********************************
Na. Majid Abdulkarim, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
anayeshughulikia maswala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito na
kuwasisitiza watumiaji wote wa huduma za afya nchini katika zahanati,
vituo vya afya na hospitali za
halmashauri kutumia namba za huduma kwa
wateja zilizopo katika vituo hivyo ili kuwasilisha kero zao mahali
sahihi na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Dkt. Gwajima
ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaama akiwa katika ziara ya kikazi
ya kukagua uimarishaji mfumo wa huduma kwa wateja katika Hospitali ya
Mnazi Mmoja na Hospitali ya Sinza Palestina .
Aidha Dkt Gwajima
amesema, mahala sahihi pa kuripoti Kero za Wateja wakati wa kupata
huduma ni kwa Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Halmashauri, Mganga
Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI na ikishindikana hapo Wizara ya
Afya.
“ Ili kurahisisha
kero hizo kufika kwa wakati kila kituo cha kutolea huduma za afya
(zahanati, kituo cha afya na hospitali ya Halmashauri) sasa kinatekeleza
kuimarisha mfumo mzima wa huduma kwa wateja kwa kutumia utaratibu wa
kuweka namba za simu kwenye enao la wazi linaloonekana hususani pale
wanapokaa wateja kusubiria huduma hivyo, wateja wahakikishe wanapata
namba hizo na kuzitumia ili kusaidiwa kwa wakati”, amesisitiza Dkt.
Gwajima.
Dkt. Gwajima
amesema kuwa Wito huo umekuja baada ya kubaini uwepo wa matukio ya
baadhi ya watumiaji wa huduma za afya katika baadhi ya vituo kulalamikia
kero walizokutana nazo wakati wa kupata huduma za afya huku muda mrefu
ukiwa umepita hivyo, kukosa fursa ya kupata ufumbuzi kwa wakati.
Lakini pia Dkt
Gwajima amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini
ndani ya siku saba kuhakikisha mfumo huu unaimarishwa mara moja na
taarifa zinawafikia wananchi wote waanaotumia huduma katika maeneo
husika.
Kwa kuongezea
Dkt. Gwajima amesema kuwa, kila zahanati, kituo cha afya na hospitali ya
Halmashauri lazima iwe na bango kubwa lenye kuonesha namba maalumu ya
simu ya kituo kwa ajili ya kushughulikia kero za wateja wanaokuja kupata
huduma za afya vilevile, namba ya Mganga Mfawidhi wa Kituo husika,
namba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri, Mganga Mkuu wa Mkoa, namba za Ofisi
ya Rais TAMISEMI na namba ya Kituo maalumu cha Simu (Call Centre) cha
Wizara ya Afya ambayo ni 199.
“Na sisi kama
Ofisi ya Rais TAMISEMI leo tunatangaza namba maalumu ya kupokea Kero na
Pongezi kutoka kwa wateja juu ya utoaji huduma za afya katika hospitali
zetu za ngazi ya afya ya msingi na namba hiyo ni 0734124191. Hivyo,
iwapo Mteja utakuwa na Kero na hujapata msaada ngazi ya kituo, mganga
mkuu wa halmashauri na mkoa basi usiondoke na kero yako bali haraka tuma
ujumbe juu ya kero hiyo ukieleza uko Halmashauri gani na Kituo gani na
sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tutakupigia na kuchukua hatua stahiki za
kupata ufumbuzi juu ya kero hiyo kwa wakati sahihi” ameeleza Dkt.
Gwajima.
Dkt. Gwajima
amebainisha kuwa lengo la kuimarisha huduma kwa Wateja ni kutatua kero
zao kwa wakati na kuhakikisha kila mwananchi anayefika kwenye kituo cha
huduma za afya ngazi ya msingi anafurahia huduma hizo na haondoki huku
moyoni akiwa na manung’uniko yasiyo ya lazima.
Katika hatua
nyingine Dkt. Gwajima amewapongeza wataalamu wa sekta ya afya nchini kwa
kupokea kwa uzalendo na kutekeleza kwa vitendo mwelekeo wa kupambana na
kudhibiti ugonjwa wa Covid 19 kupitia maono makubwa ya Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwa.
“tuwe wabunifu na
tupigane vita hii bila hofu na kwa kuzingatia mazingira mahsusi ya nchi
yetu, Kupitia maono haya Covid 19 imedhibitiwa mapema sana na Tanzania
imeandika historia duniani juu ya mbinu za ubunifu na uzalendo juu ya
mapambano haya”ameeleza Dkt.Gwajima.
Dkt Gwajima
amesema, jukumu liliko mbele ya wataalamu wa huduma za afya nchini ni
kuimarisha utekelezaji wa miongozo ya kinga kwa ujumla ili uzoefu
uliopatikana uendelee kwa ajili ya kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza
na kuipungizia Serikali mzigo wa kuhudumia wagonjwa ambao wangeepuka
kuugua magonjwa hayo iwapo wangepata elimu ya kujikinga na kutekeleza
kwa vitendo mfano kunawa mikono.
“tusiache
kuendeleza hizi mbinu za usafi zinazolenga kujikinga na magonjwa ya
kuambukiza hususan kunawa mikono ili tudhibiti na kutokomeza kabisa
magonjwa hayo yakiwemo kipindupindu na magonjwa yote ya tumbo yatokanayo
na kula vyakula kupitia mikono isiyo safi” amesisitiza Dkt. Gwajima.
Naye Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam, Dkt.Rashid Mfaume amesema kuwa yeye kwa
kushirikiana na watendaji wenzake ndani ya mkoa wa Dar es salaam ndani
ya siku saba watakuwa wametekeleza agizo la kuhakikisha kunakuwa na
mfumo na utaratibu wa kupokea na kushughulikia kero za wateja kwenye
vituo vya huduma za afya kwa kutengeneza mabango makubwa yenye ubora wa
kipekee yakionesha namba za simu zilizoelekezwa ili wananchi wafahamu na
kuzitumia kwa wakati.
Huku Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt. Delila Moshi akiahidi
kutekeleza agizo hilo haraka sana kwa kusambaza mabango hayo kwenye
maeneo yote muhimu waliko wateja huku akitumia mfumo wa matangazo ya
sauti kuwafikia wateja wengi zaidi.
Kwa upande wake
Mratibu wa Huduma za Dharura na Maafa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.
Christopher Mzava ametoa wito kwa wahudumu wa afya kuendelea
kushirikiana kwa karibu na wateja ili kuweka mazingira mazuri ya kupokea
mrejesho juu ya huduma wanazotoa kwa ajili ya kufanya maboresho zaidi.
No comments:
Post a Comment