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera (kushoto) akimkabidhi cheti mwakilishi wa kampuni ya TANGA FRESH mkoani humo Kephas Gembe ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa kampuni hiyo kwenye utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni wakati wa Maadhimisho ya Siku ya unywaji maziwa shuleni yaliyofanyika mkoani Mbeya leo (29.09.2021).
Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera akimkabidhi maziwa mmoja wa wanafunzi waliofika kwenye maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa shuleni yaliyofanyika leo (29.09.2021) mkoani humo, wengine pichani kutoka kushoto ni mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Stephen Michael, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya na Meneja Utawala na Fedha kutoka Kiwanda cha maziwa cha Sebadom Anati Kombeson.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote zilizopo mkoani kwake kutenga bajeti ya maziwa kwa wanafunzi wote wa shule za awali na msingi waliopo mkoani humo.

Homera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Siku ya unywaji maziwa shuleni ulimwenguni ambayo kitaifa imefanyika leo (29.09.2021) mkoani Mbeya amesema kuwa suala la unywaji maziwa shuleni kwa wanafunzi ni la lazima na si hiyari. “Hatuwezi kusubiri wadau tu kila siku wajitoa wakati watoto ni wetu wenyewe hivyo ni lazima wakati wa kupanga bajeti zote za halmashauri zilizopo mkoani Mbeya iwekwe bajeti ya kutekeleza mpango huu na kwa sababu mimi ndo naidhinisha bajeti zote,sitopitisha bajeti yoyote ambayo haina bajeti ya kutekeleza mpango huo” Amesema Homera. Aidha Homera amepongeza juhudi na kazi inayofanywa na Wizara ya mifugo na Uvuvi kupitia bodi ya maziwa kwa kuwa karibu na wadau mbalimbali wa tasnia ya maziwa waliopo mkoani humo ambapo amewataka wasindikaji wote wa maziwa nchini kuendelea kuwekeza katika mkoa huo. “Mimi ninapenda sana wawekezaji na kipekee kabisa niwashukuru ASAS kwa kuamua kuja kujenga kiwanda kikubwa cha maziwa hapa, niwaombe Tanga Fresh na makampuni mengine ya maziwa kufanya hivyo pia ili kuchochea zaidi uwekezaji katika tasnia ya maziwa katika mkoa wa Mbeya” Amesisitiza Homera. Akizungumzia hali ya uwekezaji kwenye tasnia ya maziwa nchini, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Stephen Michael amesema kuwa hadi sasa Tanzania ina jumla ya ng’ombe wa maziwa Mil. 1.2 ambao huzalisha jumla ya lita za maziwa Bil.3.1. “Aidha hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu, Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda vya kusindika maziwa vikubwa, vidogo na vya kati 104 na kati ya hivyo 96 ndo vinafanya kazi” Amesema Michael. Akibainisha kuhusu uwezo wa uzalishaji wa viwanda hivyo, Michael amesema kuwa viwanda vilivyopo vina uwezo uliosimikwa wa kusindika lita 865600 kwa siku lakini kutokana na uhaba wa upatikanaji wa malighafi viwanda hivyo vinasindika wastani wa asilimia 24 ya uwezo wake ambao ni sawa na lita 206849 kwa siku. Akielezea kuhusu utekelezaji wa mpango wa unywaji maziwa shuleni, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya amesema kuwa mpango huo ulianzia mkoani Kilimanjaro mwaka 2007 kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwa kujenga utamaduni huo kuanzia ngazi ya shule ya awali. “ Tunafanya hivi kwa sababu mbali na maziwa kuwa lishe nzuri na kiburudisho kwa watoto, imethibitika kuwa maziwa ni mlo kamili unaoweza kujitosheleza bila kutegemea chakula kingine na ndo chakula pekee chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini” Amesema Dkt. Msalya. Aidha Dkt. Msalya amebainisha kuwa tangu kuanza kwa mpango huo takribani watoto elfu 90 kutoka shule 210 hapa nchini wamepatiwa maziwa ambapo amesema kuwa idadi hiyo imeendelea kupungua kadri miaka inavyoendelea. “ Tunaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuwajengea uwezo wanafunzi, wazazi na walezi wao juu ya umuhimu wa maziwa ili kuhakikisha kiwango cha matumizi ya bidhaa hiyo kinaongezeka” amehitimisha Dkt. Msalya. Maadhimisho ya Siku ya unywaji Maziwa mwaka huu yalitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na ugawaji maziwa katika vituo vya afya, mahabusu ya watoto na kwenye vituo vya watoto yatima.

No comments:

Post a Comment