Na.WAMJW-Dar es Salaam
Wananchi wametakiwa kuendelea
kujifukiza kwa kutumia miti na mimea ya asili ikiwemo mwarobaini katika
kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti
wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR) Prof. Yunus Mgaya ametoa rai hiyo leo
jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa mti wa mwarobaini hauna madhara
yeyote bali ni mti wenye manufaa kwa tiba asili/mbadala ya magonjwa
mbalimbali.
Prof. Mgaya amesema
kumekuwepo na upotoshaji katika baadhi ya mitandao ya jamii ambayo
ilimnukuu kwa kusema kwamba mti wa mwarobaini haufai kujifukiza kwa
sababu una kemikali zenye sumu jambo ambalo si kweli.
“Mti wa mwarobaini unatibu
magonjwa arobaini,majani yake yanatumika kutibu minyoo,magamba
yanatumika kutibu homa na mafuta ya mti huu yanatumika kutengeneza
sabuni kwa ajili ya ngozi, hivyo mti huu ni mzuri na una manufaa makubwa
kwa jamii yetu”, Alisisitiza Prof. Mgaya
Aliongeza kuwa taasisi yake
ilifanya utafiti kupitia maandiko mbalimbali na kupata njia mbili za
kumpa nafuu mtu mwenye maradhi mbalimbali na kutaja njia hizo kuwa ni
dawa lishe ambayo ina virutubishi vinavyoweza kujenga na kuimarisha
kinga ya mwili ili mwili uweze kupambana na virusi na kumfanya mtu
apone.
Ametaja njia ya pili kuwa ni
kujifukiza kwa kutumia mimea au majani ya miti mbalimbali ambayo
husaidia kufunguka kwa mishipa ya damu,kufungua kifua kinachobana
pamoja na kuondoa uchovu na msongo wa mawazo.
“Mimea mingi ina mafuta
tete”essential oil” hivyo harufu mbalimbali za majani ya miti yanaingia
haraka mwilini na hivyo kusaidia kufanya mwili kutulia, kifua kufunguka
na lile joto linasaidia mishipa ya damu kufunguka na kufanya mfumo wa
hewa kuwa mzuri kwenye mwili wa mtu na aina hii ya tiba imetumika miaka
mingi barani afrika”.
Prof. Mgaya alisema kuwa katika
utafiti huo NIMR ilipata idadi ndefu ya majani ambayo yanatumika na
wananchi hususani Tanzania na makabila mbalimbali na hivyo walishauriana
kuweka makundi matatu na endapo mtu atapata mmoja wa mmea mmoja wapo
anaweza kujifukiza.
Alitaja kundi la kwanza ni
mkaratusi,kivumbasi (kashwagala) na mchaichai,kundi la pili ni
Karafuu(mbegu),tangawizi na limau(majani) na kundi la tatu alisema ni
mwarobaini na mpera na kusisitiza kuwa wakati wa kujifukiza joto lisiwe
kubwa na muda usizidi dakika kumi kwa watu wazima.
Hata hivyo alishauri vyombo vya
habari ni vyema kufika kwenye taasisi yake kuweza kupata taarifa sahihi
ambazo zitasaidia kutoa elimu kwa wananchi.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment