Aidha, katika kipindi hiki cha kipupwe upepo mkali wa kusi unatarajiwa kuvuma katika maeneo mengi ya nchi na vipindi vya baridi hasa katika maeneo ya miinuko.
Katika Taarifa iliyotolewe leo Mei 31, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi imesema katika miezi ya Juni hadi Agosti huwa ni msimu wa Kipupwe ambao huambatana na upepo wa kusi katika maeneo mengi ya nchi ambao hutokana na mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa Afrika huku vipindi vichache vya upepo vikitarajiwa kujitokeza pia.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hususani nyakati za usiku na asubuhi hiku vipindi vya baridi kali zaidi vikitarajiwa kujitokeza mwezi Julai 2021.
Amesema, mikoa itakayopata baridi chini ya nyuzi joto 6 ni ile ambayo iko kwenye maeneo yenye miinuko husani mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro, hivyo, inaweza kuleta athari kwa binadamu, wanyama, samaki pamoja na ustawi wa mazao mashambani hususani mazao ya muda mrefu kama migomba yanaweza kupata magonjwa ya fangasi na kudhoofisha ustawi wake.
Hali hii imesababishwa na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu linatarajiwa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.
Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa, hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya kawaida katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, maeneo ya Ukanda wa Pwani (Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Nyanda za juu kaskazini mashariki (Kilimanjaro, Arusha na Manyara), ukanda wa Ziwa Victoria na magharibi mwa nchi (Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma), hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya juu kidogo ya kiwango cha kawaida.
"Kwa upande wa maeneo ya kanda ya kati (Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini magharibi(Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe) na mkoa wa Ruvuma hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa chini kidogo ya joto la kawaida.
Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi amesema, vipindi vya Upepo wa Matlai vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara).
Aidha, katika ukanda wa Ziwa Victoria vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache.
Pia Dkt. Kijazi amesema, hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao.
Mamlaka inawashauri wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza
No comments:
Post a Comment