Pages

Wednesday, March 31, 2021

SERIKALI YAUNGANISHA MFUMO WA TANePS NA GePG KUONGEZA UFANISI


……………………………………………………………………………………

 Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imesema kwa sasa Mfumo wa Manunuzi ya Umma (TANePS) tayari umeunganishwa na

Mfumo wa kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya Serikali ili kuongeza ufanisi.

Hayo yameelezwa Bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Ukonga Mhe. Jerry Silaa alieuliza Serikali haioni haja ya kurejesha mfumo wa TANePS Hazina ili ukatekelezwe na kusimamiwa pamoja na GePG katika kuongeza ufanisi.

Alisema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410 pamoja na kanuni zake, Serikali inaendelea kuboresha utendaji wa Mfumo wa TANePS ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi na haioni haja ya kuuhamishia mfumo huo Hazina kwa sasa.

“Kifungu cha 9 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma kimeipa nguvu Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuanzisha na kusimamia mifumo na taratibu zote zinazohusu  masuala ya ununuzi wa umma ikiwa ni pamoja na mfumo wa TANePS”, alisema Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Alibainisha kuwa Mfumo wa TANePS umetayarishwa kukidhi matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ambayo imeweka misingi na taratibu za ununuzi wa umma inayohimiza uwazi, usawa na haki katika michakato ya ununuzi ili kuipatia Serikali thamani halisi ya fedha zinazotumika katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali.

Kwa upande mwingine, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alisema kuwa wateja waliowekeza amana inayozidi shilingi milioni 1.5 katika Benki ya Wananchi Meru kabla ya kufungiwa kutoa huduma za kibenki mwaka 2018 watalipwa kiasi kilichobaki chini ya zoezi la ufilisi.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za ufilisi, kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za Benki husika ambapo zoezi la kukusanya madeni na mali za Benki ya Wananchi Meru linaendelea.

Hayo aliyasema alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Arumeru Mashariki aliehoji ni lini Serikali itatoa amana na hisa za wateja waliokuwa wamewekeza katika Benki ya Wananchi Meru kabla ya kufungiwa.

“Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Februari 2021, jumla ya shilingi bilioni 1.47 zimeishalipwa kwa wateja waliokuwa na amana katika Benki hiyo. Malipo hayo ni sawa na asilimia 78.70 ya kiasi cha shilingi bilioni 1.86 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia”, alieleza Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Alisema kuwa jumla ya wateja waliolipwa ni 4,679 kati ya wateja 13,138 ikiwa ni asilimia 35.61 ya wateja wote waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliifutia leseni ya kufanya biashara ya kibenki Benki ya Wananchi Meru kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Aidha iliiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi ambapo ilianza zoezi la kulipa fidia ya Bima na Amana ya hadi shilingi milioni 1.5 na zoezi hilo linaendelea.

 

No comments:

Post a Comment