Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 24,2021 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali lenye lengo la kuongeza kasi katika kuchukua tahadhari kujikinga na magonjwa ya mlipuko na magonjwa katika mfumo wa hewa.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima,akiwa ameshika kitakasa mkono ambacho wananchi wanatakiwa kutumia ili kuchukua tahadhari kujikinga na magonjwa ya mlipuko na magonjwa katika mfumo wa hewa.
Serikali imewataka viongozi wa Serikali, sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii na Viongozi wa
Dini wa Madhehebu mbalimbali kuacha kusubiri matamko zaidi bali waamke na kuwajibika katika nafasi zao katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ya mlipuko katika maeneo yao.Hayo yamebainishwa leo Februari 24,2021 Jijini Dodoma na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akitoa tamko la Serikali lenye lengo la kuongeza kasi katika kuchukua tahadhari kujikinga na magonjwa ya mlipuko na magonjwa katika mfumo wa hewa.
Dkt Gwajima amesema imefika wakati kwa kila kiongozi katika nafasi yake kuendelea kutoa tahadhari juu ya namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali badala ya kusubiri serikali itoe tamko.
“Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameshafanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa matamko ya kukumbusha na kuelimisha taifa juu ya mwelekeo wa tahadhari za kuchukua ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Vilevile, Viongozi wa Wizara ya Afya tumetoa matamko mbalimbali ya kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari” amesema Dkt Gwajima.
Dkt Gwajima amesema jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni la kila mtu katika nafasi yake kuhakikisha wanachukua tahadhari kujikinga na magonjwa hayo.
Ameongeza kuwa “niwakumbushe viongozi wa Serikali na sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii, Viongozi wa Dini wa Madhehebu mbalimbali ngazi zote tuache kusubiri matamko zaidi bali tuamke tuwajibike kila mmoja kwa nafasi yake” amesema.
Amebainisha kuwa kila mwaka katika kipindi cha Novemba hadi Machi wimbi la magonjwa yanayoathiri mifumo ya upumuaji na chakula huongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa huku ikiwatoa wasiwasi Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Magonjwa hayo yanaweza kusababishwa na vimelea vya bakteria, virusi na fangasi huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali ikiwemo hewa, kula au kunywa kitu ambacho siyo kisafi na salama.
“Mwenendo huu wa magonjwa ni kila mwaka na kipindi hiki tumeshuhudia Dunia ikipambana na wimbi la pili la mlipuko wa ugonjwa wa COVID- 19,kwa msingi huu tunahitaji kuongeza kasi zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya mwenendo huu wa magonjwa yote haya kwenye kipindi hiki” amesema
Dkt Gwajima amesema ni vyema wakafanya ufafanuzi tena juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kutekeleza hatua za tahadhari za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na milipuko kwa ujumla wake ikijumuisha na tahadhari dhidi ya tishio la mlipuko wa COVID-19.
Amesema kwanza wananchi wanatakiwa kuondoa hofu zinazojengwa bila sababu na nia njema, kwa sababu hofu inaleta madhara zaidi kiafya.
“vifo vingi vinavyotokea duniani asilimia 90 hutokea kwasababu watu wanatanguliza hofu zaidi,”amesema
Aidha Dkt Gwajima amewataka wananchi kuendeleza tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, wanatakiwa kutumia vipukusi (sanitizer).
Dkt Gwajima ameongeza kuwa “Namuelekeza mfamasia mkuu wa serikali kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani tunaweza kutengeneza vipukusi vyetu vya ndani ya nchi ili kuwezesha wananchi kupata kwa bei nafuu ambayo kila mwananchi ataweza kuimudu” amesema .
Aidha amemuelekeza mfamasia mkuu wa serikali kutangaza orodha ya watengenezaji wa barakoa ambao tumeshawathibitisha, pia elimisha jinsi ya kutengeneza barakoa binafsi. vaa barakoa kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na wizara hususan katika maeneo ya msongamano.
Pia amesema kila mwananchi anatakiwa kufanya mabadiliko ya tabia ya lishe anayotumia kwa kuhakikisha unapata lishe bora ikiwemo matunda na mbogamboga kwa gharama nafuu kulingana na mazingira ya vyakula vya asili katika eneo lako.
“Naelekeza wataalamu wa lishe ngazi zote kuandaa daftari la orodha ya vyakula vya asili vinavyopatikana eneo husika na kutoa elimu ya milo ipi iandaliwe kama kielelezo cha lishe bora. tuache kuamini kuwa lishe bora ni vyakula vya kisasa vya biashara na vya bei ghali,” amesema.
No comments:
Post a Comment