Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili nyingi zinazoweza kuifanya nchi hii kuondokana kabisa na umasikini na utegemezi, hivyo kujiendesha bila kutegemea misaada toka nje ya nchi.
Licha ya kuwa na hifadhi za taifa za wanyama, bahari, maziwa, mito na
milima na mabonde, nchi hii imejaliwa pia kuwa na madini, bidhaa muhimu
kwa maendeleo ya kiuchumi.
Takriban madini aina zote yanayopatikana duniani yapo Tanzania ikiwemo
Tanzanite inayopatikana nchini pekee. Huu ni utajiri kwa vizazi na
vizazi endapo Yyataendelea kudhibitiwa, kusimamiwa,kulindwa na kutumiwa
ipasavyo. Yataliingizia Taifa mabilioni ya shilingi.
Juhudi za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kutumia vizuri
rasilimali ya madini zimeifanya Tanzania kuingiza mabilioni ya fedha
ambazo zinatumika katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo
ya Afya, Elimu na Miondombinu ya barabara, reli na umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ambaye ni muasisi wa mageuzi
makubwa katika Sekta ya Madini, Dkt. John Pombe Magufuli anasema haya
kuhusiana na madini: “Kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio
makubwa kwenye sekta ya madini. Mapato yameongezeka kutoka shilingi
bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020.
Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka
asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019.”
Aliongeza kwa kusema, “Zaidi ya hapo, kwa mara ya kwanza, katika
historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa
kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7.
Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge la 11 kwa kutoa mchango mkubwa
katika kupatikana kwa mafanikio haya.”
Fedha iliyopatikana kutokana na madini yaani bilioni 527 inaweza kutoa
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka na nusu, inaweza kujenga
vituo vya afya 1,150 au inaweza kulipia gharama ya elimu ya awali hadi
sekondari kwa kipindi cha miaka miwili (yaani miezi 24).
Sekta ya Madini ikiendelea kusimamiwa vyema maendeleo makubwa katika
nchi yatapatikana na kuibadilisha Tanzania kiuchumi na kuingia uchumi wa
kati wa juu hadi kufikia uchumi wa juu wa nchi zilizoendelea kama vile
Marekani, Uingereza, Sweden Ujerumani, China na nyinginezo ndani ya
kipindi kifupi.
Akionyesha dhamira yake ya dhati kuhusu mchango wa madini katika kukuza
uchumi wa Taifa, Rais Magufuli aliongeza, “Kwenye miaka mitano ijayo,
tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa madini yetu, (kama
tulivyofanya kwa kujenga Ukuta Mirerani) kwa kuimarisha Sheria zetu ili
madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato. Aidha,
tunakusudia kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kwa
kuzingatia mfano wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kampuni
ya Barrick yaliyowezesha kuundwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals
Corporation.”
Ujenzi wa ukuta wa Mirerani umedhibiti kwa kiwango kikubwa utoroshwaji
wa Tanzanite na kufanya nchi hii kupata mauzo makubwa ya madini hayo.
Zaidi ya hayo amepatikana bilionea mzawa kutokana na udhibiti huo Bwana
Saniniu Laizer ambaye amejipatia zaidi ya shilingi bilioni11kwa kuiuzia
Serikali ya Tanzania madini ya Tanzanite.
Aliyekuwa Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema,“Ujenzi wa ukuta
kuzunguka machimbo ya madini eneo la Mirerani na kuweka vifaa vya ulinzi
na usalama ili kuhakikisha kuwa madini yaTanzanite ambayo ni rasilimali
ipatikanayo Tanzania pekee inalindwa. Kufuatia uwekezaji huo, sote
tumeshuhudia kuongezeka mara dufu kwa mapato yatokanayo na madini ya
Tanzaite katika eneo hilo hususan kutoka kwa wachimbaji wadogo kutoka
shilingi 166,094,043 kabla ya kujenga ukuta hadi shilingi 2,150,000,000
baada ya kujengwa kwa ukuta.”
Lilikuwa jambo la kushangaza kuona Tanzania haikuwa ya kwanza wala ya
pili hata ya tatu kwa kuuza Tanzanite duniani wakati madini hayo
yanapatikana Tanzania pekee katika dunia nzima. Uelekeo wa sasa
utaifanya nchi hii kuwa kinara katika uuzaji madini hayo. Na kwa kufanya
hivyo pato la Taifa litaongezeka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alinukuliwa akisema haya kuhusu kudhibiti
utoroshwaji wa madini, “Katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini,
Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa
mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi.
“Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi
wa madini 28 kote nchini.”
Aliongeza kuwa masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha
upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali
kabla ya kuanzishwa kwake.
“Masoko haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa
kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama
wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha
biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya,”alisema Waziri Mkuu.
“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu,
almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel, copper, n.k. Aidha, tuna gesi
aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni
zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo
zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku
nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni
tajiri sana”,alisema Rais Magufuli hivi karibuni wakati akizindua Bunge
la 12 jijini Dodoma.
Rais Magufuli alibainisha juhudi nyingine za Serikali kwa kusema:“Kuhusu
madini pia, kwenye miaka mitano ijayo pia tutaendelea kuliimarisha
Shirika letu la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki kikamilifu
kwenye shughuli za madini; kuwawezesha wachimbaji wetu wadogo, ikiwa ni
pamoja na kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapatia mafunzo, mikopo
pamoja na vifaa. Na natambua kuwa, wapo baadhi ya watu wamepewa leseni
za utafiti na uchimbaji lakini hawajazifanyia kazi; tutazifuta leseni
zao, na maeneo hayo kuyagawa kwa wachimbaji wengine, hususan wachimbaji
wadogo. Wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kukuza sekta ya madini.”
Serikali itaendelea kuimarisha masoko ya madini pamoja na kuhamasisha
ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji
wa bidhaa za madini.
Haya yote yanalenga pia kuongeza thamani ya madini na kuongeza ajira
hasa kwa vijana zitakazotokana na shughuli zinazohusu madini kama vile
uchenjuaji na utengenezaji wa bidhaa za madini
“Tunataka madini yachimbwe hapa Tanzania, yachenjuliwe, yayeyushwe na
kisha bidhaa za bidhaa za madini zitengenezwe hapa hapa Tanzania; na
ndipo ziuzwe nje ama watu kutoka nje waje kununua bidhaa za madini hapa
nchini. Ni imani yetu kuwa, kutokana na hatua tulizopanga kuzichukua
sekta ya madini itaweza kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa
ifikapo mwaka 2025, alisisitiza Rais Magufuli.
Mchango wa asilimia 10 kwa Pato la Taifa utakuwa mchango wa maana ambao utasaidia katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi mkubwa utakaosaidia kuboresha maisha ya watanzania.
No comments:
Post a Comment