Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau akizungumza na WanaApolo wakati akitoa elimu ya kuepuka utoroshwaji wa madini na kukupa kodi ya Serikali katika machimbo ya Tanzanite.
Mwenyekiti wa WanaApolo Idd Kondo Malamsha akizungumza na wanaApolo kwenye mkutano na viongozi wa MAREMA Tawi la Mirerani.
Na Mwandishi wetu, Mirerani
CHAMA cha wachimbaji madini Mkoani Manyara MAREMA Tawi la Mirerani, limetoa elimu
kwa wafanyakazi migodini WanaApolo ambao waliomba wasipekuliwe na mameneja na wamiliki wa migodi kwani hawatoroshi madini na hawakwepi kulipa kodi ila wapekuliwe wakifika kwenye lango la kutoka kwenye ukuta unaozunguka machimbo hayo.
WanaApolo hao waliyasema hayo wakati wakizungumza na viongozi wa MAREMA Tawi la Mirerani, waliofika kwenye migodi yao na kutoa elimu juu ya elimu ya udhibiti na kutotorosha madini ya Tanzanite.
Mmoja wa wanaApolo hao Amani Mushi amesema kitendo cha mameneja wa migodi kuwapekua mifukoni pindi kunapotokea uzalishaji siyo zuri kwani wanaweza kuwadhulumu na pia huwa hawapewi mishahara hakuna sababu ya kuwapekua.
Mushi amesema wao hawatathubutu kutorosha madini ila hawataki kitendo cha kupata madini yao na kuwaonyesha mameneja na wamiliki wa migodi, kwani watawapokonya na kukosa haki zao na wapo mameneja na wamiliki wenye tamaa watawapora na kuwafukuza kazi.
MwanaApolo mwingine Noel Mbise amesema lengo lao wanaApolo ni kulinda rasilimali ya serikali kikamilifu, hivyo wanaiomba serikali kuwasaidia kuwafungulia dirisha lao wenyewe kwenye tathimini bila kuwashirikisha mameneja na wamiliki huku wakisema kodi ya serikali watalipa kama kawaida isipokuwa wakiotoka madini chini mgodini mameneja na wamiliki wasihusishwe nayo.
Mwenyekiti wa WanaApolo Idd Malamsha amewashukuru MAREMA kwa kushirikiana nao kwa lengo la kuhakikisha maslahi ya wanaApolo yanazingatiwa na kutetelewa ili kupata haki zao.
“Sisi chama chetu tumekisajili hivi karibuni na tunapaswa kukutana mara kwa mara ili kutambua changamoto zinazotukabili na kuzitatua kwa ajili ya maslahi yetu WanaApolo,” amesema Malamsha.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau amekiri kuwa wanaApolo wamekuwa mstari wa mbele katika suala la kudhibiti utoroshaji wa madini ukilinganisha na wadau wengine kwani ni wachache waliokamatwa wakiwa na madini wakitaka kutoka nje ya ukuta na mara kwa mara wamemshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuweka ukuta ili kudhibiti utoroshaji wa madini na kulipa kodi.
Njau amesema Rais John Magufuli anawapenda wachimbaji, Waziri wa Madini Dotto Biteko pia anawapenda wanaApolo isipokua kubwa ni namna na kudhibiti watoroshaji wa madini ili kudhibiti mapato ya serikali.
“Kama mnakumbuka hivi karibuni Rais John Magufuli alisema kuna utoroshaji wa madini, hivyo hata Waziri wa madini Dotto Biteko alipokuja hapa Mireani siyo kwamba aliota si mlimsikia kwenye vyombo vya habari Rais alisema hili?” alihoji Njau.
Amesema hakuna wanaApolo wengi waliokamatwa na madini kama wapo ni wawili au watatu, hivyo ukikamatwa na madini getini miaka 10 hutaingia getini, huwezi kuajiriwa Tanzania kwani picha yako itatembezwa kila mahali, magereza wataenda, hawatachimba popote, hivyo wahakikishe wanaipenda kazi yao, wanakuwa wazalendo katika hilo ili kulinda rasilimali ya Tanzania kwa manufaa ya wote.
“‘MwanaApolo kama mwanaApolo anaruhusiwa kuwa na Tanzanite cha msingi hakikisha meneja wako anafahamu hilo na mmiliki wako analifahamu ondoka na Tanzanite hadi kwenye tathimini unaruhusiwa, ila usifiche jiwe lako baadaye meneja akasingizia hujasema kama una jiwe amekukuta umeficha,” amesema Njau.
Mjumbe wa Marema Tawi la Mirerani, Japhari Matimbwa amewataka Wanaapolo kuhakikisha wanakua wazalendo katika kufuata taratibu, sheria, kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la udhibiti na utoroshaji wa madini.
Matimbwa amesema Rais John Magufuli ameweka misingi imara na madhubuti ya kuhakikisha wachimbaji wadogo na wakubwa wote wanapata stahili zao kulingana na taratibu zilizoweka, hakuna atakayeonewa wala kudhurumiwa katika hatua yoyote, cha msingi tu ni kuhakikisha watu wanakua wazalendo.
“Pamoja na hayo hakikisheni mnawapa ushirikiano viongozi wenu wanaApolo kwani hawa ndiyo watetezi wenu kabla hamjaja kwetu MAREMA na tulishirikiana nao kwenye kuhakikisha kazi inafanyika kipindi cha agizo la kulipwa mishahara au kupewa asilimia 10 madini yakitoka hivyo wanaosema hawawatambui mnakosea,” amesema Matimbwa.
No comments:
Post a Comment