Elimu ya Mpiga Kura ni kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya mambo ya msingi yatakayowawezesha kutekeleza kwa usahihi jukumu la kupiga
Na Christian Gaya, HakiPensheni Center
Tume katika kutekeleza majukumu yake kikatiba, huratibu na kusimamia Uendeshaji wa Uchanguzi wa Rais, Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Uchaguzi wa Madiwani kwa
Tanzania Bara. Kifungu 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchanguzi, sura ya 343, kimeipa Tume mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kuratibu na kusimamia asasi na watu wanaotoa elimu hiyo.Katika kutimiza matakwa ya kifungu hicho, hivyo mtu anayeruhusiwa kupiga kura ni raia yeyote wa Tanzania aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na ana kadi ya kupigia kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi; na awe ni mkazi wa kawaida wa eneo analotaka kupigia kura au amehamia na taarifa zake zimehamishiwa katika kituo anachotaka kupiga kura.
Kituo atakachotakiwa kupigia kura ni kile alichotumia kujiandikisha na kupata kadi ya kupigia kura na mahali ambapo jina lake litaonekana.
Tume itatakiwa kubadika orodha ya wapiga kura kituoni siku nane (8) kabla ya siku ya uchaguzi. Ili mpiga kura aweze kujua kituo chake kilipo cha kupigia kura ataweza kutumia simu yake ya mkononi kwa kupiga namba *152*00# kisha atatakiwa kuchagua Uchaguzi Mkuu na kufuata maelekezo au atatakiwa kupiga simu ya bure namba 0800112100 ambayo ni huduma ya bure kwa Mpiga Kura. Aidha Makarani waongozaji watakuwepo katika vituo vya kupigia kura ili kuwasaidia wapiga kura kutambua vituo vyao.
Kituo cha kupigia kura kitabandikwa bango jeupe lililoandikwa KITUO CHA KUPIGIA KURA na nje ya kituo kutabandikwa mabango yanayotoa elimu ya Mpiga Kura.
Siku ya uchaguzi vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa MOJA kamili (1:00) Asubuhi na kufungwa saa KUMI kamili (10:00) Jioni kwa Tanzania Bara. Kwa Tanzania Visiwani-Zanzibar, Vituo vitafunguliwa saa MOJA kamili (1:00) Asubuhi na kufungwa saa KUMI na MOJA kamili (11:00) Jioni.
Mpiga kura atatakiwa kufika kituoni katika muda uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi; muda wa kupiga kura ukiisha hakuna mtu mwingine yeyote atakayeruhusiwa kupiga kura; kama muda ukiisha na wapiga kura bado wapo kwenye mstari, Askari wa kituo atatakiwa kusimama nyuma ya mtu wa mwisho mpaka wote watakapomaliza zoezi la kupiga kura.
Mpiga Kura anatakiwa kutunza kadi yake na kuitumia kwa ajili ya kupiga kura tu na siyo vinginevyo. Siku ya uchaguzi Mpiga Kura hatatakiwa kuvaa nguo zinazoashiria itikadi ya chama chochote cha siasa. Watu wenye ulemavu, mama wajawazito na wenye watoto wachanga walioenda nao kituoni, wazee na wagonjwa watapewa kipaumbele.
Na ikiwa jina la Mpiga Kura halitaonekana katika orodha ya wapiga kura kituoni, mpiga kura anatatakiwa kumwona Karani Mwongozaji wapiga kura ili asaidiwe kupata maelezo au kumwonesha kituo chake cha kupigia kura.
Kura Yako, Sauti Yako, Nenda Ukapige Kura
No comments:
Post a Comment