Pages

Wednesday, July 28, 2021

TASAF YATOA MILIONI 193 KUBORESHA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO KIJIJI CHA MKAMBARANI MKOANI MOROGORO

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani ambacho TASAF imetoa shilingi milioni 193 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ili kuboresha huduma ya afya ya uzazi kijijini hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani.

Diwani wa kata ya Mkambarani Mhe. Mboma Peter akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kuwezesha upatikanaji wa shilingi milioni 193 zilizotolewa na TASAF kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika kata yake.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) ambaye amewezesha kijiji chao kupata shilingi milioni 193 kutoka TASAF ili kujenga wodi ya mama na mtoto kijijini hapo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwaeleza wananchi wa Kijiji cha Mkambarani jitihada za Mbunge wao Mhe. Hamisi Taletale katika kufanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 193 zilizotolewa na TASAF kwa ajili ya kujenga wodi ya Mama na Mtoto kijijini hapo. Aliyesimama nae ni Mbunge huyo Mhe. Hamisi Taletale.

********************************

Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 28 Julai, 2021

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imetoa kiasi cha shilingi milioni 193 kwa ajili ya kujenga wodi ya mama na mtoto katika Kijiji cha Mkambarani Mkoani Morogoro ili

kuboresha huduma ya afya ya uzazi.

Kiasi hicho cha fedha kimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa tarehe 14 Machi, 2021 ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Morogoro.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani, Mhe. Ndejembi amesema, wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya Bunge, wananchi walieleza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi inayowakabili akina mama pindi wanapohitaji huduma hiyo, hivyo Kamati iliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutatua changamoto hiyo ili kuwaondolea adha akina mama wa Mkambarani kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewaasa watendaji wa Serikali wenye jukumu la kusimamia zahanati ya Mkambarani kuhakikisha fedha iliyotolewa inatumika kujenga wodi ya mama na mtoto kama ilivyokusudiwa, na kutoa wito kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo.

“Naelekeza kutumia utaratibu wa kufanya manunuzi pasipo kumtumia mkandarasi ili kupunguza gharama za ujenzi na kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha.” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha hizo kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ili wananchi wa Mkambarani wapate huduma bora, hivyo hatosita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuzitumia vibaya fedha hizo za umma.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) licha ya kutoa ruzuku kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, umekuwa na mchango mkubwa wa kuboresha sekta ya afya kwa kutoa fedha za kujenga zahanati mbalimbali nchini ikiwepo ya Kijiji cha Mkambarani Mkoani Morogoro ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya zinazowakabili wananchi hususani wenye kipato cha chini.

 

No comments:

Post a Comment