WAJUMBE wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), ukiongozwa na Mwenyekiti wao Profesa Mayunga Nkunya umesema umefurahishwa na
kuridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea kwenye Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere ambao unatarajiwa kumalizika Juni 15 mwaka 2022.Aidha wajumbe hao wametumia nafasi hiyo kueleza wazi namna ambavyo Rais Dk.John Magufuli ambavyo amedhamiria kuleta maendeleo ya nchi yetu kwa kufanya miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambayo yote inatekelezwa kwa fedha za Watanzania wenyewe.
Akizungumza baada ya kukagua na kuona shughuli za ujenzi katika mradi huo baada ya wajumbe wa bodi ya wakururugenzi wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa bodi hiyo Profesa Nkunya amesema wameridhishwa na kasi ya ujenzi na hakika Tanzania inakwenda kuandika historia kwani mradi utakapokamilika kutakuwa na umeme wa kutosha,uhakika na gharama nafuu.
"Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ujenzi la Taifa tunampongeza sana Rais John Magufuli kwa kuvalia njuga mradi huu na kuhakikisha unatekelezwa, kihistoria mradi huu umezungumzwa kwa muda mrefu bila mafanikio.
"Lakini kwa Rais Magufuli ameweza,anastahili pongezi na sisi Bodi ya Wakurugenzi tunampongeza ,tumeona kasi ya ujenzi, na wasimamizi wametueleza kwa kina hatua mbalimbali za ujenzi zinavyokwenda na tumeshuhudia kwa macho yetu,"amesema Profesa Nkunya.
Amesisitiza viongozi waliomtangulia Rais Magufuli walikuwa wanafikiria huo mradi hautekelezeki kwa sababu ya gharama na mengineyo, lakini unatekelezeka na ni muhimu kwa taifa letu."Hivyo tunamshukuru Rais kwa kufanya uamuzi mgumu na kufanikisha kujenga mradi huu wakati huu ambapo tunajitayarisha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na tunajenga reli ya SGR ambapo umeme utahitajika sana."
Aidha amesema wamefurahishwa na utalaamu wa hali ya juu ambao unatumika kujenga bwawa hilo na la kufurahisha zaidi ni idadi kubwa ya watalaamu wanaojenga na kusimamia kwa sehemu kubwa ni Watanzania, hivyo ni mradi ambao mbali ya nishati ya umeme, lakini umesaidia kujenga na kukuza uwezo wa Watanzania katika kuwawezesha kutekeleza miradi mingine kwa miaka mingine ijayo.
Akizungumzia sababu za kufanya ziara hiyo ambayo pia ilihusisha menejimenti ya baraza hilo akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu Dk.Matiko Mturi, Profensa Nkunya amesema kwamba wao wamefanya ziara hiyo kuona shughuli za ujenzi zinavyoendelea.
Prof. Nkunya amesema " Huu mradi ni mkubwa na wa kihistoria, hivyo ni fursa kubwa kwetu kuja kuona kujifunza.Pia mradi huu ni mgeni, una vitu vipya na sisi kama Baraza la Ujenzi kati ya vitu ambavyo tunafanya ni kuweka viwango ambavyo vitaweza kutusaidia katika miradi kama hii baadaye."
Hata hivyo amesema wamejifunza miradi mikubwa ya aina hiyo inahitaji watalaam wengi na waliobobea katika maeneo mbalimbali,kwani wameelezwa pamoja na kuwepo mradi mkubwa lakini kuna miradi mingine midogo midogo kati ya tisa hadi 10 na yote inakwenda sawa.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Mturi, amesiaitiza kwamba mradi huo ni mkubwa na Rais Magufuli amechukua uamuzi mgumu kuutekeleza na leo ujenzi unatekelezwa kwa kasi na Rais amethibitisha tukiamua hakuna kitakachoshindikana.
"Tumekuja kuutwmbelea mradi huu kwasababu ukiambiwa tu hauwezi kuelewa ukubwa wa mradi huu na hata kufahamu kinachoendelea lakini ukifika utaona kazi kubwa inayofanyika , hivyo Bodi ya Wakurugenzi na menejimeti tumeamua kuja kuona kinachofanyika.
"Tulichokiona katika mradi huu ni kikubwa sana, mradi ni mmoja, lakini una miradi 10 ndani yake inaendelea na yote inakwenda kwa uwiano sawa,hakuna mradi unaojengwa na kuzidi mwingine, watalaam wa ndani wanafanya kazi nzuri na hili ni jambo ambalo limetupa faraja sana baraza la ujenzi la Taifa,"amesema.
Pia amesema katika Serikali ya Awamu ya Tano, watanzania wanashuhudia miradi mikubwa ikiendelea kutekelezwa wakati huko nyuma miradi mingi iliyokuwa ikitekelezwa ni ile midogo midogo.Dk.Mturi ameongeza pia kwenye mradi huo wameona namna ya ushiriki wa watu wa kawaida ambao nao wanashiriki katika ujenzi huo.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi huo,Meneja Msimamizi wa Mradi kutoka Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Said Kimbanga amewaambia wajumbe hao wa bodi kwamba kasi ya ujenzi inakwenda vizuri na ujenzi umefikia asilimia 60 na matarajio yao utakamilika Juni 15,2022." Itakapofika Juni 15 ,2022 saa tisa alasiri Watanzania watapata umeme utakaozalishwa hapa Bwawa la Mwalimu Nyerere."
No comments:
Post a Comment