Soko la Kisasa la Chuno lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Jengo la Old Boma Mikindani Mtwara Jengo hilo ni Kivutio cha Utalii wa Majengo ya Kale na Ni Hoteli ya Utalii kwa Sasa.
Barabara za Lami zilizojengwa Mtwara Mikindani na Nyingine Inaonyesha Taa za barabarani Usiku.
Uwanja wa Wazi wa Kupumzika wa Mashujaa.
………………………………………………………….
Na Judith Mhina- Maelezo
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya
Tano, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, ya kuifanya
Manispaa
ya Mtwara Mikindani kuwa eneo la uwekezaji, utalii na kuimarisha ukanda
wa uchumi wa Kusini imetimia.
Hayo amesema Mhandisi wa Manispaa
ya Mtwara Mikindani Isaac Mpaki alipofanya mahojiano na Idara ya
Habari-Maelezo hivi karibuni, ambapo ameeleza mambo yaliyofanyika katika
Miradi Kimkakati ya Kuendeleza Miji Tanzania (TSCP), uliotumia kiasi
cha shilingi milioni 767.7 na kuleta sura mpya ya manispaa husika,
yenye chimbuko la nishati ya gesi, lango kuu la bandari ya Mtwara,
kiwanja kikubwa cha ndege na barabara zinazofungua milango ya kiuchumi
ndani na nje ya nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.
“Manispaa yetu imebadilika ambapo
kwa sasa inavutia na kupendeza kutokana na miundombinu ya barabara
iliyojengwa ikiwa ni pamoja barabara ya Shangani na Chuno yenye urefu wa
kilometa 2.4. Barabara hiyo inapita pembezoni mwa soko kuu la Mtwara
Chuno, lililopo mtaa wa Ligula ‘A’ ambalo limejengwa kwa gharama ya
shilingi bilioni 5.6, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 10,200,
vizimba vya biashara 336, maegesho ya magari 81, maeneo ya kupakia na
kushusha mizigo saba, maeneo ya kuuza chakula manne na maeneo ya
biashara za jumla mawili” amesema Mpaki.
Aidha, soko hilo lina stoo tatu
za kuhifadhi kuku, maeneo ya bucha matano, ofisi nne vyoo vya kulipia
ndani ya maeneo manne yenye matundu sita kila moja ,ambapo inakadiriwa
kuwa wafanya biashara 400 wataweza kufanya biashara ndani ya soko kwa
wakati mmoja.
Akionyesha uwezo wa soko la Chuno
nje ya jengo, Mhandisi Mpaki amesema kuwa eneo la kiwanja cha soko la
Chuno lina ukubwa wa ekari 3.9, lenye thamani ya shilingi milioni
237,283,800, ambapo linatoa nafasi nje ya jengo kwa kuwekwa mabanda ya
biashara iwapo itaruhusiwa kufanya hivyo katika suala zima la kutoa
huduma za biashara mbalimbali kwa umma wa Mtwara.
“Soko la Chuno lina faida nyingi
ikiwemo kupunguza muda wa wananchi kusafiri kwenda nje ya mji sokoni kwa
ajili ya kutafuta mahitaji mbalimbali, kuongeza fursa za
wafanyabiashara wadogo kwa kuwawezesha kuwa na sehemu maalum ya kufanya
biashara ikiwa ni pamoja na kuwa na mji wa kisasa unaovutia na wenye
mandhari safi yenye kuthaminisha mji wa Mtwara huku Manispaa ikiwa na
chanzo cha mapato cha uhakika” amethibitisha Mhandisi Mpaki.
Akifafanua maboresho yaliyofanyika
katika Manispaa hiyo, Mhandisi Mpaki amesema kuwa pamoja na soko kuu
la kisasa la Chuno, kuna bustani za kuvutia zilizoboreshwa katika maeneo
matatu ya wazi yanayotoa huduma muhimu kama vile kuwekwa sehemu za
michezo kwa wakubwa ambako kuna viwanja vya basketball na Volleyball,
michezo kwa watoto, bwawa la kuogelea, mahali pa kupumzika penye sanamu
za wanyama, jukwaa, hoteli, migahawa, vioski vya vinywaji baridi,
maeneo ya kuegesha magari na ofisi za watumishi wa manispaa. Bustani ya
Mashujaa ina ukubwa wa mita za mraba 37.154, ikiwa imejengwa kwa
gharama ya shilingi bilioni 1.2, ambapo bustani ya Tila ambayo ni
bustani mbili zilizounganishwa kuwa moja, iliyopo mtaa wa Rahaleo yenye
mita za mraba 7,270 imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 996. Pia
katika uboreshaji huo kuna ujenzi wa stendi ya Mikindani, pamoja na
mfereji mkuu wa kupeleka maji baharini wenye urefu wa kilometa 2.6.
Aidha, Mtwara ina barabara
nyingine za lami kama COTC yenye urefu wa kilometa 0.9, barabara ya
Senegal yenye urefu wa kilometa 0.8, barabara ya Mikindani yenye urefu
wa kilometa 0.5 na kufanya barabara zilizojengwa kuwa na urefu wa
kilometa 22.09, hivyo jumla za barabara za lami katika halmashauri kuwa
ni kilomita 43.50. Barabara zote zina taa za barabarani zinazofanya
manispaa ya Mikindani kuwa na wafanyabiashara wadogo wengi zaidi nyakati
za usiku ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia wafanyabiashara hao ulinzi
wa mali zao kutokana na uwepo wa mwanga wa kutosha.
Akielezea faida nyingine za
uboreshaji wa Manispaa hiyo Mhandisi Mpaki amesema “Kwa sasa kuna
mandhari nzuri katika manispaa, usafi wa mji umerahisishwa ambapo kuna
utaratibu mzuri wa kusafisha mji na wananchi kulipia uzoaji wa takataka
ambazo zinapelekwa kwenye dampo la kisasa. Jambo hili limepunguza
kiwango cha magonjwa ya mlipuko katika mji huu na kuongeza usalama wa
mji kutokana na uwepo wa taa za barabarani zenye kuwafanya wananchi
kufanya biashara nyakati za usiku na kuwawezesha kutembea wakati wote
bila hofu”.
Uboreshaji wa barabara na stendi
ya Mji Mkongwe wa Mikindani Mtwara ambao ni maarufu kwa Utalii wa
majengo ya kale yenye zaidi ya miaka 120 umezidi kung’arisha mandhari ya
Manispaa hiyo ambayo imehifadhi historia ya wavumbuzi kama vile Dkt
David Livingstone, Waarabu waliotembelea Pwani hiyo katika kufanya
biashara ya utumwa, Wajerumani walioweka ngome yao Mikindani na
kuendesha utawala wao, pamoja na historia ya Uhuru wa Tanganyika ambapo
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifika Mikindani mwaka 1955 katika
harakati za kudai uhuru na kuhamasisha Watanganyika kuunga mkono chama
cha Tanganyika African Union na baadaye Tanganyika African National
Union (TANU)
Katika suala zima la kuweka
mazingira mazuri ya uwekezaji, Manispaa ya Mikindani imehakikisha uwepo
wa hospitali ya Rufaa ya Mitego ya Kanda ya Kusini itakayotoa huduma
katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Uwepo wa hospitali hii ni fursa
pekee ya kwa wawekezaji na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi
kuhakikisha usalama wa afya zao wawapo katika Kanda hiyo. Hospitali
imejengwa pembezoni mwa bahari ya Hindi, katika lango la bahari la Mji
Mkongwe wa Mikindani, Kata ya Mitego , mtaa wa Rahaleo.
Vilevile changamoto ya mafuriko
katika manispaa imeondolewa kutokana na ujenzi wa mifereji ya maji
iliyopita katika Kata ya Vigaeni, Chikongola, Majengo, Reli, na Likombe,
ikiwa ni pamoja na ongezeko la thamani ya ardhi na pango la nyumba na
maeneo ya biashara kando mwa barabara zilizojengwa.
“Hakika tunaona bahati tuliyoipata
katika Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani, kwa dhati kabisa naishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhakikisha imefanya maajabu haya
yanayoonekana leo. Haikuwa rahisi kwa Mkoa wa Mtwara kupata maendeleo
yote haya kwa muda mfupi ndani ya miaka mitano Njooni muone Mtwara
umekuwa Mji wa utalii na kivutio kwa uchumi”, amesema Mpaki.
Kutokana na uboreshaji huo,
Halmashauri hiyo imefanikiwa kutengeneza ajira nyingi kwa wananchi
hususan vijana na wanawake ambao ni wafanyabiashara wakubwa ikiwa ni
pamoja na kuwafanya wakulima kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya
uhakika. Miradi yote hiyo itasababisha kuongezeka kwa kodi na mahitaji
ya leseni za biashara.
MWISHO
No comments:
Post a Comment