Na Mohamed Saif, Geita
KATIBU
Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesitisha mkataba na
Mkandarasi Kampuni ya PET Cooperation Ltd na Al Baruwani Investment Ltd
kwa kushindwa kukamilisha kwa wakati mradi wa maji wa Nyamtukuza
Wilayani Nyang’hwale, Mkoani Geita.
Kwa
mujibu wa Msimamizi wa Mradi, Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Nicas Ligombi ni
kwamba utekelezaji wake umefikia asilimia 65 na ulianza kutekelezwa
rasmi Januari 2014 na ulipaswa kukamilika ndani ya miezi sita yaani
Julai 2014.
Katibu
Mkuu, Mhandisi Sanga alifikia uamuzi wa kusitisha mkataba na Mkandarasi
baada ya kutembelea mradi huo Agosti 1, 2020 ili kujionea utekelezaji
wake ambapo hakuridhishwa na hatua iliyofikiwa licha ya kuwa Mkandarasi
alikwishaelekezwa kuhakikisha unakamilika haraka na viongozi mbalimbali
waliowahi kuutembelea na kutoa maelekezo.
“Mkataba
ulikuwa wa miezi sita lakini sasa imefika miaka sita na kama sasa
ujenzi wake umefikia asilimia 65 kwa hesabu ya haraka inamaanisha kwamba
tukimuachia Mkandarasi aendelee tunahitaji miaka mingine mitatu yaani
mwaka 2023 ndipo ukamilike, hili halikubaliki,” alifafanua Mhandisi
Sanga.
Alisema
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
wakati wa kampeni Mwaka 2015 aliahidi wananchi watapa maji na
haitowezekana awamu yake ya kwanza ya uongozi inamalizika hali yakuwa
bado maji hayajawafikia wananchi.
“Mwaka
2015, wakati wa kampeni Rais aliahidi kufikisha maji hapa Karumwa Makao
Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, haitokuwa sawa arudi tena kuomba kura
hapa halafu ahadi yake aliyoitoa haijakamilishwa, hili sisi kama Wizara
hatuwezi kulikubali,” alisema Katibu Mkuu Sanga.
Alisisitiza
kuwa mkandarasi hatopewa muda wa nyongeza kukamilisha ujenzi badala
yake alielekeza mradi huo ukamilishwe na wataalamu wa ndani kwa mfumo wa
force account ambapo alimuelekeza Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Wakala ya
Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi
Deusdedit Magoma kuhakikisha anasimamia maelekezo hayo.
Mhandisi
Sanga alitoa siku mbili kwa RUWASA Mkoa wa Geita na Mwanza pamoja na
Mamlaka za Maji Geita (GEUWASA), Mwanza (MWAUWASA) na Mamlaka ya Maji
Kahama Shinyanga (KASHWASA) kufanya maandalizi ya kuanza ukamilishwaji
wa mradi.
“Siku
mbili zinawatosha kufanya maandalizi na ikifika Jumatano (Agosti 5,
2020) timu ya wataalam iwe imeripoti kwa Mkuu wa Wilaya tayari kwa
kuanza kazi na hakikisheni wataalam wanakuwa hapa muda wote na sio
kulala Geita na utekelezaji unapaswa kufanyika usiku na mchana hadi
mradi utakapoanza kutoa maji,” alielekeza Katibu Mkuu Sanga.
Alisema
kwa kuanzia ifikapo tarehe 5 Agosti, 2020 Wizara itapeleka kiasi cha
shilingi milioni 100 na kwamba kabla ya mwezi huu kumalizika fedha
nyingine itapelekwa.
Aidha,
akizungumzia hali ya ujenzi wa miradi ya maji nchini, Katibu Mkuu Sanga
alisema kuna zaidi ya miradi 1,425 inayotekelezwa kwenye maeneo
mbalimbali kote nchini ambapo kati yake ipo yenye changamoto na huku
akiutaja mradi huo wa Nyamtukuza kuwa mmojawapo baada ya mradi wa
Same-Mwanga.
Alisema
maamuzi yaliyofikiwa kwa miradi yenye changamoto ni wakandarasi wake
kusitishiwa mikataba na miradi hiyo kukamilishwa na wakandarasi wenye
uwezo pamoja na wataalam wa ndani kwa mfumo wa force account na kwamba
tayari mfumo huo umeonyesha mafaniko kwenye baadhi ya miradi ambayo
wakandarasi wameondolewa.
“Hatuwezi
kuwabembeleza wakandarasi, miradi yote ya Wizara ya Maji ambayo
inasuasua tunakwenda kuwapokonya na tutajenga kwa kutumia wataalamu wetu
wa ndani na pia wakandarasi hao hawatapewa tena kandarasi za miradi ya
maji, Serikali hii ya Awamu ya Tano inachohitaji ni kuona ni wananchi
wanapata maji, na sio maneno,” alisema Katibu Mkuu Sanga.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Wilson Shimo alimpongeza
Katibu Mkuu Sanga kwa maelekezo yake kuhusiana na mradi huo.
“Tumefurahishwa na maelekezo yako, tupo tayari kuwapokea wataalam wa
wizara utakaowaagiza kukamilisha mradi na tupo tayari kuwezesha makazi
yao na maandalizi mengine ili kurahisisha utekelezaji kwani hadi hivi
sasa tupo nyuma ya wakati,” alisema Shimo.
Naye
Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa
Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Deusdedit Magoma alisema
wameyapokea maelekezo na ni wajibu wao kuhakikisha utekelezwaji unaanza
mara moja.
“Sisi
kama RUWASA hatujaridhishwa na hali ya ujenzi; nimepokea maelekezo na
tutajitahidi kuhakikisha tunakamilisha hata kabla ya siku hizo 60
tulizoelekezwa,” alisema Mhandisi Magoma.
Mradi
wa Maji wa Nyamtukuza unatarajiwa kunufaisha wakazi 38,000 kutoka
vijiji Nyamtukuza, Nyarubele, Nyantukara, Kitongo, Ikangala, Kakora,
Kayenze, Izunya, Bukwimba na Kharumwa.
Ziara hiyo Mkoani Geita ni ya kwanza kwa Katibu Mkuu huyo tangu ameteuliwa na kuapshiwa rasmi kushika nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment