Katibu
Mkuu Wizara ya katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome akitoa hotuba ya
ufunguzi wa Mafunzo ya siku nne kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na
Magereza kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma
ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya
Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.
Washiriki
wa Mafunzo ya siku nne kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria
kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya-
jijini
Katibu
Mkuu Wizara ya katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya siku nne kwa maafisa
wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya
kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika
ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini
*******************************
Na: Karimu Meshack, Mbeya
SERIKALI
imewataka Polisi na Magereza nchini kuhakikisha haki na maslahi ya
mtoto
anayekinzana na sheria zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuhakikisha kuwa
shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome wakati
akifungua Mafunzo ya siku nne kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza
kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya
msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania
Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.
Prof. Mchome
amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau, kama vile UNICEF na wengine,
imeendelea kuzingatia maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria kwa
kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na
linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.
“Ni rai yangu
kuwa mnapokabiliana na kesi za watoto hakikisheni mtoto anapata msaada
wa kisheria mara unapokutana naye au kusikia habari zake. Kwa kuwa
mtakutana na watoto wa namna hii, ninaomba mafunzo haya yawakumbushe
wajibu wenu katika kumhudumia mtoto huyu ili haki itendeke kwa wakati.”
Hivi karibuni,
Mhe. Jaji Mkuu alitoa Kanuni za ushughulikiaji wa mashauri yanayohusu
watu wenye mahitaji maalum, wakiwamo watoto. Kanuni hizo zinaweka
masharti ya kuhakikisha upelelezi, uendeshaji na utoaji wa hukumu kwa
mashauri ya watoto unafanyika kwa wakati kutokana na changamoto zilizopo
katika mashauri hayo amesisitiza Prof. Mchome.
Aidha, Prof.
Sifuni Mchome ametaja hatua za zilizochukuliwa na Serikali katika
kuboresha mfumo wa haki jinai kuwa ni marekebisho ya sheria ya Mwenendo
wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kwa kuweka utaratibu wa kufifisha makosa
na kuimarisha mfumo wa upatanishi katika makosa ya jinai kwa lengo la
kupunguza mrundikano wa mashauri Mahakamani na kuondoa msongamano wa
mahabusu na wafungwa katika vituo vya polisi na magereza, hivyo kuwataka
mafisa wa polisi na Magereza kuzitumia njia hizo.
“Ninyi mnaopatiwa
mafunzo haya mnapaswa kuwa mabalozi kuonesha mfano kwa kuzitumia njia
hizi kwani zipo kwa mujibu wa sheria kuwezesha mfumo huo kufanya kazi
kwa mujibu wa Sheria. Kutokana na Wizara yangu kusimamia masuala ya
utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria na mfumo wa haki jinai, ni imani
yetu kuwa, kama wadau wakubwa, mtaitumia fursa hii kujitathimini na
kushiriki kujenga mfumo wa utoaji haki wenye tija usio na malalamiko kwa
wananchi.”
Akiwashukuru
UNICEF kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuunga mkono juhudi za
Serikali za kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuhifadhiwa Prof.
Mchome amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto
zinazomkabili mtoto anayekinzana na sheria katika maeneo mbalimbali
nchini. Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na UNICEF
pamoja na wadau wa haki mtoto, imeandaa Mkakati wa Haki Mtoto ambao
hivi karibuni utazinduliwa. Mkakati huu unalenga kuhakikisha kuwa wadau
wa masuala ya mtoto wanafanya kazi kwa pamoja katika kusimamia masuala
ya haki mtoto.
“Moja ya wadau
wakubwa katika mkakati huu ni Jeshi la Polisi na Magereza ambapo jukumu
lenu ni kubwa mno katika masuala ya haki mtoto. Mkakati huu unawalenga
watoto wote walioathirika na ukatili wa kijinsia, waliotenda makosa au
kujikuta kizuizini kutokana na mzazi kutenda kosa.”
Ni wazi kwamba
Mkakati huu kitakuwa chombo kinachoaminika na sehemu salama kwa mtoto
tofauti na ilivyo sasa ambapo kumekuwa na malalamiko ya watoto kupewa
umri mkubwa tofauti na uhalisia, amesisitiza Prof. Mchome.
“Ni rai yangu
kwamba Wadau wote tutashirikiana katika kuhakikisha ulinzi na ustawi wa
mtoto linakuwa ni jukumu letu la msingi. Hivyo, nawahimiza kwa mara
nyingine kujaribu kutumia njia mbadala za kushughulikia masuala
yanayohusu haki za mtoto badala ya kujielekeza katika kuwaweka vituoni
au magereza jambo linalosababisha msongamano.”
Mwaka 2017 Wizara
ya Katiba na Sheria ilisimamia mchakato wa kutunga na kupatikana kwa
sheria ya Msaada wa Kisheria Na 1 ya 2017. Pamoja na mambo mengine,
Sheria hiyo ina lengo la kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu
wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili. Aidha, sheria hii
imeweka masharti ya kutoa msaada wa kisheria katika mashauri ya jinai.
Ni kwa muktadha huo, Wizara ya Katiba na Sheria iliingia makubaliano na
Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2018 kuhusu utekelezaji wa masuala ya
msaada wa kisheria katika vituo vya Polisi na magereza nchini.
No comments:
Post a Comment