AFISA Mipango, Anold Kamala amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salam akikabiliwa na mashtaka manne ya kugushi.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Yusuph Aboud amedai mshtakiwa ametenda makosa hayo, Machi 8,2021 huko katika ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zilizopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rita Tarimo imedaiwa, siku hiyo mshtakiwa Kamala kwa nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka za uongo tatu ambazo ni invoice zenye namba tofauti tofauti kwenda kwa Muhidin Jeram ya Sh. 7,805,730, Anna Mwamlenga ya Sh, 1,617,300 na Fadhili Muhidin ya Sh, 4,254,023 kwa madhumini ya kuonesha kuwa nyaraka hizo zimetolewa na wizara ya Ardhi huku akijua kuwa siyo kweli.
Katika shtaka la nne imedaiwa Februari Mosi, 2018 huko huko Wizara ya , Nyumba na Makazi, mshtakiwa kwa nia ya kudanganya alighushi invoice namba 937618 ya tarehe 1/2/2018 iliyotolewa kwa Anna Mwamlenga na kuisaini kwa jina la Johansen Chibanda kwa madhumuni ya kuonesha kuwa invoive hiyo imetolewa na Wizara ya Ardhi na ni halali kwa malipo Sh. 1,617,300 huku akijua kuwa siyo kweli.
Hata hivyo mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kufanikiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili kutoka Taasisi inayotambulika kisheria ambapo kati yao mmoja wao ametakiwa kuweka fedha kiasi cha sh. Milioni saba.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24,2021 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment