Pages

Thursday, April 1, 2021

JAJI MKUU, SPIKA WA BUNGE WATOA YA MOYONI KWA VIONGOZI WALIOPISHWA IKULU NA RAIS SAMIA



Charles James, Michuzi TV

JAJI Mkuu wa Tanzania, Ibrahim Juma amewataka viongozi wote

walioapishwa leo Ikulu na Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa huku akitoa wito kwa mawaziri watatu ambao wizara zao zinagusa moja kwa moja mambo ya kimahakama.

Amewataja mawaziri na wizara zao kuwa ni pamoja na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi huku pia akimsifu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga.

Ametoa sifa kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Katanga akimsifu kwa namna ambavyo aliisaidia Mahakama ya Tanzania kufanya maboresho huku akisema anaamini mahusiano yake aliyoyatengeza akiwa Balozi wa Tanzania nchini Japan yatasaidia kuifanya Tanzania kuwa mshindani wa Japan kiuchumi.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Job Ndugai amewapongeza wateule wote walioapishwa huku akitoa wito kwa Watumishi wote wa umma kuwa na kasi ya utendaji kazi, uvumilivu na nidhamu ili kuweza kukua katika nafasi zao.

" Mfano wa mtu mvumilivu na mwenye nidhamu ni Katibu Mkuu wetu Kiongozi Balozi Katanga ambaye nimemtambua kwa muda mrefu, ameanza akiwa chini kabisa lakini amepanda hadi leo ni Katibu Mkuu Kiongozi, niwaombe tuwe na nidhamu na utii katika kazi," Amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai amewataka walioteuliwa wote kuchapa kazi kwa bidii kwani Rais Mama Samia ameonekana ni kiongozi asiyetabiriki hivyo Ili waendelee na nafasi zao ni vema wakaendana na kasi ya Rais Mama Samia.

 

No comments:

Post a Comment