Pages

Wednesday, June 30, 2021

CCM YAWAOMBA WADAU UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI KUUNGANA KATIKA KUWEKA MIKAKATI KUKABILI CHANGAMOTO YA AJIRA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Chama cha Mapinduzi CCM ,Shaka Hamdu Shaka akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM katika kikao cha wadau 28 kutoka katika Taasisi za Uwezeshaji Nchini  kilichofanyika ukumbi wa Takwimu Mjini Dodoma.
Shaka Hamdu Shaka ambaye ni Katbu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) akizungumza wakati wa mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kinahitaji kuona mipango ya Serikali

yenye kuleta majawabu kwa vitendo badala ya kutumia muda mwingi kuwa na mipango inayoanisha malengo mazuri kwa kila mwaka lakini utekelezaji wake ni mdogo.

Aidha kimesema Rais Samia Suluhu Hassan ameshaonesha njia na utayari wa kuwa mkombozi wa changamoto za kiuchumi pamoja na ajira kwa Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu hivyo ni lazima aungwe mkono sio kwa maneno bali kwa mipango na mikakati inayotekelezeka kivitendo.

Akizungumza na wadau 28 kutoka katika taasisi za Uwezeshaji nchini  Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ndugu Shaka Hamdu Shaka kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo , katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Takwimu Dodoma amesema wakati umefika kuweko na mpango shirikishi kwa wadau hao na uwekewe uratibu mzuri wa kufanyiwa tathimini kila baada ya muda.

 "Kizazi cha miaka ya 1960 kilikuwa na wajibu wa kuleta uhuru kwa nchi yetu, kizazi baada yao  na sisi tukiwemo tunao wajibu wa kuleta uhuru wa kiuchumi na kuhakikisha nchi yetu inajenga uchumi wa kisasa ambao sio tegemezi kupitia Mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda kwa kutumia teknolojia, kazi kwetu kuamua kutekeleza wajibu huo au kuusaliti,"amesema Shaka.

Amefahamisha sifa kubwa ya CCM ni kuwa na fikra na vitendo vya kimapinduzi. Fikra hizo ni yale mawazo yanayolenga kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa na ya haraka katika nchi, ili kufanikisha tunahitaji Sera, mipango na mikakati inayozingatia maarifa, ujuzi na teknolojia yenye kuweza kufanya Mapinduzi kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, usindikaji na viwanda.

"Hili linawezekana ikiwa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi zitakuwa na bajeti, mipango shirikishi, utaratibu usiyo na urasimu pamoja na masharti magumu, inafahimika au kupatikana kirahisi, ina mchakato wa wazi  wa utoaji mikopo au vitendea kazi, ina mfumo mzuri wa kuwasimamia vijana wakati wote wa utekelezaji wa miradi ili kupata matokeo yaliyotarajiwa,"ameongeza Shaka

Hata hivyo Shaka amebainisha kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM imeahidi upatikani wa ajira 8 millioni katika kipindi cha miaka 5 hivyo CCM inahitaji majawabu halisia  kwa kila taasisi ya umma namna alivyotekeleza  sambamba na kuanisha mikakati iliyojiwekea ambapo Chama kitapita kukagua na kujiridhisha.

Kikao hicho kikehudhuriwa na viongozi wa taasisi mbali mbali na mashirika ya umma na binafsi ni sehemu ya  CCM kufatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020 -2025.

 

No comments:

Post a Comment