Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula (wa
kwanza kushoto) akifurahia jambo wakati anawasili ofisi za Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote, Dodoma. Kulia kwake anayemsikiliza ni Mtendaji
Mkuu wa Mfuko huo, Justina Mashiba
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba, akimkaribisha Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.
Zainab Chaula (aliyeketi) alipowasili kwenye ofisi za Mfuko huo
kujitambulisha na kuzungumza na bodi na Menejimenti ya Mfuko huo, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula
akizungumza na wajumbe wa bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote,
Menejimenti ya Wizara yake na ya Mfuko huo kilichofanyika kwenye ofisi
za Mfuko huo, Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote, Dkt. Joseph Kilongola (aliyevaa tai) akiagana na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula (wa kwanza kushoto) baada ya kuzungumza
na bodi hiyo kwenye ofisi za Mfuko huo, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula
(mwenye ushungi wa bluu) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa
Menejimenti ya Wizara yake na ya Mfuko huo. Wa kwanza kulia kwake ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Dkt. Joseph Kilongola na wa kwanza
kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Justina Mshiba
Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote na Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania, Mhandisi Francis Mihayo, akijitambulisha kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.
Zainab Chaula (hayupo pichani) wakati wa kikao chake na wajumbe wa bodi
hiyo kilichofanyika Dodoma
………………………………………………………………………………………………..
- Aipongeza kwa kufikisha huduma za mawasiliano ya simu kwa wananchi
- Bodi yamweleza changamoto ya mawasiliano ya redio ya uhakika
Na Prisca Ulomi, WUUM, Dodoma
Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab
Chaula amepokea changamoto kutoka kwa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) ya huduma za mawasiliano ya redio ya uhakika kwenye maeneo
mbali mbali nchini
Dkt. Chaula amepokea changamoto
hizo leo wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa wajumbe wa Bodi ya
UCSAF na kuzungumza nao kuhusu utekelezaji wa majukumu ya UCSAF ya
kupeleka huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini,
yasiyo na mvuto wa kibiashara, mipakani na kwenye hifadhi za taifa na
mapori ya akiba.
Ameipongeza Bodi hiyo kwa
kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini ambapo
hadi sasa asilimia 94 ya wananchi wanawasiliana. Aidha, ameiarifu Bodi
kuwa wanafahamu changamoto walizonazo na wana majibu ya namna ya kutatua
changamoto hizo na yeye yuko tayari kupokea ushauri wa kutatua
changamoto walizonazo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata
huduma za mawasiliano ya simu na redio kwa kuwa redio inasikilizwa na
wananchi walio wengi waishio vijijini bila kusahau usafirishaji wa
vifurushi na vipeto kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kutumia
anwani za makazi na postikodi zilizopo nchi nzima pamoja na kuhakikisha
kuwa huduma za tiba mtandao zinafika kwenye hospitali za ngazi ya
kitaifa, rufaa na hata ngazi ya wilaya kwenye halmashauri 184 zilizopo
nchini kote
Akizungumza na wajumbe wa Bodi
hiyo, Dkt. Chaula amesema kuwa wote tunategemeana iwe unafanya kazi
Serikalini au sekta binafsi kwa kuwa wote tunahudumia wananchi na
wanatutegemea, hivyo kila mmoja atimize wajibu wake kwa kuwa
tunachohitaji sisi ni mawasiliano
Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Dkt.
Joseph Kilongola amemshukuru Dkt. Chaula kwa kuwatembelea na
kujitambulisha kwao na kuwapa mwelekeo, kuonesha utayari wa kufanya kazi
kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano
kuendana na matakwa ya Serikali ya kuhudumia wananchi wake
Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF
amempongeza Dkt. Chaula kwa kufika na kuzungumza na wajumbe wa Bodi na
wa Menejimenti ya UCSAF kwa kuwa ameonesha njia, umoja na ushirikiano
ambapo taasisi ilibidi ifike kujitambulisha kwake
Justina amesema kuwa, Menejimenti
ya UCSAF iko tayari kushirikiana na Bodi na viongozi wa Wizarani ili
kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano ya redio ya uhakika; usambazaji
wa vifurushi na vipeto kupitia anwani za makazi na postikodi; na tiba
mtandao zinaongezeka na zinafika kwenye hospitali mbali mbali nchini ili
kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma za tiba kwa ajili ya
kuboresha afya ya wananchi waishio maeneo mbali mbali nchini
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe
wengine wa Bodi ya UCSAF, Gogfrey Simbeye, ambaye anawakilisha sekta
binafsi kwenye Mfuko wa UCSAF, ameishukuru Serikali kupitia UCSAF kwa
kutambua mchango wa sekta binafsi na kuishirikisha sekta hiyo katika
kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi
Simbeye amesema kuwa Sekta ya
Mawasiliano kupitia UCSAF imetekeleza vema sera ya Ushirikiano Baina ya
Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership –PPP) kwa kutoa
ruzuku kwa kampuni za simu kujenga minara ili kufikisha huduma za
mawasiliano kwa wananchi
Dkt. Chaula ameanza ziara hiyo ya
kujitambulisha na kuzungumza na taasisi zake za Sekta ya Mawasiliano na
wadau wake ili kuhakikisha kuwa watendaji wa Wizara, taasisi na wadau
wanashirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia kuwa Sekyta ya Mawasiliano ni
Sekta nyeti na mtambuka ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Sekta hiyo
inaendelea kukua, kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa
maendeleo ya taifa letu
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment