Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli akizungumza na washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa walimu, yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba na kulia ni Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akitoa hotuba ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Gelard Mweli (wa pili-kushoto) ili azungumze na washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa walimu, yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Wengine pichani kutoka kulia ni Kamishna wa TSC kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) Assela Luena, Kamishna wa TSC kutoka TAMISEMI Suzan Nussu na Katibu wa TSC Mwl. Paulina Nkwama.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama akizungumza wakati Naibu Katibu Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Gelard Mweli (wa tatu-kushoto) alipowatembelea na kuzungumza na washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa walimu, yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Wengine pichani kutoka kushoto ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza Mwl. Martin Nkwabi, Mwenyekiti wa TSC Prof. Willy Komba, Makamishna wa TSC Suzan Nussu kutoka TAMISEMI na Assela Luena kutoka NACTE.
Washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa walimu, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli (hayupo pichani) alipofika kuwatembelea na kuzungumza nao wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.
……………………………………………………………………………….
Na Veronica Simba – TSC
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli ametoa maelekezo kuwa upandishaji madaraja kwa
walimu uzingatie sifa zao katika kazi, hususan utendaji mahiri.Alitoa maelekezo hayo mwishoni mwa wiki, wakati alipozungumza na washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa walimu, yaliyofanyika jijini Mwanza.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), yalilenga kuwawezesha washiriki kufahamu na kutekeleza majukumu yao ya Tume kwa haki.
Akifafanua, Naibu Katibu Mkuu Mweli alisema kuwa, zipo sifa kadhaa zinazopaswa kuzingatiwa wakati wa upandishaji madaraja ambazo alizitaja baadhi kuwa ni pamoja na muda ambao mtumishi amekuwa kazini pamoja na utendaji kazi wake.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ni muhimu zaidi kuzingatia utendaji kazi wa Mwalimu kama sifa kuu ya upandishaji Daraja.
“Ukimpandisha Daraja asiyefanya kazi vizuri, ukamwacha mtendaji mzuri, unamvunja moyo anayefanya vizuri lakini pia inachangia kushusha hadhi ya taaluma ya ualimu,” alisisitiza.
Mweli aliendelea kusisitiza kuwa, ni vema kabla Mwalimu hajadai kupandishwa Daraja, ajitathmini utendaji wake kama anafaa kupanda au la.
Alisema iko mifano hai kadhaa ambapo baadhi ya Walimu wenye muda mfupi kazini wamekuwa watendaji mahiri kushinda wenye muda mrefu kazini, hivyo akasisitiza kuwa uwepo wa muda mrefu kazini usitumike kama kigezo pekee cha kumpandisha Mwalimu Daraja isipokuwa sifa hiyo iende sambamba na utendaji kazi.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu aliwataka watendaji wa TSC kushughulikia masuala ya walimu kwa haki, weledi na kwa wakati.
Alisema kuwa TSC ilianzishwa ili iwe Mkombozi kwa walimu na siyo kinyume chake hivyo akawataka watendaji katika ngazi zote kuwajibika ipasavyo ili walimu wajivunie uwepo wake.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa TSC, Katibu wake Mwl. Paulina Nkwama, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa, Tume itazingatia maelekezo yote aliyoyatoa ili kuendelea kutoa huduma nzuri kwa Walimu ambao ndiyo wadau wake wa kwanza.
Naye Mkurugenzi Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Christina Hape, alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuwa, TSC imejiwekea utaratibu wa ndani ambapo inahakikisha mashauri yote ya Walimu yanashughulikiwa ndani ya muda mfupi zaidi kulinganisha na ule uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo hayo yalihusisha Wilaya zote kutoka Mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita.
No comments:
Post a Comment