Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa mara ya kwanza
amewafanyia usaili wahitimu wa taaluma ya Sheria kwa ajili ya kuwapokea
na kuwakubali kuwa Mawakili kwa njia ya Mtandao ‘Video Conference’.
Akizungumzia
kuhusu usaili huo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Messe Chaba, alisema usaili huo unafanyika
baada ya wahitimu hao, kufanya maombi ya kukubaliwa kuwa mawakili kwa
mtandao na kukidhi vigezo vinavyotakiwa na Baraza la Elimu ya Sheria.
‘‘Tumetumia
njia hii ya mtandao ili kuendena na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) na kuliishi agizo la Jaji Mkuu alilolitoa
katika hotuba yake ya kilele cha Siku ya Sheria nchini Februari Mosi,
mwaka 2018, ambapo aliwataka Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama
kubadili fikra na mtazamo ili kujiandaa na kujiimarisha kwenye matumizi
ya TEHAMA katika karne hii ya 21, ikiwa ni hatua ya kurahisisha
utendaji kazi wetu. Tumefanikiwa kutumia njia vizuri kwa siku na tuna
wahitimu takribani 80 wanaofanyiwa usaili, ’’ alisema Mhe. Chaba.
Alisema usaili huo, umeanza kufanyika Juni 23, mwaka huu na utamalizika Julai 3, mwaka huu.
Chaba
ambaye pia Katibu wa Baraza la Elimu ya Sheria, alisema njia hiyo ina
faida kwa wanataaluma hao, kwa kuwa inawapunguzia gharama za usafiri,
malazi, muda na usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa wa kusafiri
Jijini Dar es Salaam ili kufika kwenye ofisi za Jaji Mkuu kwa ajili
ya kufanyiwa usaili huo.
Aliongeza
kuwa usaili huo umekuwa ni fursa kwa Mahakama kwa kuwa umeongeza
matumizi ya TEHAMA hususan kipindi ambacho dunia na nchi ya Tanzania
inakumbwa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu, COVID 19
unaosababishwa na virusi vya Corona, ikiwa ni hatua mojawapo za kuepuka
maambukizi dhidi ya tatizo hilo.
‘‘Mchakato
wa kuwapata wanataaluma hao ulifanyika mwezi Aprili na Mei, lakini
hufanyika mara mbili kwa mwaka, ambapo utafanyika tena Novemba na
Desemba mwaka huu. ‘‘Wanataaluma hawa walituma maombi katika baraza
hili, kuanzia Aprili Mosi mwaka huu hadi Mei 14, mwaka huu kwa ajili ya
kuomba kuwa mawakili, hivyo jumla yao walikuwa 651 na waliokidhi vigezo
ni takribani 613 ambao ndio tunawafanyia usaili,’’ alisema Mhe. Chaba.
Alivitaja
baadhi ya vigezo vya kukubalika katika usaili huo ni kuleta maombi,
kumaliza Shule ya Sheria (Law School), kuwasilisha vyeti, kupitia elimu
ya Diploma ya Sheria, Elimu ya Sheria ya Chuo Kikuu, kuleta matokeo ya
taaluma hiyo, kuwa na tabia njema, hati ya kiapo cha majina, na barua ya
utambulisho wa kazi.
Wanataaluma
hao baada ya kumaliza usaili na kufaulu,wanatarajiwa kukubaliwa na
kupokelewa kuwa Mawakili kwenye Sherehe ya 62 itakayofanyika Julai 10,
mwaka huu. Aidha, mawakili hao wakishakubaliwa wataingizwa katika Mfumo
wa Kusimamia Mawakili (TAMS). Sherehe hizo zilianzishwa rasmi mwaka
1986.
Maeneo
yanayotumika kufanya usaili huo ni Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es
Salaam watahiniwa (438), Arusha (46), Tanga (watano), Tabora (16),
Mtwara (watatu), Dodoma (23), Mbeya (27) na Mwanza (44). Awali
wanataaluma wa fani ya Sheria walikuwa wakikutana na Jaji Mkuu ana kwa
ana kufanyiwa usaili.
picha namba 1.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa ofisini kwake
Jijini Dar es Salaam akimfanyia usaili mhitimu wa Shule ya Sheria kwa
njia ya mtandao maarufu kama ”Video Conference” ikiwa ni maandalizi ya
kuapishwa kuwa Wakili .
No comments:
Post a Comment