Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara, mhandisi Zephania Chaula akikabidhi funguo ya moja ya pikipiki
sita kwa Ofisa Tarafa ya Moipo Joseph Mtataiko zilizotolewa na Rais
John Magufuli.
……………………………………………………………………………………
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani
Manyara, Zephania Chaula amekabidhi pikipiki sita
kwa ajili ya maofisa
wa Tarafa wa wilaya hiyo walioahidiwa na Rais John Magufuli Juni 4 mwaka
jana.
Chaula akikabidhi pikipiki hizo
alisema maofisa tarafa wote sita wa tarafa za Naberera, Moipo, Emboreet,
Terrat, Ruvu Remit na Msitu wa Tembo wamepatiwa pikipiki hizo.
Aliwataka maofisa tarafa hao
kutumia nyenzo hizo kuhudumia jamii kwa kuwafikia kwa urahisi zaidi
tofauti na hapo awali kabla hawajakabidhiwa.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa
kutimiza ahadi yake aliyotoa Juni 4 mwaka jana baada ya kukutana na
maofisa tarafa wa nchi nzima na kuwaahidi kuwapatia pikipiki kila mmoja
kwa ajili ya kuzitumia kwenye majukumu yao.
Alisema pikipiki hizo zitakuwa
msaada mkubwa kwa viongozi hao kwani wilaya ya Simanjiro kijiografia ni
kubwa ina zaidi ya kilomita 21,000.
“Simanjiro ni kubwa mno mfano
tarafa ya Naberera ina ukubwa wa zaidi ya kilomita 8,000 na imezishinda
ukubwa baadhi ya wilaya zenye ukubwa wa kilomita 3,000 hivyo changamoto
ya ukubwa ipo,” alisema.
Aliwataka viongozi hao kuzitunza
pikipiki hizo kwa kuzitumia kwa matumizi waliyopewa na serikali na siyo
vinginevyo huku wakiepuka ajali za uzembe.
“Msitumie hizi pikipiki kama
bodaboda na kuanza kubebea abiria kwani mmepewa kwa sababu ya kuendesha
shughuli zenu za kila siku tarafani mwenu mfike kwenye kata zenu na
vijiji vyenu,” alisema Chaula.
Ofisa Tarafa ya Moipo Joseph
Mtataiko akizungumza kwa niaba ya maofisa Tarafa wenzake amemuahikishia
mkuu huyo wa wilaya kuwa watafanya kazi zao kwa wepesi zaidi tofauti na
awali.
“Kupitia usafiri huu tutazidi
kuchapa kazi zaidi na zaidi kwani utawasaidia kufika katika maeneo yao
hasa sehemu za pembezoni wanazozisimamia kiutendaji hususani tarafa ya
Moipo.
“Pamoja na hayo tunamshukuru na
kumpongeza Rais Magufuli kwa kutimiza ahadi yake kwetu kwani Juni 4
mwaka jana alitualika Ikulu jijini Dar es salaam na kutuahidi kupatiwa
pikipiki,” alisema.
No comments:
Post a Comment