Moja ya Ghala lililojengwa na Shirika la MIICO katika kijiji cha Katete, Wilayani Kalambo.
Mkutano wa Mgeni rasmi mwakili wa Mkuu wa mkoa pamoja na wananchi uliofanyika ndani ya Ghala hilo lenye thamani ya Shilingi milioni 107.6 katika kijiji cha Katete.
Mwakili wa Mkuu wa mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akikata utepe ishara ya kuzindua mradi wa ujenzi wa maghala matatu uliotekelezwa na Shirika la MIICO chini ya udhamini wa Shirika la Maendeleo Agra.
Mwakili wa Mkuu wa Mkoa Dkt. Khalfan Haule (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi na Wataalamu mbalimbali kutoka Shirikala la MIICO, Shirika la Maendeleo Agra, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.
…………………………………………………………………………………..
Shirika la MIICO kupitia utekelezaji wa mradi wa PiATA TIJA TANZANIA umeikabidhi
serikali ya Mkoa wa Rukwa maghala matatu yenye thamani ya Shilingi 322,990,050 ili yatumiwe na wakulima waliojiunga katika vyama vya ushirika katika vijiji vya kimkakati ambavyo maghala hayo yamejengwa na hatimae kuwaondolea wakulima adha ya kuhifhadhi mahindi katika nyumba zao.Akizungumza katika taarifa yake Afisa Mradi wa Ujenzi wa Maghala hayo Daniel Palingo amesema kuwa Shirika hilo limefanikiwa kujenga maghala matatu ya kuhifadhia mazao katika wilaya tatu za mkoa wa Rukwa katika vijiji vya Sakalilo Wilayani Sumbawanga, Katete Wilayani Kalambo na Katongolo Wilayani Nkasi ambapo Maghala hayo yana ukubwa wa Mita za mraba 2700 yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 1980 za mazao huku yakiwa yamefikia asilimia 89 ya ujenzi wake.
“Maghala haya ni nguzo kubwa kwa vyama vya msingi vinavyo yatumia, vyama hivi vya Silunda, Sakalilo na Umoja wa umwagiliaji Katongolo vinahudumia jumla ya wakulima 7000 na Zaidi katika huduma za masoko na upatikanaji wa pembejeo.Maghala haya matatu yamekuwa ni ya muhimu sana kwa wanufaika kwani yalianza kutumika hata kabla hayajakamilika, mathalani Ghala la hili limeweza kutumika na chama cha msingi cha Silunda ambapo wameweza kuhifadhi Tani 60 za mahindi na Tani 12.5 za mbolea kwaajili ya msimu ujao wa kilimo,” Alisema.
Halikadhalika, Msimamizi Mshauri waShirika la Maendeleo la Agra katika Mkoa wa Rukwa na Katavi, Japhet Laizer aliiomba serikali kuona namna ya kuweza kuvisaidia vyama vya ushirika kwa kuwaondoa viongozi wabovu katika vyama hivyo ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya wakulima wengi na kusababisha wakulima kutokuwa na Imani na vyama hivyo na hivyo lengo la serikali la kuunganisha wakulima kushindwa kufanikiwa kama inavyotarajiwa.
“Tunaiomba serikali, wawe mara kwa mara wanajitahidi kuvipitia hivi vyama vya ushirika, vya ma vya ushirika kwa upande mwengine vimekuwa ndio vya kupiga na kuwaumiza wakulima, hivyo tunaiomba serikali ipitie mara kwa mara katika kutatua changamoto za vyama vya ushirika ili mwisho wa siku tuone wakulima wananufaika na uwekezaji huu, katika taarifa mmeweza kusikia pia tumewekeza katika sekta binafsi, ukipitia kwenye maghala yanayosimamiwa na watu binafsi unakuta mazao yamejaa mpaka hakuna nafasi, lakini ukienda kwenye maghala yanayosimamiwa na vyama vya ushirika unakuta hakuna hata gunia moja la mahindi,” Alisisitiza.
Wakati akitoa nasaha zake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema kuwa wakulima wengi katika Mkoa wamekuwa wakiuza mazao yao mara baada ya kuvuna ili kukidhi mahitaji mbalimbali yanayowakabili na kiasi kinachobakia kimekuwa kikihifadhiwa katika nyumba zao na kuongeza kuwa hiifadhi hizo si salama na ni hatarishi hasa pale wanapotumia viuatilifu kwa ajili ya kuua na kuzuia wadudu waharibifu.
“Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imekuwa ikiweka mikakati ya muda mrefu na mfupi ya kutatua changamoto za uhifadhi wa mazao katika Mkoa. Mikakati hiyo ni pamoja na kukarabati maghala yaliyopo katika Mkoa na kujenga maghala mengine.Katika mkakati wa ujenzi wa maghala nashukuru shirika la MIICO kwa kujenga maghala Matatu katika Mkoa wetu,” Alisema.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali kupitia NFRA inajenga vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mahindi katika eneo la Kanondo na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo NFRA watakuwa wameongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kwa tani 25,000 na kufanya uwezo wao wa kuhifadhi nafaka kufikia tani 58,500.
Wakati akitoa neno la Shukran aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na Diwani wa Kata ya Katete Daudi Sichone aliushukuru uongozi wa mkoapamoja na serikali kwa ujumla katika kuhakikisha wanaendelea kuyashawishi mashirika mbalimbali kujenga miundombinu ili wakulima wasiendelee kupata shida ya kutimiza wajibu wao kwa serikali na familia zao.
Tofauti na Ujenzi huo wa maghala Shirika la MIICO limefanikiwa kukarabati maghala 18 kati ya mabovu 29 kwa mkoa mzima wenye jumla ya maghala 82 ambapo 53 ni mazima yenye uwezo wa kuhifadhi tani 22,800 za mazao huku NFRA ikiwa na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 33,500 kwa sasa kabla ya kumalizika kwa mradi wa vihenge na hivyo kuufanya mkoa kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 56,300 ambazo ni sawa na asilimia 19.5 ya ziada ya mahindi tani 293,914.59 yaliyopo mkoani Rukwa.
No comments:
Post a Comment