Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabirle akizungumza
mara baada ya kukagua shamba darasa la malisho bora ya mifugo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singi
Muonekano wa shamba darasa la
malisho bora ya mifugo lililopo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mbegu
za moja ya aina ya malisho alipotembelea shamba darasa la malisho
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singi
Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na
Ugani Dkt. Angello Mwilawa (kushoto) na Afisa Mifugo Mkuu Bibi Bezia
Rwongezibwa wote kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakionesha malisho ya
mifugo ambayo yamevunwa tayari kwa kuhifadhiwa.
********************************
Na. Edward Kondela
Serikali imesema
itahakikisha changamoto ya malisho ya mifugo nchini inatatuliwa kwa
wafugaji kuelimishwa namna ya kulima malisho bora yenye tija kwa mifugo
yao.
Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole
Gabriel amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akikagua shamba darasa
la malisho ya mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya
Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida na kubainisha kuwa, serikali itaendelea
kuwatia moyo wafugaji ili wawe na mashamba ya malisho bora ya mifugo
yao pamoja na kuhakikisha uwepo wa maji ya kutosha ya kunyweshea mifugo
mambo ambayo yatasaidia kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na
watumaji wengine wa ardhi.
“Makatibu tawala
wa mikoa mingine waige mfano wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa mashamba ya
malisho ya mifugo, lazima iendelezwe kwenye mikoa mingine. Wafugaji
wengine nchini wakiweza kutenga maeneo yao na kupewa mafunzo na kulima
malisho yao itakuwa njia sahihi pia ya kuwasaidia wafugaji kuondokana na
hali ya kuhamahama ya mifugo yao kutafuta malisho.” Amesema Prof.
Gabriel
Aidha Prof.
Gabriel ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa kuhakikisha anashirikiana
na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kutunza mashamba hayo
dhidi ya uvamizi wowote wa watu kukata malisho hayo au kuingiza mifugo
yao kulisha bila utaratibu unaokubalika.
Pia amewataka
wafugaji kote nchini kufahamu nchi yeyote duniani inaendeshwa kwa
sheria, taratibu na kanuni hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi haitamtetea
mfugaji yeyote atakayeenda kinyume na sheria kwa kulisha mifugo yake
katika eneo au shamba la mmiliki mwingine bila kufuata utaratibu.
Katibu mkuu huyo
ameongeza kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha uwepo
wa mifugo bora nchini ambayo inatokana na kula malisho bora ya
kisayansi, ambapo badala ya kula wingi wa majani wale majani yaliyo
bora.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bw. Justice Kijazi
ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara
hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kusambaza
wataalam wake wa malisho katika maeneo mengine hapa nchini ili
kuwashauri wakulima kuwa na mashamba mengi ya malisho bora ya mifugo
ambayo yatakuwa na tija kwa wafugaji kwa kuwa na mifugo bora.
Bw. Kijazi
amefafanua pia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ina majosho 10 ya kuoshea
mifugo huku akiishukuru wizara kwa kuwapatia fedha ya kukarabati
majosho matatu na kuiomba wizara iwasaidie pia fedha nyingine kwa ajili
ya kukarabari majosho saba yaliyobaki ili wafugaji wengi zaidi katika
halmashauri hiyo waweze kuogesha mifugo yao.
Kuhusu idadi ya
mifugo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Kijazi
amesema kuna jumla ya mifugo takriban 600,000 ambapo ng’ombe wapo
350,000 mbuzi na kondoo zaidi ya 200,000 licha ya halmashauri kuwa na
changamoto ya kutokuwa na machinjio nzuri, ameiomba wizara kutoa msaada
wowote ili kuiwezesha halmashauri hiyo kuwa na machinjio nzuri na kisasa
kulingana na idadi ya mifugo iliyopo na hatimaye kuweza kuuza nyama
ndani na nje ya nchi.
Akibainisha
umuhimu wa uwepo wa mashamba bora ya malisho yanayotokana na kupandwa
kwa aina mbalimbali za nyasi zilizofanyiwa utafiti wa kisanyansi na
kuthibitishwa kuwa ni bora kwa malisho ya mifugo, Afisa Mifugo Mkuu
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bibi Bezia Rwongezibwa amesema wafugaji
wanafundishwa kulima, kupalilia, kuweka mbolea, kuvuna na hatimaye
kuhifadhi malisho hayo ambayo yatatumika wakati wa uhaba wa malisho.
Nao baadhi ya
wananchi wakiwemo wa vikundi vya wajasiriamali ambao wamejitolea kulima
mashamba darasa kwa ajili ya mifugo kutoka katika Kijiji cha Mahambe
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, wamesema Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imewatia moyo namna ya kulima malisho na kuyahifadhi
ambapo baadhi yao wameanza kupanda malisho hayo ili wapate mifugo bora
wakiwemo ng’ombe.
Wamesema uwepo wa
mashamba darasa katika eneo lao ni darasa tosha kwao kwa kuwa wataweza
kujifunza zaidi kuhusu malisho bora ya mifugo na hatimaye kulima katika
mashamba yao.
Katika hatua
nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo
Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati akikagua shamba darasa la malisho ya
mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi Mkoani Singida, amezungumzia pia kuhusu uwepo wa virusi vya
corona nchini vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ambapo amebainisha
kuwa kwenye sekta ya mifugo wizara imeweka mkazo mkubwa kwa jamii ya
wafugaji kote nchini kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kukabiliana na
janga hilo kwa kuchukua tahadhari, kufanya maombi pamoja na kufanya kazi
kwa bidii.
No comments:
Post a Comment