Na Amiri Kilagalila, Njombe
WASHTAKIWA
watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji namba 84 ya mwaka 2014
ya Alice Mtokoma (56), mkazi wa kijiji cha Usalule kilichopo mkoani
Njombe wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Wakisomewa
shtaka hilo leo Machi 31, 2021 na mawakili wa serikali Andrew Mandwa na
Matiko Nyangelo katika kikao cha mahakama kuu kilichofanyika mkoani
Njombe mbele ya Jaji Firmin Matogolo, walisema watuhumiwa hao Mei 13,
2012 walimuua kwa kumpiga Alice Mtokoma kwa kitu chenye ncha kali, kosa
ambalo ni kinyume na kifungu cha sheria na 196 na 197, kanuni ya
adhabu, sura ya 16, marejeo ya 2019.
Wakili
Nyangelo alieleza kuwa siku ya tukio hilo, watuhumiwa walimfuata
nyumbani kwake marehemu na kumueleza kuna sehemu wanatakiwa kwenda naye
ndipo walipotekeleza mauaji hayo.
Hukumu
hiyo ya kunyongwa hadi kufa kwa washtakiwa hao ilitolewa na Jaji
Matogolo katika kikao cha Mahakama Kuu kilichofanyika mkoani Njombe.
Alisema
washtakiwa waliohukumiwa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ni James
Msumule, Emmanuel Ngailo, Izack Ngailo, Anitha Mbwilo na Upendo Mligo.
Alisema
chanzo cha washtakiwa hao kutekeleza mauaji hayo ni kutokana na kifo
cha mume wa Upendo Mligo, ambaye ni mtoto wa Anitha Mbwilo lakini baada
ya kifo hicho ndipo wawili hao walikwenda kwa mganga ili kubaini chanzo
cha kifo cha kijana huyo.
Alisema
baada ya kwenda kwa mganga waliambiwa kuwa aliyemuua kijana wao ni
marehemu Alice Mtokoma ambaye alikuwa mke mwenzie na mshtakiwa Anitha
Mbwilo.
"Baada
ya kupewa maelezo hayo ya mganga, Anitha na Upendo walikula njama ya
kutafuta watu ili kumuua Alice Mtokoma," alisema Matiko.
Alisema
Upendo Mligo na Anitha Mbwilo waliwatafuta washtakiwa wengine watatu
ambao ni James Msumule, Emmanuel Ngailo na Izack Ngailo na kuwapa kiasi
cha fedha Sh300,000 ili wafanye mauaji hayo.
Kutokana
na kosa hilo walilotenda washtakiwa hao, Jaji Matogolo aliwahukumu
adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kufuata kifungu 197 cha kanuni ya
adhabu, sura ya 16 marejeo ya 2019, ikisomwa pamoja na kifungu 322
(1)(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20, marejeo ya
2019.
No comments:
Post a Comment