WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha mali zote za wakulima wa zao la
mkonge nchini zinarudishwa mikononi mwao na hakuna mtu yeyote
atakayeonewa.
“Tutarudisha mali zote za wakulima na ninawahakikishia hakuna mtu yoyote atakayeonewa,
kama
tulivyorudisha hizi mali za Bodi ya Mkonge Tanzania tutafanya hivyo
hivyo kote bila kumuonea yeyote na kuanzia leo Bodi hii ya Mkonge
imethibitishwa kuwa bodi kamili.”
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Juni 1, 2020) wakati akifungua jingo la
Bodi ya Mkonge Tanzania zilizopo jijini Tanga. “Mkonge ni fedha
Halmashauri wekeni vitalu mzalishe mbegu muwape wananchi bure. Kama
unashamba kubwa hujaliendeleza, kulingana na muda uliowekwa,
tutalichukua.”
Amesema
Serikali imedhamiria kulirudisha zao hilo, hivyo ametoa wito kwa
wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wajipange katika kuyafufua mashamba
yao na kuanzisha mapya na Serikali itawasaidia kuhakikisha mbegu bora na
pembejeo zinapatikana.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi katika kila mkoa wenye ardhi nzuri
ambayo inastawi zao hilo waanzishe kilimo cha zao mkonge walime na
Serikali itawasaidia bila kujali ni mtu mmoja mmoja, wakulima wa kati na
wakubwa.
“Wakuu wa
wilaya waondoeni Maafisa Kilimo waliopo Ofisini waende vijijini
wakawasaidie wakulima namna nzuri ya kulima zao hili kwa faida, mkonge
ni pesa, Serikali yenu itasimamia. Tunataka mkonge urudi kwenye nafasi
yake. Endeleeni kuwahamasisha walime mkonge, tunataka kila tunapopita
tuone mashamba ya mkonge.”
Ameiagiza
Bodi ya Mkonge kufanya utambuzi wa mashamba na wayarudishe kwa watu
walime. Pia mapori yote makubwa yaliyoko kwenye halmashauri ambayo
hayatumiki nayo wayatambue na waishauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ili nao wamshauri Rais Dkt. Magufuli kwa ajili ya
kugawiwa kwa wananchi waweze kulima.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu amesema amewahusisha wadau kutoka taasisi
mbalimbali za kifedha na kwamba Serikali imeweka utaratibu
utakaowawezesha wakulima wanaotaka kuboresha mashamba yao waweze kukopa.
“Nendeni Benki ya Kilimo mkachukue mikopo.”
“Zao la
mkonge ni muhimu nchini kwani linawanufaisha wakulima wadogo, wa kati na
wakubwa. Mkonge kwa Tanga ni uchumi kwa wananchi na ni mkombozi kwa
sababu unawawezesha kupata riziki zao. Zao hili hapo katikati halikuwa
na tija, zao hili lilikuwa linalimwa na mikoa zaidi ya 12 lakini sasa
limeachwa kwenye mikoa minne tu.”
Waziri Mkuu
amesema kwenye miaka ya 60 Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa
mkonge duniani, ambapo ilikuwa inazalisha tani 235,000 huku mahitaji ya
mkonge duniani yakiwa tani 550,000. “Tulikuwa tunazalisha zaidu ya nusu
ya mahitaji ya dunia, leo hii mchango wake haupo ukiuliza kwa nini
hakuna sababu. Serikali imeagizwa na CCM kuwa ni lazima zao hili lirudi
kwenye hadhi yake na litarudi.”
Kufuatia hali
hiyo, Waziri Mkuu ameagiza mikoa yote inayolima zao la mkonge kuanzia
sasa ijipange kwa sababu Serikali imeamua kulifufua zao hilo na inataka
kulirudisha katika nafasi yake, hivyo viongozi wahakikishe wanaendelea
kuwahamasisha wananchi walime kwa wingi.
“Tunataka
mkonge ushamiri, Bodi tumieni vyombo vya habari kuhamaisha wananchi
walime zao hili pamoja na kuwaeleza fursa zitokanazo na zao hilo.
Wawekezaji wetu panueni mashamba, leteni mitambo ya kuchakata mkonge
pamoja na vyote vitokanavyo na mkonge. Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga
amefanya kazi kubwa katika hili.”
Naye, Naibu
Waziri Kilimo, Omar Mgumba ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu
kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kusimamia sekta ya kilimo
likiwemo zao la mkonge. “Uadilifu wako na uzalendo wako ulikufanya uunde
kamati ya kuchunguza mali za Bodi ya Mkonge Tanzania na leo hii mali
zao zimerudi.”
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu utaingizwa kwenye kumbukumbu za Tanzania kwa kujitoa kwako
katika kuhakikisha zao hili linarudi kama ilivyokuwa awali. Tutafufuka
katika mikoa yote ambayo imeonesha inaweza kulima zao hili la mkonge,
lengo ni kuhakikisha zao hili linarudi kwenye hadhi yake.”
Kwa upande
wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kusimamia ajenda za maendeleo katika
mkoa wa Tanga, hususani zao la mkonge.
“Tunashukuru
uliporejesha hadhi ya zao hili.Tutawahimiza wananchi kulima mkonge kwani
tunaona muelekeo na maono ni makubwa sana, Tanga tunajivunia jitihada
hizi za maendeleo, uchumi wa Tanga utakuwa kwa kasi sana.”
Awali, Mbunge
wa Lushoto Rashidi Shangazi alisema wanaishukuru sana Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza
kuwarejeshea wananchi mashamba yao.
Nao, Wakuu wa
Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kilimanjaro waliishukuru Serikali kwa
kulifufua zao hilo na kwamba wameshaweka mipango ya kuendeleza zao hilo
na wameiomba Wizara ya Kilimo ishirikiane nao kwa kuwasaidia wakulima
katika kuendeleza zao hilo, ikiwemo uandaaji wa mashamba, uendelezaji
pamoja na utafutaji wa masoko. “Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi
zitusaidie kutenga maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji.”
No comments:
Post a Comment