Mkuu wa Kituo cha TVLI_Kibaha Dr Stela Bitanyi akionyesha nanna bora ya kuhifadhi sampuli za chanjo za mifugo.
TAASISI
ya Utafiti wa Chanjo za Mifugo Tanzania (TVLI) Kibaha iliyopo chini ya
Wakala wa Maabara ya Utafiti wa Mifugo (TVLA) ilianzishwa mwaka 2012
ikiwa na jukumu la kuhakikisha inadhibiti magonjwa ya mifugo yaliyopewa
kipaumbele nchini.
Katika
utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikikumbana na changamoto ya
upungufu wa vifaa kwa maabara yenye ubora wa kusaidia udhibiti wa chanjo
za magonjwa ya kimkakati, kwa miaka ya hivi karibuni Taasisi ilikuwa
inazalisha chanjo mbili (2), na kwa sasa imefikisha chanjo sita (6) huku
kukiwa na mkakati wa kufikisha chanjo nane (8) mpaka kumi na tatu (13)
kwa mwaka 2022.
Mwaka
2018, Taasisi ya TVLI ilipata ruzuku kutoka Serikalini kupitia Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kujenga maabara ya
kudhibiti ubora wa chanjo.
Maabara
hiyo imeshakamilika na kuanza kutumika. Taasisi ya TVLI inatengeneza
makundi ya aina mbili (2) za chanjo: kundi la kwanza ni chanjo dhidi ya
bakteria na kundi la pili ni chanjo dhidi ya virusi ambazo zote ubora
wake huthibitishwa katika maabara hii.
Kwa
kutambua umuhimu wa chanjo ya mifugo na kuongezeka kwa idadi ya chanjo
zinazozalishwa ili kuthibitisha ubora wake, kabla ya kuzipeleka kwa
wakulima, COSTECH ilitoa ruzuku iliyofanikisha ujenzi wa maabara
inayosaidia kupata chanjo zenye ubora.
Kwa
sasa maabara imekamilika ina vifaa vyote muhimu vya kupima na
kuthibitisha ubora wa chanjo pamoja na uteketezaji wa uchafu
utakaozalishwa na maabara (laboratory waste). Hii imeongeza tija katika
vipimo vya chanjo kwa kuzingatia ubora kabla hazijapelekwa kwa wafugaji
pamoja na wadau wengine wenye uhitaji huo.
Meneja
wa kituo, Dkt Stella Bitanyi anasema TVLI ipo kwenye mazungumzo ya
kupima ubora wa chanjo zitakazozalishwa na viwanda binafsi wakianza na
kiwanda cha Hester Biosciences International kinachoendelea kujengwa
mjini Kibaha.
Uwepo
wa maabara hii umechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa chanjo kutoka
aina tatu (3) zilizokuwa zinazalishwa kabla ya maabara hii mpaka kufikia
aina sita (6) ambazo ni chanjo ya: Mdondo wa kuku, Kimeta, Chambavu,
Homa ya mapafu ya Ng’ombe, Mchanganyiko (Kimeta na Chambavu) pamoja na
Ugonjwa wa kutupa mimba kwa ng’ombe.
Vilevile
mradi huu umesaidia kuongeza tija na ufanisi kwa wafanyakazi, wakulima,
wazalishaji na waagizaji wa chanjo nchini, hatimaye kukuza pato la
Taifa, kuimariisha afya (lishe bora) na kuongeza wigo wa biashara.
No comments:
Post a Comment