Pages

Monday, August 30, 2021

TEN/MET YAIPONGEZA SERIKALI KUMSAIDIA MTOTO WA KIKE KIELIMU

 

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania Kitaifa, Bw. Ochola Wayoga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na wadau wa elimu kubaini ufanisi, changamoto na uwezo wa vituo vya elimu kwa njia mbadala (alternative education pathways) vinavyoweza kumuandaa na kumsaidia mtoto wa kike aliyelazimika kuacha shule kwa sababu ya ujauzito.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania Kitaifa, Bw. Ochola Wayoga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na wadau wa elimu kubaini ufanisi, changamoto na uwezo wa vituo vya elimu kwa njia mbadala vinavyoweza kumuandaa na kumsaidia mtoto wa kike aliyelazimika kuacha shule kwa sababu ya ujauzito.

MTANDAO wa Elimu Tanzania, TEN/MET umeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa hatua ya kutenga fedha za kimarekani million 500 kuhakikisha mtoto aliyeachishwa shule kwa ajili ya ujauzito atakapo faulu kupitia elimu ya njia mbadala anaweza kurudi kwenye mfumo rasmi na kupangiwa shule za serikali.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Bw. Ochola Wayoga alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti kubaini ufanisi, changamoto na uwezo wa vituo vya elimu kwa njia mbadala (alternative education pathways) vinavyoweza kumuandaa na kumsaidia mtoto wa kike aliyelazimika kuacha shule kwa sababu ya ujauzito ili kuweza kutimiza ndoto zake kimaisha.

Mbali na pongezi hizo, Bw. Wayoga amesema wadau wa elimu nchini waliokutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam pia wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa mabadiliko ya sera, sheria na miongozo ya elimu nchini kumpa nafasi ya kurudi shuleni kwa mfumo wa kawaida msichana aliyekatishwa masomo kwasababu ya ujauzito ili apate elimu stahiki.

"Hii ni kwasababu, Tanzania imesaini maridhiano kadhaa ya kimataifa ili kuhakikisha kuna upatikanaji wa elimu bora na yenye kuzingatia usawa wa kijinsia. Lakini pia hatutakiwi kuwa na sheria ambazo ni kandamizi, zinazokinzana na zisizojali haki za watu kwa ujumla.

Kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wadau wa elimu, imebainika kuwa sababu ya wanafunzi kupata ujauzito ni umaskini uliokithiri hivyo kupelekea wao kudanganyika kwa vizawadi vidogovidogo, umbali kutoka shule ambapo njiani hukumbana na vishwawishi vingi, ubakaji, ndoa za kulazimishwa na ukosefu ya afya ya uzazi na jinsia." Alifafanua Bw. Wayoga.

"Sisi kama wadau tunapongeza sana serikali kwa jitahada hizi lakini utafiti wetu umetujulisha kuwa umbali mrefu na gharama ya kujiunga kwenye mfumo wa elimu mbadala umekuwa ni kikwazo cha watoto wa kike kujiunga. Pia taarifa hii ya kifursa haijaweza kuufikia uma kwa mapana ili kutambua fursa hii mbadala ingawa ina changamoto zake," alisema Mratibu huyo.

Aidha aliongeza kuwa, vituo vingi vinavyotoa elimu kwa njia mbadala vinapatikana maeneo ya mjini na sio vijijini huku vikiwa na gharama mbalimbali ambazo pia ni changamoto kwa watoto wengi waishio vijijini na kwenye mazingira magumu kujiunga navyo, hivyo kukosa fursa hiyo moja kwa moja.

Hata hivyo, wadau hao wa elimu waliiomba Serikali sikivu ya awamu ya sita kuangalia suala hilo tena kwa jicho pana na yakinifu kwani matokeo ya kundi hilo linaloathiriwa kwa kukosa elimu ni kuendeleza umasikini uliokithiri na kuongeza wimbi la wanawake wasio na elimu nchi na hivyo kuwa kikwazo cha kuweza kufikia malengo ya kidunia ya kufikia usawa wa kijinsia mnamo mwaka 2030

No comments:

Post a Comment