Wananchi
wa Kijiji cha Kwastemba wilayani Kilindi, mkoani Tanga wakiwa kwenye
mkutano wa kijiji wakipatiwa elimu kutoa kwa maofisa wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) kuhusu sumukuvu, madhara yake na jinsi ya
kudhibiti kwenye mazao ya mahindi na karanga. Mkutano huo ulifanyika
wiki hii. Na mpiga picha wetu.
Na Mwandishi Wetu, TangaWANANCHI wa Wilaya za Handeni na Kilindi, mkoani Tanga wamepatiwa elimu ya kuwajenga uelewa kuhusiana na sumukuvu, madhara yake na jinsi ya kukabiliana.
Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi hao na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutokana na Shirika hilo kuwa na dhamana ya kudhibiti usalama wa chakula nchini.
Akizungumza na gazeti hili mkoani hapa wakati wa utoaji elimu hiyo, Ofisa Usalama wa Chakula Mkuu wa TBS, Dkt. Candida Shirima, alisema elimu hiyo imetolewa kwenye wilaya hizo kwa kuwa zipo kwenye ukanda wenye hali ya hewa inayowezesha ustawi wa fangasi wanaozalisha sumukuvu kwenye mazao ya chakua hususan mahindi na karanga hivyo ni muhimu wananchi wake wakafahamu jinsi ya kudhibiti sumu hiyo.
Dkt. Shirima alisema TBS imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la sumukuvu kwa lengo la kulinda afya ya jamii na kuwezesha biashara ya mazao ya chakula.
Alifafanua kuwa TBS imechukua hatua hiyo muhimu ya kutoa kipaumbele katika kuelimisha jamii namna ya kukabiliana na sumukuvu hususan katika kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya mahindi ili wananchi waweze kufahamu taratibu muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kukabiliana na sumukuvu katika mnyororo wa mazao kuanzia yanapokuwa shambani na baada ya kuvunwa wakati wa kukausha, usafirishaji, uhifadhi na uandaaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Shirima, sumukuvu (mycotoxins) ni sumu zinazozalishwa na jamii ya fangasi kwenye mazao ya chakula na kwamba mazao yanayoathiriwa zaidi ni nafaka hasa mahindi na mbegu za mafuta hasa karanga. Sumukuvu huweza kuzalishwa kwenye mazao wakati yakiwa katika hatua mbalimbali kuanzia shambani na baada ya kuvunwa endapo taratibu bora za kilimo, uvunaji, ukaushaji, usafirishaji, uhifadhi na uandaaji hazitazingatiwa.
Wananchi wakifuatilia elimu kuhusu sumukuvu Alieleza kuwa mambo yanayowezesha uzalishaji wa sumukuvu ni pamoja na uwepo wa jamii ya fangasi husika na kuchochewa na hali ya hewa ya joto kali na unyevu, ukame na wadudu waharibifu.
Wataalam wa TBS wametoa elimu ya sumukuvu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na wananchi wengine kwa ujumla katika wilaya za Kilindi na Handeni kupitia kwenye mashule, masoko, minada, mikutano ya vijiji, magulio, kliniki za mama na mtoto na maeneo mengine ya biashara.
Kupitia elimu liyotolewa, jamii ilielimishwa pia kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na sumukuvu ambayo huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na maumivu ya tumbo, kuathirika kwa ini na hata kifo endapo mtu atakula kiwango kikubwa sana cha sumukuvu ambacho mwili hautaweza kukihimili. Aidha, sumukuvu huweza pia kusababisha madhara yanatokea baada ya muda mrefu ambayo ni pamoja na saratani ya ini, upungufu wa kinga mwili na udumavu.
Kuhusu namna ya kudhibiti sumukuvu kwenye mazao, Dkt. Shirima alihimiza hatua muhimu zichukuliwe kabla na baada ya kuvuna mazao.
Alitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupanda kwa wakati mbegu zilizothibitishwa na taasisi za udhibiti wa viwango vya ubora wa mbegu, kuhakikisha shamba ni safi wakati wote, kutumia viuatilifu mara wanapoona dalili za visumbufu (wadudu, magonjwa) kwenye mazao, kuvuna kwa wakati na kuondoa mazao shambani mara baada ya kuvuna.
Aliwaambia walengwa wa elimu hiyo kwamba kuchelewa kuvuna au kulundika mazao muda mrefu shambani huchochea uzalishaji wa sumukuvu.
Kuhusu udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao baada ya kuvuna, Dkt. Shirima aliwaambia walengwa wa elimu hiyo kuwa baada ya kutoa mazao shambani, taratibu nyingine zote zinazofuata zifanyike kwa umakini ili kuzuia mazao kupata mashambulizi ya fangasi wanaozalisha sumukuvu.
Kwa mujibu wa Dkt. Shirima baada ya mazao ya mahindi na karanga kuvunwa, ni muhimu kuchambuliwa vizuri ili kuondoa taka, unji zilizooza, zilizobadilika rangi, zilizo hafifu, zilizopasuka na zilizoharibiwa na wadudu.
“Ni muhimu mazao yaliyooza na yaliyoharibika yasitumike kama chakula au kutengenezea pombe. Pia yasiuzwe na yasilishwe wanyama,”alisisitiza Dkt. Shirima.
Aliwataka wananchi kuepuka kuanika mazao moja kwa moja kwenye udongo au sakafu kwani huchochea uzalishaji wa sumukuvu na badala yake wanatakiwa kuanika kwenye vichanja au vifaa vingine vya kuanikia mfano mkeka, turubai au jamvi ili kuepuka mazao kugusana na udongo.
Aidha, alisema mazao ya nafaka na karanga yanatakiwa kukaushwa hadi yakauke vizuri kabla ya kuhifadhiwa kwani yasipokauka ipasavyo hubakia na kiwango kikubwa cha unyevu ambao huchochea uzalishwaji wa sumukuvu.
Kuhusu udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao wakati wa kuhifadhi, Dkt. Shirima aliwataka wananchi kuhakikisha ghala au chumba cha kuhifadhi mazao kinakuwa katika hali nzuri.
“Ni muhimu kuhifadhi mazao kwenye ghala au chumba kisafi, kinachoruhusu mzunguko wa hewa, kutumia vifaa vyenye ubora kama vile magunia, mifuko au mapipa kuhifadhia mazao na kuepuka kuchanganya mazao ya zamani na mazao mapya,”alisema na kuongeza;
Wanafunzi wakipatiwa elimu kuhusu sumukuvu “Weka mazao juu ya vichanja na epuka kuweka moja kwa moja kwenye sakafu au udongo, hakikisha sehemu ya kuhifadhia haiingii maji au mvua, zuia wadudu waharibifu kwa kuweka viuatilifu vinavyopendekezwa na wataalam na kwa vipimo sahihi na kuzuia wanyama waharibifu kama vile panya” alisema Dkt. Shirima.
Dkt. Shirima aliwatoa wasiwasi walaji kwa kusema kuwa mahindi ni chakula chetu muhimu na hawapaswi kuwa na hofu hata kidogo bali jambo la msingi ni kufahamu kuwa endepo taratibu bora hazitazingatiwa wakati wa kilimo, uvunaji, ukaushaji, uhifadhi, usafirishaji na uandaaji, basi chakula huweza kuchafuliwa na sumukuvu. Kwa mantiki hiyo, ni muhimu sana kuzingatia kikamilifu ushauri unaotolewa na wataam ili kuepuka sumukuvu katika chakula chetu.
Wakizungumzia kuhusu elimu iliyotolewa, baadhi ya wananchi wa wilaya za Kilindi na Handeni waliishukuru Serikali kwa jitihada zinazofanyika ili kuhakikisha usalama wa chakula na kuahidi kutekeleza yote waliyofundishwa na kuwa mabalozi kwa wananchi na wakulima ambao hawatakuwa wamepata elimu hiyo.
Mmoja wa wananchi hao, Amina Salehe alisema kupitia elimu hiyo atahakikisha anafuata hatua zote alizoelekezwa ili kudhibiti sumukuvu kwenye mazao.
Kwa upande wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopata elimu hiyo walisema wataifikisha kwa wazazi wao na watasimama imara kuhakikisha mazao ndani ya familia zao hayashambuliwi na sumukuvu.
No comments:
Post a Comment