Pages

Thursday, April 1, 2021

MAKAMU WA RAIS DK.MPANGO AWAONYA MAWAZIRI NA MANAIBU WAZIRI WANAOVUTANA KAZINI..KATIBU MKUU KIONGOZI AFICHUA SIRI


 Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Mpango amempa waziri wa fedha Dk. Mwigulu Nchemba  majukumu ya

kushughulikia uhusiano wa kifedha kati ya Tanzania Bara na Visiwani huku akisisitiza atasimamia agizo hilo ambalo limetolewa na Rais.

Ameweka wazi kuwa pia Serikali itafuatilia mivutano ya mawaziri na manaibu mawaziri na kwamba Rais amezungumzia hilo na wamesikia lakini pia hali hiyo ya mvutano kati ya makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu kwenye Wizara, hivyo watafuatilia.

Akizungumza leo Ikulu Chamwino, baada ya kuapishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Mawaziri na Manaibu Mawaziri ametumia nafasi hiyo kueleza kuna umuhimu wa mawaziri kushirikiana ili kutekeleza majukumu yao.

Amesema jana Rais Samia Suluhu Hassan amezungumzia mvutano uliopo kati ya mawaziri na manaibu waziri na kwamba mvutano huo uishe na atasimamia maagizo hayo na wanafuatilia kwa karibu zaidi.

Dk.Mpango amesema kwamba mvutano pia upo kwa Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu katika Wizara nao wamekuwa wakivutana katika kutekeleza majukumu yao, amesema watafuatilia na watachukua hatua.

Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba kuhakikisha makusanyo ya fedha kwa mwezi yaongezeke hadi kufikia Sh.Trilioni mbili kwa mwezi na hilo linalowezekana.

Dk.Mpango amemtoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Ummy Mwalimu kuhakikiha anaisimamia vema Wizara hayo ambayo ina mambo mengi ambayo yanagusa maisha ya Watanzania.

Aidha Dk.Mpango amemtaka Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Ummy Mwalimu kuhakikisha anasimama imara katika kuisimamia Wizara hiyo kwani ina mambo mengi.

Awali akizungumza mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan , Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga amefichua siri kwamba leo alikuwa anatakiwa kurudi nchini Japani kuendelea  na majukumu mengine ya kikazi,lakini jana mchana akafuatwa na watu wakimuambia anatakiwa Dodoma na hakujua anaenda kufanya nini.

Akizungumza zaidi, Balozi Katanga amesema akiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati anasubiri ndege akawa anaangalia televisheni hivyo akaona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

"Nilikuwa niondoke leo kwenda Japan, tiketi nilikuwa nayo tayari,ila nachokumbuka jana mchana nikafuatwa na watu wananiambia natakiwa kwenda Dodoma, na nikiwa uwanjani nikaona Rais ameniteua. Nikuahidi Rais nitatekeleza majukumu yangu kama yanavyoelekeza kwa mujibu wa Katiba.

Pamoja na hayo,Balozi Katanga amezungumzia umuhimu wa Taasisi na Wizara zote kufanya kazi kw kushirikiana kwani Serikali ni moja."Wizara na tasisi zimewekwa ili kuleta ufanisi na lazima iwepo Serikali inayofanya kazi pamoja kufikia malengo ya ya 2025.

"Na kama tuna safari ya kwenda mwaka 2025 tufahamu kuwa tuko barabarani, na ili tufike lazima tusubiriane wote ili twende pamoja kati ya Wizara moja na nyingine, tutafika bila kuachana njiani.Hivyo  najua kazi yangu ina changamoto lakini Serikali iko vizuri katika kutekeleza majukumu yake,"amesema .

 

No comments:

Post a Comment