Na Estom Sanga- Dodoma
Naibu
Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF
umeendelea kuwa kichocheo muhimu katika kupiga vita umaskini nchini na
hivyo kuutaka Uongozi wa Mfuko huo kuboresha zaidi huduma zake ili
ziwafikie wananchi wanaozihitaji kwa ufanisi zaidi.
Mhe.Ndejembi
amesema kutokana na mchango wake muhimu katika kupiga vita dhidi ya
umaskini , Serikali imeendelea kuuamini Mfuko huo na kuupa fursa ya
kupata fedha ili uweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Ametoa
rai hiyo mjini Dodoma alipotembelea ofisi za TASAF na kukutana na
Watumishi wa Mfuko huo walioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake ,
Ladislaus Mwamanga akiwa katika ziara ya kujitambulisha na kuona
utendaji kazi wa taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo kufuatia uteuzi
uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John
Pombe Magufuli mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Aidha
Mhe. Ndejembi ameuagiza Uongozi wa TASAF kufanya tathmini za huduma
zitolewazo na mfuko huo mara kwa mara ili kujiridhisha ikiwa Walengwa
wake wanatumia vizuri fursa zitolewazo na pale inapobainika kuwa
Walengwa wanakiuka misingi ya kuanzishwa kwake hatua madhubuti
zichukuliwe mara moja.
Akitoa
taarifa ya utendaji kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus
Mwamanga ameeleza namna Mfuko huo ulivyosaidia jitihada za Serikali za
kuwahudumia wananchi hususani wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri .
Amesema kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Walengwa wamefanikiwa
kuboresha makazi yao, kusomesha watoto , kupata huduma za Afya kwa
uhakika baada ya kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii,kuanzisha miradi ya
kiuchumi na kujiongezea kipato.
Bwana
Mwamanga pia amesema kuanzia mwaka huu TASAF itaanza kutekeleza maagizo
ya Rais Mhe. Dr. John Pombe Magufuli ya kuwafikia wananchi watakaokidhi
vigezo vya umaskini uliokithiri katika mitaa, vijiji na shehia kote
nchini.
Adha
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha
Mfuko huo kupata fedha za ndani na Wafadhili jambo ambalo amesema
limeupa nguvu zaidi ya kuwafikia Walengwa nchini kote kwa wakati na kuwa
sekta za elimu, afya na maji pia zitapewa msukumo katika utekelezaji wa
Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF.
Kuhusu
uhakiki wa Walengwa Mwamanga amesema suala hilo ni endelevu na limekuwa
likitekelezwa kila baada ya miezi miwili ili kuondoa uwezekano wa
kunufaisha watu ambao hawajakidhi vigezo vya Mpango.
No comments:
Post a Comment