Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOM
WAZIRI
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy
Gwajima amemwagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya
namna ya kutengeneza vipukusi kupitia taasisi mbalimbali nchini ili
kusaidia wananchi kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu zaidi ili kuweza
kujikinga dhidi ya magonjwa yakuambukiza na yasiyoambikiza.
Dkt.
Gwajima ametoa maelekezo hayo leo wakati akitoa tamko la kuongeza kasi
ya utekelezaji wa hatua za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na
yasiyoambukiza katika Kongamano la Mkutano Mkuu wa Wataalamu wa
Maendeleo ya Jamii nchini.
"Namuelekeza Mfamasia Mkuu wa
Serikali kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani tunaweza kutengeneza
vipukusi vyetu vya ndani ya nchi kupitia taasisi zetu, zilizo karibu
zaidi na wananchi ili kuwezesha wananchi kupata huduma hii ya vipukusi
kwa bei rahisi zaidi hali itakayosaidia kujikinga dhidi ya magonjwa"
amesema Dkt. Gwajima.
Ameendelea kusema kuwa, tuendeleze tabia
ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayo tiririka na sabuni.
Iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, tumia vipukusi (sanitizer).
Hata
hivyo, amewataka wananchi kuvaa barakoa safi na salama ambayo
wametengeneza wao mwenyewe au wamenunua kwa watengenezaji wa ndani
waliothibitishwa na Wizara ya Afya mfano Bohari ya Dawa, taasisi za
afya na watengenezaji wengine ambao wamethibitishwa.
Vile vile
amemwelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali kutoa elimu ya jinsi ya
kutengeneza barakoa binafsi na kuwataka wananchi kuvaa barakoa kwa
kuzingatia muongozo uliotolewa na Wizara hususan katika maeneo ya
msongamano, huku akimwagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kutangaza orodha
ya watengenezaji wa barakoa ambao wamesha thibitishwa.
Pia, Dkt.
Gwajima ameendelea kutoa wito kwa wananchi kufanya mazoezi mara kwa
mara, baadhi ya mazoezi rahisi kama vile kutembea kwa kasi siyo chini ya
dakika 30 au zaidi walau utoke jasho, kuruka kamba, kukimbia mwendo
unaoona unakufaa na kufanya zoezi la kusimama na kukaa.
Hata
hivyo ameendelea kusisitiza matumizi ya tiba asili kwa dawa za kunywa na
kujifukiza zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili kama inavyoelimishwa
na wataalamu husika, na kuwaagiza waratibu wa tiba asili ngazi zote za
mkoa na halmashauri kuendelea kutoa elimu kwenye redio za maeneo yao.
Amewataka
wananchi, kuepuka misongamano isiyo ya lazima ikiwemo kwenye vyombo vya
usafiri, huku akiwataka wananchi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma
za afya mara waonapo dalili za maradhi ili watoa huduma wapate nafasi
nzuri zaidi ya kutoa matibabu.
Pages
▼
No comments:
Post a Comment