…………………………………………………………………………….
Napenda kuvipongeza vyombo vya
ulinzi na usalama kwa kugundua kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rufiji Bw. Brighton Kilimba alitoa taarifa za uongo kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Magufuli kuwa gari ya
wagonjwa ya Kituo cha Afya Ikwiriri haiwezi kutembea kwa sababu ni
mbovu na inahitaji matengenezo makubwa.
Nikiwa mtumishi wa Wilaya hii
niliumia sana kwa sababu nilikuwa najua ni uongo wa
mchana kweupe na
niliumia zaidi kwa kuwa aliyekuwa anadanganywa ni Rais wangu
ninayempenda Dk. John Pombe Magufuli.
Hata hivyo nilifurahi muda mfupi
baadaye nilipomuona kwenye mitandao ya kijamii Bw. Brighton Eliud
Kilimba, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji akiwa
kwenye pingu na bango linaonesha anatuhumiwa kumdanganya Rais. Nikasema
kweli vyombo vya ulinzi na usalama sasa hivi vipo makini na havijalala.
Ukweli ni kwamba gari ya wagonjwa
ya Kituo cha Afya Ikwiriri ipo na viongozi waliamua tu kuipaki wakati
wananchi wanahangaika kupeleka wagonjwa wao Jijini Dar es Salaam pale
wanapohitaji matibabu ya rufaa.
Gari hilo ni zuri, ni aina ya
Toyota Landcruizer namba STL 940, ni gari imara na limekuwa msaada
mkubwa sana kwa wananchi kabla viongozi hawajaamua kulipaki na kuwaacha
Wananchi wanahangaika kukodi magari kwa gharama kubwa na wakati mwingine
kupanda bodaboda, ni jambo la kusikitisha sana kwa viongozi
kutotekeleza wajibu wao kiasi hiki.
Kumbe siku ile Mheshimiwa Rais
alipopita Rufiji na kulalamikiwa na wananchi juu ya ukosefu wa gari la
wagonjwa, gari lilikuwepo na lilikuwa limetelekezwa katika Kituo cha
Afya Ikwiriri likiwa halina tatizo lolote zaidi ya kuhitaji kufanyiwa
service ya kawaida ya kubadilishwa oil na pengine kubadili matairi yake.
Kaimu Mkurugenzi Bw. Kilimba
alipokuwa anamdanganya Rais kuwa gari ni bovu sana na haliwezi kutembea,
Rais kwa machale akaamua kuagiza gari hilo lipelekwe TEMESA mara moja,
nikajua hapa siri lazima itafichuka.
Kwa kuwa gari halikuwa gereji kama
Bw. Kilimba alivyosema hadharani, alichofanya Bw. Kilimba ni kupiga
simu na kuagiza gari hilo lipelekwe gereji mara moja ili maafisa
watakapofuatilia wakute lipo gereji, jamaa wa gereji waliposikia hivyo
machale yakawacheza wakakataa kulipokea na ndipo maafisa wakagundua kuwa
gari halikuwa gereji ambako Rais aliambiwa na halikuwa bovu kama Rais
alivyoambiwa. Ni michezo tu ya viongozi.
Navipongeza sana vyombo vya ulinzi
na usalama kwa kugundua mchezo huu, na kisha kumkamata na kumweka ndani
Bw. Kilimba ambaye ni Afisa Kilimo wa Wilaya.
Aidha, nampongeza Rais Magufuli
kwa hatua alizochukua siku ileile hata kabla hajafika Dar es Salaam kwa
kumtumbua Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Bw. Juma Njwayo ambaye ndio alikuwa
anaongoza kutoa taarifa za uongo kuhusu ubovu wa magari. Hawa wote ni
tatizo kubwa sana hapa Rufiji na yapo mengi ya hovyo wanayafanya, endapo
uchunguzi wa kina utafanyika yatabainika vizuri.
Naamini hili litakuwa funzo kwa
viongozi wengine kuwajibika ipasavyo katika kuwatumikiwa wananchi kama
ambavyo Mheshimiwa Rais Magufuli anasema kila siku, kuwatumikia wanyonge
vizuri badala ya kuwaacha wanahangaika wakati Serikali inajitahidi
kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi.
Msimamo wa Mheshimiwa Rais wa
kuagiza gari hilo litengenezwe ndani ya wiki 1 na wakati gari
linatengenezwa gari la Mkurugenzi ndilo litumike kubeba wagonjwa ni
ujumbe tosha kuwa sisi watumishi ni lazima tuweke maslahi ya wananchi
mbele na tuwatumikie kama ambavyo tunapaswa kufanya.
Asante Mheshimiwa Rais kwa uongozi wako makini unaojali watu hasa wanyonge.
Pichani ni Bw. Brighton Kilimba na gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Ikwiriri.
Ni mimi Mtumishi
Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
02 Agosti, 2020.
Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
02 Agosti, 2020.
No comments:
Post a Comment