BOHARI Kuu ya Dawa(MSD) imesema kwa sasa hakuna kiwanda cha kutengeneza mipira ya kiume maarufu Kondomu ambacho kinamilikiwa na bohari hiyo.
Majibu hayo yametolewa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD Meja Jenerali Gabriel Mhidze wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye semina iliyoandaliwa na MSD kwa lengo la kuelezea shughuli wanazozifanya katika kuboresha sekta ya afya na hasa katika eneo la upatikanaji dawa na vifaa tiba.
Katika semina hiyo mwandishi wa habari ambaye amejikita zaidi kuandika habari za afya Veronica Mrema aliuliza swali kwa MSD akitaka kujua kuna mikakati gani inafanyika ili kuwa na kiwanda cha kutengeneza mipira kiume kutokana na uhaba wa mipira hiyo.
Hivyo wakati anajibu swali hilo Meja Jenerali Mhidze amesema kwa sasa MSD ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono(gloves),hivyo hakuna kiwanda cha kutengeneza mipira ya kiume.
Amefafanua kiwanda cha mipira ya mikono na kiwanda cha mipira ya kiume haikai pamoja.
"Viwanda hivi havikai pamoija, mwanzoni tulikuwa na wazo la kujenga sehemu moja, lakini kumbe havitakiwi kukaa pamoja.Hivyo kiwanda cha mipira ya kiume kitajengwa baadae baada ya teknolojia kukua," amesema Meja Jenerali Mhidze.
Ametaja viwanda vya MSD vilivyopo sasa ni kiwanda cha kutengeneza vidonge, kiwanda cha kutengeneza vidonge vya rangi mbili,kiwanda cha kutengeneza barakoa,kiwanda cha kutengeneza dawa za majimaji pamoja na mkakati wa kutengeneza kiwanda cha kutengeneza cream ambayo ni maalum kwa magonjwa ya ngozi hasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino)
No comments:
Post a Comment