Meneja
wa Huduma za Sheria wa TMDA, Wakili Iskari Fute akizungumza katika
kikao kazi cha Uhamasishaji wa Waandishi wa Habari kuhusu Usimamizi wa
Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba.
Baadhi
ya Wanahabari wa Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam wakiwa
katika picha ya pamoja na maafisa waandamizi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa
Tiba (TMDA) wakati wa kikao elekezi mjini Morogoro.
Na Andrew Chale - Morogoro
MAMLAKA
ya Dawa na Vifaa Tiba nchini, (TMDA) imebainisha kuwa, hadi sasa
imefungua mashauri 146 kutokana na watu kukiuka sheria za mamlaka hiyo.
Hayo
yameelezwa Mjini hapa na Meneja wa Huduma za Sheria, Wakili Iskari
Fute, wakati wa kuwasilisha mada kuhusu Usimamizi wa Sheria ya Dawa na
Vifaa Tiba katika kikao kazi cha Uhamasishaji wa Waandishi wa habari
kutoka Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani.
Fute
alibainisha kuwa, TMDA imekuwa ikifuatilia kwa karibu masuala yote ya
kisheria na kuchukua hatua mbalimbali kwa watuhumiwa ikiwa ni kulinda
afya ya jamii.
"Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hadi kufikia sasa TMDA imefungua mashauri 146.
Kati ya mashauri hayo 146, yaliyokwisha na watuhumiwa kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kulipa faini ni 32.
Lakini
pia mashauri mengine 32 pekee ndio yamebaki hadi sasa na mashauri 82
uchunguzi wake unaendelea katika Mahakama na vituo vya Polisi." Alisema
Fute.
Fute
alibainisha kuwa, watuhumiwa hao waliofunguliwa mashauri baada ya TMDA
kufanya kaguzi mbalimbali za kushtukiza katika maeneo tofauti ikiwa ni
lengo la mamlaka kulinda afya ya jamii kupitia sheria ya Dawa na Vifaa
Tiba sura ya 219.
Aidha, Alieleza msingi wa sheria ya TMDA ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Sura ya 2 ibara ya 63 (c) na 64.
Ambapo Ibara hizo zinaweka mamlaka ya Bunge kutunga sheria zote.
"Kwa
vile haki ya kuishi kwa kila mtu inalindwa na Katiba, ni wazi kuwa
sheria ya TMDA inatekeleza masharti ya Katiba ya haki ya kuishi kwa vile
jukumu lake ni KULINDA AFYA ZA WATANZANIA". Alimalizia Fute
Kwa
upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Anza Ndossa
aliyekuwa Mgeni rasmi, aliwataka Wanahabari kutumia taaluma yao
kufikisha elimu pamoja na kufichua wakiukwaji wa sheria za dawa na vifaa
tiba.
No comments:
Post a Comment