Kaimu Katibu Mtendaji Baraza
la Kiswahili Tanzania Consolata Mushi akitoa taarifa kwa
Waziri wa
Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe kuwa taasisi
yake tayari imekwisha sajili jumla ya wahitimu 1224 katika kanzidata ya
wataalamu wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wageni,leo jijini Dodoma
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa wahadhiri wa Kiswahili katika
chuo kikuu cha Dodoma.
……………………………………………………………………………………….
Na. Anitha Jonas – WHUSM, DODOMA
Baadhi ya watanzania wamekuwa na
hulka ya kutokuwa na matumizi sahihi ya baadhi ya maneno ya lugha ya
Kiswahili, hali ambayo imesababisha Baraza la Kiswahili Tanzania
(BAKITA) ikiwa ni taasisi yenye dhamana kuanza kutoa elimu sahihi
yamatumizi ya maneno ya lugha hiyo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa BAKITA
Bibi. Consolata Mushi, hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwa njia ya
simu na Afisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya
Habari, Bibi. Anitha Jonas alisema kuwa baadhi ya watumiaji wa lugha ya
Kiswahili wamekuwa wakifanya makosa ya matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Aidha, Bi.Consolata alisema kuwa
baadhi ya maneno yamekuwa yakitumiwa kimakosa na utumiaji huo umepelekea
kuibua mgogoro wa kifikra miongoni mwa watumiaji wa lugha husika hivyo
kuepukana na madhara yanayoweza kuwa makubwa ni bora kusahihisha
matumizi hayo.
“Nitoe mfano ambao ulisikika siku moja kupitia chombo fulani cha habari kuwa mtaalamu wa kilimo amewaasa wakulima kutumia mbolea, utumiaji wa namna hii si tu kwamba unapotosha bali unaharibu kabisa dhana nzima ya kile kinachosemwa,”alisema Bibi.Consolata
Akitolea mfano wa maneno ambayo yanapotoshwa ni neno ‘asa’ kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili
(2015) lina maana ya “Kanya au kataza mtu kufanya jambo fulani”, na
kusema kuwa matumizi hayo yanaweza kupotosha na kuharibu maana ujumbe
uliokusudiwa.
Vilevile, Bibi.Consolata
alifafanua matumizi sahihi ya neno ‘asa’ kuwa linaweza kutumika kwa
kuonya mfano: “Walimu wamewaasa wanafunzi kujiingiza katika matumizi ya
dawa za kulevya” au “Serikali yawaasa wazazi wanaowaachisha watoto wao
shule kwa ajili ya kuwaoza.
Kwa mujibu wa BAKITA neno lingine
ambalo limekuwa likipotoshwa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni
mrabaha, chanzo cha upotoshaji wa neno hilo ni ubadilishaji wa mpangilio
wa vitamkwa vya mwisho vinavyounda neno hilo, badala ya kusema mrabaha
watu husema mrahaba.
Mrabaha maana yake ni, “Malipo
yanayotolewa na mchapishaji kwa mtunzi wa kitabu kwa kipindi fulani kama
sehemu ya mauzo ya kitabu kinachohusika, au inaweza kuwa ni “Malipo
yanayotolewa kama sehemu ya faida inayotokana na biashara fulani.
Halikadhalika, neno mrahaba halina
maana yoyote katika lugha ya Kiswahili hivyo utumiaji wa neno hilo ni
upotoshaji na watu wengi wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi yake.
****************MWISHO******
No comments:
Post a Comment